Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, kwa sisi jamii tunaotoka kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo ni dhahiri kabisa tumepata Waziri ambaye Ofisi yako inaingilika kirahisi. Tuliyaona, kabla ya wewe kulikuwa na Mawaziri Maprofesa hapa siku unataka kukutana naye yaani inabidi uende kwa dobi ukafue hata suluari kwanza, lakini tunakuombea Mungu na uendelee na moyo huo kwa sababu unamsikiliza kila mtu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kwa kweli Wizara hii inafanya vizuri na sisi wapiga kura wetu ambao ni wachimbaji sidhani kama ukimsema vibaya Waziri Doto atakuelewa; tunahitaji tu kukushauri kwa machache ambayo pengine tunaona ukiyafanya utakuwa rafiki mzuri zaidi ya wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, kama alivyoeleza Mheshimiwa Kasu, tunaona kwenye maeneo yetu ya wachimbaji kuna shida kubwa sana ya watendaji, shida kubwa sana. Wachimbaji wadogo wengi wameitikia wito wa kulipa kodi lakini pale ambapo mtu anapotaka sasa afuate zile procedure za kulipa kodi kuwapata watendaji wa Wizara yako ni shughuli; inabidi mtu akae na carbon saa nyingine mpaka siku tatu risk wezi wako kule wanajua carbon imeshaiva. Sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri, kama Serikali haijakupa kibali cha kuajiri tunaweza kutumia njia ya dharura tu kama tuliweza kuchukua Wanajeshi wakaenda kuchukua kangomba kule Mtwara tunashida gani? Tumuombe Mheshimiwa Rais akupe Wanajeshi waende wakasimamie ni shida kubwa sana unakuta kwa mfano Geita kuna erosion plant labda 30 mpaka 50 watumishi wanane inawezekana vipi? Ni mateso makubwa. Mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri nimeona hata makusanyo ya Wilaya yangu ya Geita tuna kilo karibu 600 sasa hivi kwa miezi mitatu. Mheshimiwa Waziri mimi naangalia kabisa kwa macho yangu na uzoefu wangu hata theluthi bado hujakusanya dhahabu bado inaibiwa.
Mheshimiwa Spika, hebu nikushauri kwa sababu mimi ukikusanya sana wewe na mimi kwenye halmashauri napata pesa nyingi hebu jaribu hata miezi miwili chukua Wanajeshi tusambazie kule uone dhahabu itakayokuja, kuna dhahabu nyingi. Lakini nikuambie kingine ni kwamba watu wako pia si waaminifu ubovu unaanzia kwenye Ofisi yako humo humo kwa wasimamizi na nikuombe Mheshimiwa Waziri ushauri wangu tu pengine unapotaka kuajiri hawa wasimamizi wako Mikoani na Wilayani kuna chuo kile cha Jeshi kiko Kunduchi, nilizungumza hapa, kile cha NDC, hebu wachukue kwanza wakafundishwe uzalendo wa kuyalinda haya madini yetu pengine nakuona kila siku mara unafukuza mara unahamisha utaumiza kichwa unazofukuza ni hela dhahabu ni pesa watafutie utaratibu waende wakafundishwe pale miezi mitatu wakirudi hapo hawataiba, hawatashiriki huo wizi unaoendelea.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine kuna kitu inaitwa inspection fee inachukuliwa kule kwetu kwenye migodi yetu kule asilimia moja. Sasa nilikuwa tu nakushauri hii asilimia moja hebu jaribuni kuangalia hata theluthi ibaki kule mikoani. Leo Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Kamati ya Ulinzi na Usalama ndiyo tumemkabidhi majukumu yote; tukishafungua maduka tu tunawaachia walinzi wao kufukuzana na wezi wao halafu hawana kitu unampigia Mkuu wa Mkoa njoo kuna watu wanaiba madini anaanza kuomba mafuta kwa Mkurugenzi, hiki kitu si sawa, turudishieni hata kidogo ili Wakuu wetu wa Wilaya na Wakurugenzi na Wakuu wa Mikoa wale na fungu la kuwapa hata motisha wale watu wanaoenda kufukuzana na wezi kule kwenye machimbo usiku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, linguine, Geita hatujalipwa hela zetu, na wewe mwenyewe unafahamu. Mheshimiwa Nyongo amekuja Geita Mjini Nyamarembo, Magema na Katoma, kuna watu wamefanyiwa compensation miaka minane; na ninapata taarifa kwamba wanaanza kulipwa lakini hizo fidia wanazolipwa ni wamepunjwa nataka nijue kama mdhamini mkuu wa Serikali alishirikishwa kwenda kuhakikisha kwamba watu wetu wanapata pesa inayostahili na maeneo yao au na nyumba zao? Si vibaya Mheshimiwa Waziri mimi nikuambie na yeye wenyewe ulikuwa mjumbe wangu wa Kamati ya Siasa, nilivalia njuga kipindi kile 2013, mama Tibaijuka Mungu amsaidie sana alitusaidia watu walilipwa mabilioni ya pesa si vibaya mkachukua uzoefu wake alitumia njia gani watu wetu wakalipwa, nakushukuru sana. (Makofi)