Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Same Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuunga mkono hoja hii ya Wizara ya Nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 21, miradi ya kuzalisha umeme; mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji ya Mto Rufiji, megawatt 2,115. Kwanza nianze kusema kwamba naunga mkono hoja ya ujenzi wa mradi huu kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze kwa kumshukuru Mungu kutupatia maporomoko ya Mto Rufiji kwa sababu siyo kila nchi imepata maporomoko kama yale. Huku duniani kuna mabwawa makubwa 70 tu na ili bwawa liitwe kubwa linatakiwa liwe na sifa ya kuweza kufua umeme wenye zaidi ya megawatt 2,000. Bwawa letu hili ambalo linajengwa litakuwa na uwezo wa kufua umeme megawatt 2,115 na hivyo kuingia kuwa kwenye sifa ya kuwa mabwawa makubwa 70 duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende katika dunia, katika dunia kama nilivyosema mabwawa makubwa yapo 70, lakini ukienda duniani bwawa la kwanza kubwa liko China; la pili kubwa lipo Brazil na Uruguay na la tatu lipo Brazil. Twende Afrika, mabwawa ni mengi makubwa lakini tuanze bwawa kubwa mpaka sasa hivi linaloonekana ni kubwa ni bwawa lililopo Msumbiji bwawa la Cahora Bassa Dam ambalo linafua umeme kwa megawatt 2,075. Ina maana la kwetu linalojengwa litakuwa kubwa kuliko hili ambalo linaongoza sasa hivi. Bwawa lingine ni Aswan High Dam ambalo lipo Egypt ambalo linafua umeme megawatt 2,100, hili la kwetu ambalo linajengwa Rufiji litakuwa kubwa kuliko hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Ethiopia walianza kujenga bwawa ambalo litakuwa kubwa kuliko yote Afrika, Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance. Bwawa hili litakuwa na uwezo wa kufua umeme kwa megawatt 6,000 na lilianza tangu mwaka 2011 likikamilika litatumia dola bilioni 6.4, bado halijakamilika mpaka leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili bwawa linalojengwa hapo katika maporomoko ya Mto Rufiji; ni kweli kelele ni nyingi sana, upinzani ni mkubwa sana katika ujenzi wa bwawa hili lakini naiomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ielewe kwamba hakuna mtu yeyote duniani, hata haya mabwawa yote yaliyojengwa China, Brazil, Uruguay na wapi, si kwamba walijenga bila ya kuwa na changamoto, wote walipata changamoto kubwa sana na wote walipata upinzani, lakini naomba tuelewe kwamba huwezi kufanya jambo kubwa lenye manufaa katika nchi kama manufaa tutakayopata kutoka kwenye bwawa hili tunalojenga usiwe na changamoto, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yangu kwa unyenyekevu naisihi twendeni bila kusikiliza kelele zozote. Kwanza, ni lazima mwelewe kwamba moja ya tano ya umeme wote unaotumika duniani unatoka kwenye mabwawa haya 70. Sasa sisi tumepata nafasi ya kuwa na bwawa kubwa na sisi tuingie katika kuwa kwenye moja ya tano ya umeme unaozalishwa duniani, tunasikiliza kelele, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasihi sana, changamoto zilizopo tusisikilize kelele kushoto wala kulia, Serikali wasonge mbele kwa sababu kwanza ukiangalia umeme huu wa hydro ni rahisi. Pili huu umeme wa hydro utatusaidia kwa mambo makubwa mawili; kwanza; ajira kwa vijana wetu; pili. tayari tutakuwa na uwezo wa kuwa na uwekezaji mkubwa kwenye nchi hii. Sasa iwapo hatutakuwa watu tunaothubutu Serikali ya CCM, tunaogopa kelele za watu, tutakuwa wapumbavu. Naomba uthubutu huu uliooneshwa na Awamu ya Tano tusikatishwe tamaa na kelele zozote zile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Anne muda umeisha, ni dakika tano.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, nafikiri Watanzania wamenielewa. (Makofi/Vigelegele)