Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kupongeza hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, wajibu wetu ni kuwashauri kama tunavyowashauri kwenye mambo mengine; mkitaka yachukueni, lakini mnapoyaacha na madhara yake yanatokea kama yaliyotokea kwenye kikokotoo na kwenye mambo mengine. Kwa hiyo, Waziri na Naibu Waziri Mheshimiwa Jesca Kishoa ambaye leo ni birthday yake wamefanya kazi yao, wamelitendea haki Taifa lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge wa term ya pili, na tangu nimeingia kwenye Bunge hili Serikali ya Chama cha Mapinduzi haijawahi kutoa pesa za REA zote, mbali ya kwamba pesa zipo kwenye uzio na tunajua pesa zikiwekwa kwenye uzio zinatakiwa ziende zote kwa mujibu wa Katiba na kwa mujibu wa taratibu zetu tulizojiwekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naanza na awamu ya nne; mwaka 2010/2011 tulitenga bilioni 56.883, zilizotolewa ni bilioni 114; mwaka 2013/2014 zilitengwa bilioni 53.158, zilizotolewa ni bilioni 6.757; 2015/2016 zilitengwa bilioni 420, zilizotolewa ni bilioni 141, sawa na asilimia 34; 2017/2018, awamu ya tano sasa ya majigambo mengi… (Makofi)
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. ESTER A. BULAYA: …zilitengwa bilioni 499, zimetolewa bilioni…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester, subiri. Taarifa Mheshimiwa Dkt. Mollel.
MHE. JOHN W. HECHE: Wanataka kuharibu Bunge hawa...
T A A R I F A
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumpa dada yangu mpendwa taarifa kwamba ameanza…
(Hapa Mheshimiwa John W. Heche alizungumza bila kufuata utaratibu na bila kutumia kipaza sauti)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche, siyo vizuri unavyofanya.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Charles Wegesa, tulia.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche, naomba utulie jamani na wenzio. Mheshimiwa Dkt. Mollel, naomba umalizie taarifa yako.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumpa taarifa dada yangu kwamba ameanza vizuri na ameonesha jinsi ambavyo kwa awamu ya nne kumekuwa na kwamba inatengwa hela lakini tunahitaji kufikia lengo hatufikii, ndiyo maana tunaweka miradi ya kimkakati, kama ya Stiegler’s na mingine ambayo itahakikisha tuna-boost viwanda na chanzo mapato ya ndani yaweze kuongezeka ili tuweze kubadilisha bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha kusikitisha wanaongea kizalendo wakidai kwamba ni makosa kufanyika hayo ambayo yangetusaidia tuweze kufikia lengo yeye analolitaka. Kwa hiyo, wakati tuna-address issues hizo anazolalamikia anapinga kwa hiyo tunafikiri dada yangu ungetusaidia sasa kuunga mkono Stiegler’s na nyingine ili mwisho wa siku tuweze kufikia lengo ambalo unataka tufikie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester, taarifa hiyo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni uchanga wa kuingia Bungeni unamsumbua, ni njuka siyo size yangu, siwezi kumjibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo trend ya Serikali…
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Nitaanza vibaya mama.
MHE. ESTER A. BULAYA …ya Chama cha Mapinduzi kushindwa…
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Halima Mdee yuko wapi kwanza nikushtaki kwake?
MWENYEKITI: Waheshimiwa naomba tutulizane, tusikilizane Waheshimiwa, Mheshimiwa Ester naomba uendelee tafadhali.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema, kwamba pesa zikiwekwa kwenye uzio ni tofauti na pesa zingine anazozisema yeye, hizi zinaenda kwenye matumizi maalum, lazima ziende zote, ndiyo hoja iliyopo hapa. Ziko kwenye ring-fenced, ndicho ninachokisema, na hiyo trend ilianza tangu Bunge lililopita mpaka hili la Serikali ya Awamu ya Tano bado hamjafanikiwa kutoa pesa zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu hii imejipambanua inashughulika na ufisadi, imeanza na mishahara hewa…
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.
MWENYEKITI: Kuhusu Utaratibu.
KUHUSU UTARATIBU
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasimama kwa mujibu wa Kanuni ya 64(f) na (g). Kuwa Mheshimiwa Mbunge ametumia lugha ya kuudhi na inayodhalilisha wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa anayechangia amemwambia Mheshimiwa Dkt. Mollel kuwa ni ushamba wa kuingia Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester, umezungumza maneno ya ushamba? Haya, endelea.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti…
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge mnaosema ushamba nitawatoa nje, Mheshimiwa Ester endelea.
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na mchango wangu.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Amenivurugia ndoa yangu huyu unajua, Halima Mdee mke wangu halafu ukaolewa…
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati pesa za REA…
MWENYEKITI: Waheshimiwa tuwe na nidhamu jamani, hebu Mheshimiwa Ester naomba umalizie.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati pesa za REA Serikali hii inachelewa kupeleka, lakini bado…
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti,…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Selasini.
