Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Nishati; na ninapoanza, leo tarehe 28 zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania kufikisha miaka 50, nichukue fursa hii kuwapongeza Watanzania kwa shirika la Kitanzania kufikisha miaka 50. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mtumishi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania kwa miaka 18, lakini ni mtumishi wa sekta ya mafuta kwa miaka 30. Kwa hiyo ninachokizungumza sikukisoma darasani, ninachokizungumza nakijua ndiyo maana wakati mwingine huwa naona mnyukano nashika kichwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposherehekea miaka 50 ya TPDC napenda nichukue fursa hii kuipongeza Serikali na pia nilipongeze Bunge hili. Bunge la Kumi lililopita kupitia Sekta ya Mafuta tuliwahi kufanya mambo makubwa, moja wapo ni kutengeneza tozo, la pili kuzuia uchakachuaji na la tatu bulk procurement. Wabunge waliokuwepo watamkumbuka Mheshimiwa January Makamba, Mwenyekiti wetu na Mzee wa SCOPO, Mheshimiwa Mzee Ndassa, haya ni mambo makubwa ambayo tunapaswa kujivunia. Sekta ya mafuta watu wengine wanaweza wasilewe; ni wakala mkubwa wa Serikali kwenye kukusanya kodi; kodi kubwa inakusanywa na TRA hupitia kwenye sekta ya mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine cha kujivunia kwenye sekta ya mafuta, ndiyo sekta nafuu, ndiyo sekta ya kipekee ambako kuna ubia wa sekta binafsi na Serikali. Vituo vya mafuta 1,400 vilivyoko nchini vyote ni vya sekta binafsi, ndipo mahali pa kulea Watanzania ili kuweza kuwaonesha kwamba kumbe sekta binafsi inaweza kufanya kazi. Tanzania tunayo hifadhi ya mafuta ifikayo milioni 1,200 m3, lakini yote hiyo asilimia 89 inamilikiwa na sekta binafsi. Mimi ni muumini wa sekta binafsi nimesimama kuisemea sekta binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kitu kinachoitwa power mix. Tunapokwenda kujenga uchumi wa viwanda ifikapo 2025 nchi hii inahitaji gigawati 25 au megawati 25,000. Kwa hiyo mimi mtu anayejadili Stiegler’s Gorge nashindwa kumuelewa. Mahitaji yetu ni makubwa mno kuliko Stiegler’s Gorge, tunaihitiaji Stiegler’s Gorge na… (Makofi)
(Hapa sauti ilikatika)
MWENYEKITI: Sogea kwenye microphone nyingine. MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hapa. MWENYEKITI: Muda wake bado upo, anaendelea, dakika kumi.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niseme washindwe na walegee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumza kuhusu power mix. Mahitaji ya nchi hii kufika 2025 ni gigawati 25 ambayo mnaita megawati 25,000. Kwa hiyo suala la Stiegler’s Gorge yenye megawati 2,000 wala si kachumbari, tunaihitaji jana. Lakini ina maana tunahitaji vyanzo vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuwapa uzoefu; niliwahi kwenda huko SADC, Congo DRC wanatengeneza gigawati au megawati 40,000; South Africa ameshaomba 16, Mheshimiwa Waziri ukija hapa uwakumbushe. Ndiyo maana tunatengeneza kitu kinaitwa interconnector, tunatengeneza mtandao wa kutoka Kongo, wa kutoka kaskazini, nchi za Ethiopia. Sasa kama baba anakwenda kuhemea usimshangae mama anayelima viazi. Yaani Stiegler’s Gorge ni kama viazi, chakula bado kinahitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninapenda niwaeleze katika mambo ya nishati kuna vyumba vitatu; chumba cha kwanza kinaitwa availability, cha pili liability na cha tatu affordability. Wawekezaji tunaowatafuta, kama hawajui kwamba una nishati ya kuaminika kesho hawawezi kuja. Kwa hiyo anayejenga Stiegler’s Gorge anawavuta wawekezaji waje. Mwekezaji makini haangalii umeme ulionao leo…
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: …anaangalia keshokutwa utakuwa na…
MWENYEKITI: Mheshibiwa Mwijage, taratibu; taarifa.
T A A R I F A
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimpe taarifa rafiki yangu anayechangia. Amezungumza mambo ya energy mix; suala la energy mix ni kwamba unakuwa na aina tofautitofauti za umeme, yaani upepo, maji, makaa ya mawe. Sasa hapa anachosema energy mix tayari tuna Mtera, tuna Kihansi, sasa kule tena tunaleta tena mambo ya maji tena, sasa hiyo ni energy mix ipi?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwijage.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema hii sekta siyo mchezo. Huwezi kuisoma umelala, hili si somo la kulala kwenye kitanda ukaanza kusoma. Yaani nimekwambia mwanzo nina miaka 30 kwenye sekta, naweza kuanzia jotoardhi, nikakueleza umeme wa mawimbi, nikakueleza mambo ya mkaa, kwa hiyo watu wengine muwe mnakaa Bungeni mnasikiliza. Mheshimiwa Maige asubuhi ametoa somo la makaa ya mawe na yenyewe nishati tunayo; hiyo taarifa siikubali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika hiyo niwaeleze dhana isiyo, kuna dhana isiyo; mtu anasimama anasema bomba la kutoka Mtwara linatumika asilimia sita it’s a failure, it is not! Ukijenga barabara ukamaliza, traffic ika-jam umeshindwa; ile bomba ni barabara tunawavutia wawekezaji wachukue gesi zaidi, ile gesi mmesema itakwenda Uganda, bomba halipaswi kujaa na uwepo wa bomba lile ni kivutio cha gesi ya maji marefu ipitie pale ije huku itumike. Lakini gesi ile ni kivutio cha visima vilivyoko kusini vichimbwe vitatumia bomba ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie bomba la Uganda. Wako watu hawajui faida ya bomba la Uganda. Faida ya bomba la Uganda linafungua fursa zetu. Nchini Tanzania tuna kitu kinaitwa stranded reserve, sehemu za Kigoma, sehemu za Eyasi, kuna mafuta kule Mungu atatujalia tutayapata, lakini watafutaji hawakuwa na motisha ya kwenda kule. Kwa hiyo kwa kuwepo bomba la kutoka Kabale, Hoima, mpaka Tanga ina maana wawekezaji sasa watavutiwa, watakwenda kuchimba mafuta kule na siku moja nchi yetu itaweza kupata mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali na mwanzo, hili ni somo gumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kumalizia naomba niwaeleze mojawapo ya mambo niliyofundishwa. Wanasema wasafiri wenye busara ni wajibu wao kukumbuka wafikapo safari salama au njiani wakiwa, kukitunza chombo chao vyema na nahodha wao kushikilia. Chombo ni Tanzania na nahodha mtajaza wenyewe. (Makofi)