Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu. Pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Naomba nami nichangie mchango wangu kwenye Wizara hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, mwaka 2017 uliunda Kamati ya Kuchunguza Madini ya Tanzanite na Madini ya Almasi na nilikuwa miongoni mwa wajumbe kwenye Kamati ile. Naomba nizungumze yale mapendekezo ambayo Kamati ilipendekeza utekelezaji wake umekuwa kwa kiasi gani. Nimshukuru Mheshimiwa Dotto Biteko, Waziri wa Wizara hii kwa sababu ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa ile Kamati ya Tanzanite na kwa kiasi kikubwa hotuba yake imegusagusa mambo hapa nimeweza kuyasikia, lakini nataka niweze kufahamu utekelezaji hasa ukoje.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, jambo la kwanza, tuliona pale Mererani pale ambapo kuna Mgodi wa Tanzanite kwamba kumekuwa na mrundikano wa leseni nyingi sana za wachimbaji hawa wadogowadogo ambao amewataja na tuliweza kubaini kwamba kuna leseni zaidi ya 900 pale ambazo zimetolewa na Serikali na Wizara na kukawa na changamoto kubwa kule chini, wale wachimbaji wadogowadogo wanavyochimba, kwamba wanafikia sehemu inaitwa mtobozano, wanatobozana kule chini wanakutana wanauana huko chini, watanzania wengi wanakufa.

