Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Dotto Biteko na Naibu wake Mheshimiwa Stanslaus Nyongo kwa kazi nzuri wanayoifanya. Mheshimiwa Dotto, tunajua mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe; hayo mawe endelea kuyapokea, piga kazi kama unavyopiga msaidieni Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tarehe 22 Januari, Mheshimiwa Rais aliitisha kikao cha wadau wa madini wote Tanzania pale Dar es Salaam; na wadau wale walifurahi sana na kumshukuru Mheshimiwa Rais wa wanyonge kwa kuwajali na kuwaona na kuona umuhimu wao na kuwaita.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa changamoto ambazo wadau wa madini waliziomba kwa Mheshimiwa Rais; changamoto kubwa ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ilikuwa asilimia 18 na kodi ya zuio asilimia 5. Mheshimiwa Rais aliyapokea na akaahidi atayafanyia kazi. Serikali sikivu ya Awamu ya Tano ilileta Bungeni tarehe 9 Februari kufanya marekebisho Muswada wa Sheria wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na hii ya zuio la asilimia tano, ilipitishwa na Mheshimiwa Rais alisaini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini mpaka sasahivi zuio ndilo ambali limepita lakini mpak asasahivi wachimbaji wanateseka. TRA bado wanachaji ongezeko la VAT la asilimia 18, sasa mimi najiuliza, kama Bungeni tulipitisha, Mheshimiwa Rais alisaini, wao ni nani? Najua Waziri wa Fedha ananisikia, jamani hawa wafanyabiashara wa madini wanateseka, na mnawachonganisha na Mheshimiwa Rais, alipitisha na Bunge tulipitisha, nani mwingine zaidi wa kuacha kutekeleza haya maagizo? Waziri wa Fedha unanisikia, Waziri wa Madini unanisikia na leo nashika shilingi kwa sababu Bunge tulishapitisha. Hawa wafanyabiashara wazawa wana mitaji midogo ukilinganisha na wageni ambao hii asilimia 18 ya VAT haiwahusu, inawahusu hawa hawa wafanyabiashara wetu wadogo.
Mheshimiwa Spika, naomba sana Serikali uangalie na Mheshimiwa Rais huko ulipo unisikie, ulichokisaini mpaka sasa hivi wafanyabiashara wa madini hawajatendewa haki. kwa hiyo Mheshimiwa Rais siku ile ni kama siku nzima amekaa na wale wafanyabiashara umepoteza muda kwa sababu hawajatekeleza. Tunaomba watekeleze haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze moja kwa moja mchango wangu katika export permit, kibali cha kusafirisha madini. Sheria ya Madini inatamka kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ndiye mwenye mamlaka ya kusaini vibali vya kusafirisha madini. Katibu Mtendaji wa Tume yupo Dodoma. Wafanyabiashara wengi nchini wako sehemu mbalimbali. Inachukua muda mrefu Katibu huyu kuletewa hapa Dodoma mpaka kusaini madini yaweze kusafirishwa nje. Hapa Tanzania inachukua hata wiki ilhali wenzetu Kenya wanachukua dakika 10.
Naomba kila mkoa angeteuliwa mtu ambaye mnamuona anafaa aweze k ufanya hii kazi kuliko kukaa kusubiri huyu Katibu Mtendaji wa Tume, akiwa hayuko, akiumwa, kazi zinasimama. Hivi jamani, hii Serikali ya Awamu ya Tano kuna kitu kama hiki? Kazi zisimame kwa ajili ya mtu mmoja? Haiwezekani! Mheshimiwa Waziri, naomba uliangalie hili, wawepo watu ambao wanaweza kufanya hii kazi, sio mtu mmoja tu wamtegemee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeona Wizara ya Mazingira imepiga marufuku mifuko ya plastiki. Nawapongeza sana kwa sababu ni katika suala zima la kuhifadhi mazingira; lakini wafanyabiashara wa madini hasa ya Tanzanite wanasafirisha madini yao kwenda nje kwa mifuko ya aina hii ambayo kama imepigwa marufuku madini haya ambayo yanakuwa yamesafishwa, yameshawekwa katika ubora yataharibika. Kwa hiyo wenyewe bila kutumia mifuko kama hii tutaharibu biashara yao. Naomba, najua hii Serikali ni sikivu na iko radhi kuongea na hawa wafanyabiashara, iangalie ni jinsi gani wao waruhusiwe hata kutumia mifuko ambayo wamekuwa wakitumia bila kuathiri mazingira kwa sababu kwanza mifuko yenyewe inaenda nje haikai hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Arusha kulikuwa na maonesho ya madini tangu mwaka 1992, yalikuwa yanaitwa Arusha Game Fair lakini cha kusikitisha…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Bahati mbaya dakika tano zimeisha Mheshimiwa Catherine.
MHE. CATHERINE V. M AGIGE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia 100. (Makofi)