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
MWENYEKITI: Sasa Mheshimiwa Chief Whip amesimama bado mnapiga kelele ya nini?
Mheshimiwa Chief Whip endelea.
MWONGOZO WA SPIKA
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba mwongozo wako, kwanza kuhusu aina ya taarifa zinazotolewa hapa Bungeni, lakini pamoja na hayo, Mbunge anachangia lakini Mbunge mwenzake anawasha microphone na kutukana. Na bahati mbaya sana inawezekana Kiti chako hakisikii, lakini maneno ambayo yamesemwa ni maneno makubwa sana na yameingia kwenye microphone. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi naomba mwongozo wako; hivi hii miongozo inayotolewa kwa ajili ya dhihaka tu pamoja na matusi na nini, unairuhusu iendelee kwenye Kiti chako ili vilevile iamshe hasira za watu? (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Selasini, nimekuelewa. Waheshimiwa tutulizane. Waheshimiwa tulizaneni, wote Wabunge hapa mnaelewa vizuri Kanuni na mnajua nini mnafanya, kwa hiyo mnafanya makusudi, mnaposema wawili, watatu, wanne mimi huku sisikii kinachozungumzwa na mtu mmoja, siyo ninawaachia, ukiongea wewe na mwingine na mwingine hakuna kinachosikilizika, kwa hiyo, mimi nashindwa kutoa maamuzi. Ila ninyi Wabunge mnaelewa Kanuni na mnafanya makusudi, yeyote ambaye atakwenda sasa hivi kinyume atatoka nje hana ruhusa ya kuchangia, naomba umalizie muda wako.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mbali ya kwamba fedha za REA haziendi zote, lakini kumekuwa na ufisadi, kuna malipo hewa. REA imeipa Kampuni ya HIFAB fedha za ziada, zilizozidi, Dola za Kimarekani 81,000 na ushee wakati ilipaswa kulipa dola 9,000; na hili jambo halijafanyika mwaka 2010, 2011, limefanyika mwaka 2017 kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni wizi kama wizi mwingine, wahusika wanatakiwa washughulikiwe na mpaka sasa hivi na kwenye hotuba yetu tumesema bado Dola za Kimarekani 44,000 hazijarudishwa ambapo huko Serikali hii inasema ya wanyonge ndiko pesa za wanyonge zinapigwa. Huko ndiko ambako tunahitaji umeme vijijini, huko ndiko ambako Serikali hii imewapa Wakuu wa Mikoa waanzishe viwanda; wakati kuna uchafu huu hivyo viwanda vitakamilikaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna ukaguzi ulifanywa kwa mikataba mitatu iliyogharimu shilingi bilioni 984 ambapo imegundulika vijiji 55 kwenye Mikoa ya Tanga, Mwanza, Arusha na Manyara tayari vina umeme lakini wakandarasi wamelipwa tena waende wakaweke umeme. Huu ni wizi, na tunaposema wizi hatuwezi kunyamaza eti tukachagua awamu, huu ni wizi kama wizi uliofanyika awamu zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji ukaguzi maalum ufanywe ili hiyo dhamira sasa ya kuzima vibatari mikoani huko na vijijini itekelezwe. Kwa hiyo tutahitaji majibu sahihi. Sasa kama vijiji 55 hivi, je, kwa nchi nzima tunaingizwa mkenge kiasi gani, huo wizi upo kiasi gani? Kwa hiyo haya lazima yafanyiwe kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa pia na malalamiko kwenye suala zima la kuunganishiwa umeme vijijini. Wanasema wenye pesa ndio wamekuwa wakipewa kipaumbele katika kuunganishiwa umeme. Wananchi wa kawaida huko majimboni kwetu wanalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninapenda kulizungumzia ni kuhusiana na suala la TANESCO. Mpaka sasa hivi Shirikia TANESCO linajiendesha kwa hasara kwa bilioni mia tatu na. Kipindi cha awamu ya nne wakati inaondoka madarakani hasara ilikuwa bilioni 124, yaani kuna ongezeko la bilioni 122. Sasa tulitegemea Serikali hii inayokusanya kodi ingeenda kuondoa zile hasara na kuleta faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado madeni; madeni kutoka bilioni 700 mpaka bilioni 958 na TPDC peke yake inaidai TANESCO bilioni 340. Ndiyo maana Kambi Rasmi ya Upinzani tulisema shirika hili litakufa, sisi siyo wa kwanza, tumeshauri ligawanyeni, kuwe kuna mashirika mawili, limezidiwa uwezo na athari ya madeni, athari ya kujiendesha kwa hasara inakwenda kuathiri kwenye mtaji. Haya ndiyo ambayo tunayasema… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)