Mheshimiwa Spika, napenda kujua je, pendekezo lile Mheshimiwa Waziri limetekelezwa kwa kiasi gani kwamba, wale Watanzania wanaokufa kutokana na idadi kubwa ya leseni ndogondogo zilizotolewa pale Mererani na kule chini wanauana kwa sababu wanakutana kule chini na wakati mwingine wanakutana na ule mgodi wa TML na wanauawa kule chini, Watanzania wengi sana. Suala hili limefikia wapi na utekelezaji wake ukoje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine naomba kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri hapa, kwamba amezungumza suala la one stop center kwamba itajengwa katika ule ukuta wa Mererani pake Arusha. Utaratibu wa hii one stop center ukoje, unakwenda kujenga kwa ajili ya kuuza yale madini yetu kwa sababu ya wanunuzi ambao wanakuja kununua kutoka nje ya nchi au tunakwenda kujenga zile smelters za kuchenjua yale madini. Kwa sababu tatizo limekuwa ni kubwa sana kwamba uchenjuaji unafanyika India kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, hili jambo Kamati ilizungumza sana, kwamba Watanzania wanakosa ajira sana kwa sababu yake madini yetu hayachenjuliwi hapa Tanzania, hasa madini ya Tanzanite na kwa kiasi kikubwa yanachenjuliwa kule India na taarifa zinaeleza kwamba India kuna watu zaidi ya laki sita wamepata ajira kutokana na uchenjuaji wa madini ya Tanzanite ambayo yanatoka Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kujua seriousness ya Serikali juu ya kuchenjua madini haya pale Mererani Arusha. Kwa hiyo, hiyo smelter one stop center inakwenda kutoa suruhisho la kudumu, kwamba Watanzania sasa tuweze kuchenjua wenyewe na kule India kuwe hakuna tena ajira ya kuchenjua haya madini ya tanzanite.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine naomba kufahamu, Mheshimiwa Waziri atueleze, wakati tunapitia zile taarifa mbalimbali za watoa taarifa mbalimbali tulielezwa kwamba kutokana na utoroshwaji wa madini ya tanzanite ambao unafanyika kwenye Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, kuna njia za panya zaidi ya 400 ambazo madini haya yanapita kuelekea kule Kenya na hili limepelekea Watanzania wenyewe tuwe ni watu wa mwisho kunufaika na madini haya ambayo yanapatikana Tanzania tu duniani, sisi wenyewe tukawa watu wa mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wa kwanza ni kule yanakokwenda Marekani, ambako ni Tucson kule Marekani ndiko yanakouzwa na wanaopeleka kule ni Wahindi, ambao wanakwenda kuuza kwa kiasi kikubwa sana haya madini! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hao ndiyo wanufaikaji wa pili, wanufaikaji wa tatu ni watu wa Afrika Kusini, ambako hii kampuni ya TML ndiyo inaonyesha kwamba uhusiano wake mkubwa na nchi ya South Africa ndiko wanakotoka kule, lakini wengine ni Wakenya, wa nne, na sisi wenyewe ni wa mwisho watu Watanzania. Sasa hili limepelekea kwa sababu kuna njia nyingi za panya, haya madini yanatoroshwa katika nchi ya Tanzania kuelekea nchi ya Kenya na taarifa zinasema, Kenya imeendelea baadhi ya miji imekuwa ni mikubwa, imekuwa na maendeleo ukiwemo Mji wa Naivasha kwa sababu ya madini ya tanzanite yanayotoroshwa kutoka Mererani Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kujua, hizi njia 400, kwa sababu imeelezwa hapa kwenye na taarifa ya Kamati na ya Upinzani imezungumzwa pia kwamba personnels wenyewe hawatoshi. Mpango wa Wizara ukoje wa kuajiri personnel ya kuweza kuhakikisha kwamba tunadhibiti hizi njia za panya, njia 400 zilizopo pale Arusha na kule Mkoa wa Kilimanjaro. Mheshimiwa Waziri naomba atupe maelezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, kulikuwa na suala hili la STAMICO, kwamba, STAMICO tumekuwa tunazungumza kwa muda mrefu sana, kwamba ni taasisi ya Serikali ambayo imekosa nguvu, aidha nguvu ya kifedha ama nguvu ya kiusimamizi, kwamba hata wale watendaji wake wamekuwa ni watu ambao tulivyoenda kuangalia wizi ambao ulikuwa unafanywa na watu wa TML, pale Mererani Arusha, yaani zinaibiwa ndoo sita za madini, yule mtu wa STAMICO yuko palepale ndani, ukiangalia ile clip inaonesha kabisa mtu wa STAMICO amewekwa pembeni kule, watu wanafanya sorting ya madini, ndoo sita zinaibiwa, yeye yuko palepale, ambaye ndiyo tegemeo la Serikali, tegemeo la Watanzania kwamba aweze kusimamia madini yetu pale ili Serikali iweze kupaya gawio, iweze kupata tozo, iweze kupata kila kitu, yeye yuko palepale, ndoo sita za madini zinaibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atuambie, kwamba Watanzania hawa tunaowapeleka kwenye kampuni hii ya Serikali, ambayo sisi tunaitegemea, sasa hivi wameweka mkakati gani wa kuweka personnel ambao wana uwezo wa kusimamia madini yetu ili Serikali isikose mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi STAMICO tuna asilimia pale 49 katika ile kampuni ya TML, kwamba ushirikiano wa Serikali tunategemea kampuni hiyo, kwa hiyo ni lazima tuwe na watendaji ambao wana capacity kubwa ya kuweza kuwazuia wale wageni, wale akina Riziwani Ulaa,na wengine wale wenzao ambao walikuwa wanaiba yale madini yetu takribani ndoo sita na Serikali kukosa kabisa gawio na kukosa kabisa mapato.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna hisa moja ambayo ilikuwa imezungumzwa sana katika ile kampuni ya TML, tunaita hisa kivuli, ya mtu mmoja anaitwa Amy Mpungwe, hii hisa imekuwa haielewekieleweki, kwamba hiyo hisa hata gawio nalo halipatikani kwa huyo Amy Mpungwe, ambaye ni Mtanzania, aliingia kwenye ile TML. Sasa Mheshimiwa Waziri tunaomba atupe taarifa, tumezungumza suala la local content hapa, kwamba kuwawezesha watanzania waweze kujihusisha na rasilimali za Tanzania na sheria hii inaeleza asilimia 25 Watanzania waweze kuhusishwa katika ajira na katika kumiliki rasilimali za Watanzania. Ile hisa moja iliyopo kwenye kampuni hii ya TML, ya Amy Mpungwe ambaye ni Mtanzania, bado inaendelea kuwa hisa kivuli, hisa hewa au namna gani. Tunaomba atupe maelezo Mheshimiwa Dotto Biteko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, naomba kuzungumza, mwaka jana nilieleza hapa suala la madini ya blue sapphire, ambayo kwa kiasi kikubwa duniani sasa hivi yanaonekana kwamba yanazalishwa kutoka nchi ya Sri Lanka, lakini ukija kule kusini, Ruvuma pale Tunduru, madini ya blue sapphire yanapatikana kwa kiasi kikubwa sana na wanunuzi wa madini haya hapa Tanzania ni watu wa Sri Lanka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niiombe Serikali, kwa sababu haijaweka utaratibu mzuri, haijaweka utaratibu wa kuwa wa certificate of orgin, yaani kuoesha kwamba madini haya yanatoka Tanzania, kwa sababu yakinunuliwa na wale wa Siri Lanka, wanapeleka kule Sri Lanka, wanajumuisha na ya kwao, halafu ni madini yenye thamani sana duniani, blue sapphire, halafu wanasema haya madini yote yanatoka Sri Lanka, wakati mengi yake yanatoka kwetu Tanzania na haijulikani kama yanatoka Tanzania na yanatoka Tunduru Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, mwaka jana nilizungumza hapa hili suala kwamba aende Tunduru akaweke utaratibu mzuri, yale madini yetu yanayotoka pale Tunduru, yaweze kuonyeshwa kweli yanatoka Tanzania na yanatoka Tunduru badala ya kwamba yanajumuishwa kule dunia nzima inafahamu blue sapphire inatoka Sri Lanka pekee, kumbe siyo kweli. Namwomba Mheshimiwa Waziri na Wizara, hili suala waliangalie kwa jicho la kipekee kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, kuna suala hili Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa, kwamba tunahitaji kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo waweze kupata manufaa na hawa ni Watanzania na hawa ndiyo maskini ambao tunawazungumzia hapa, lakini ukienda Tanga leo hii hawa wachimbaji wadogo wamepewa leseni, lakini bado wanasumbuliwa sana na Askari wetu. Yaani wale wachimbaji wakubwa kwa mfano, ukienda kwenye maeneo ya Umba River, eneo la Kalalani, Mgombeni, Kigwase, Mwakijembe, wanatumwa wale watu polisi Askari wa….

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Maftah, nakushukuru sana.

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie, kidogo tu.

SPIKA: Haya haya.

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, nilichokuwa nasema, kwamba ukienda kule Tanga kwenye maeneo hayo niliyoyataja, wale wachimbaji wakubwa, wanawatuma Askari, kwenda kuwabugudha hawa wachimbaji wadogo ambao ni Watanzania kwenye maeneo yetu hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana Serikali kwamba hawa watu wana haki na wamepewa leseni zile za kisheria kabisa, waachiwe ili tuweze kuondokana na umaskini hapa nchini Tanzania. Ahsante sana. (Makofi)