Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii ambayo nimeipata jioni ya leo kuchangia kwenye bajeti hii. Nipende kwanza kuipongeza Serikali, kwanza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na nimtakie kila la kheri kwenye ziara yake aliyopo nchini Namibia arudi salama, tunamuombea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumpongeza pia Waziri na Naibu Waziri na Timu nzima ya Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa ambayo wanafanya kuhakikisha kwamba wanatuletea maendeleo katika sekta hii. Najua mkandarasi wa kule Kigoma na Katavi wameanza utekelezaji wa mradi ule late kidogo, lakini naamini kwamba kama Serikali ambavyo imekuwa ikielekeza wakandarasi kumaliza miradi kabla ya wakati nina imani kwamba mkandarasi ambaye anafanya kazi Mkoa wa Kigoma naye atamaliza kwa wakati na kuhakikisha kwamba Kata zangu za Nyachenda, Bugaga, Buzye, Kasangezi, Lusesa, Kalela, Lungompya na nyingine zinapata umeme kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende pia kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa na maamuzi magumu ambayo walifanya kwenye mradi wa Rufiji Hydro Power. Naomba niseme kitu kimoja, ndugu zangu nimekaa hapa nikiwa nasikiliza michango ya watu tangu mwaka jana na mwaka huu nimeona, hasa ndugu zetu wa upande wa pili. Niseme Rais wa Awamu ya Nne aliwahi kusema kwamba akili za kuambiwa changanya na za kwako, akimaanisha usiamini kila unachoambiwa. Sasa ndugu zangu kwa sababu mabeberu wamekuwa wanakataa mradi huu ambao ni very potential kwa Taifa letu, msiingie kwenye mgogoro wa kuwasapoti ili hali mnajitoa ufahamu kwa faida za mradi huu wa Rufiji Hydro Power. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme tu kwa faida ya Watanzania, Mradi huu wa Rufiji Hydropower una faida nyingi sana kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla. Faida ya kwanza kabisa tunaenda kupata umeme ambao tunaupata kwa bei ndogo kuliko umeme wa chanzo chochote katika nchi hii, namba moja kabisa. Tunaenda kupata umeme mwingi; kwa study iliyopo kwamba katika nchi yetu ya Tanzania hakuna chanzo chochote cha nishati ya umeme ambacho kinaweza kikatoa nishati ya bei ndogo lakini kwa wingi kama chanzo cha maji. Kwa hiyo uamuzi wa Serikali kujikita kwenye miradi ya kuzalisha umeme wa maji ni uamuzi sahihi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, faida ya pili, mradi ule ukiusoma vizuri utaona kwamba kutakuwa na miradi ya uvuvi pia. Wanavyojenga lile bwawa kutakuwa kuna potential watu kufanya shughuli za uvuvi ambayo ni shughuli ya kiuchumi ikayoweza kuwasaidia wananchi ambao watafanya shughuli hiyo. Sababu ya pili au faida ya pili, tunategemea mradi ule kutakuwa na umwagiliaji, watu wanafanya kilimo cha mpunga na miwa na study inaonesha kwamba mpunga au mchele utakaotoka kule kwenye bonde lile utaweza kulisha Afrika Mashariki na Kati, sasa wanakataa nini kwenye mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye sababu nyingine, ule mradi kwa sababu ni wa kipekee nawahakikishieni ule mradi utakuwa ni kivutio cha utalii Afrika Mashariki. Wako watu ambao wakija Tanzania watataka kwenda kuona kule Rufiji Hydro Power namna ambavyo ilivyo na kujifunza. Pia huu mradi naamini, nitofautiane na wengi ambao wanaamini kwamba huu mradi unaenda kuharibu mazingira, niseme huu mradi unaenda kutunza mazingira kwa sababu gani, wananchi wengi vijijini kule wanatumia nishati ya kuni kwa ajili ya kuleta mwanga lakini pia na kupika. Kama haitoshi wanatumia vibatari kwa ajili ya nishati ya mwanga. Sasa umeme unapokuwa umeenda tunaamini kwamba matumizi ya kuni yatapungua lakini na matumizi ya vibatari yatapungua. Huo utakuwa ni utunzaji wa mazingira kupitia mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme huu mradi mimi naufananisha na three gorges ya China, huu mradi ulianzishwa na Rais wa kwanza wa China ambaye alikuwa anaitwa Sun Yat-Sen. Huu ni kama vile mradi wetu huu ilivyokuwa wazo la Mwalimu Nyerere vilevile na ulibuniwa zaidi kabla ya mwaka 1980, huu wa three gorges. Sasa kwa sababu ya figisu figisu kama ambazo tunasema hapa kwetu Tanzania, huu mradi ulianza kutekelezwa kuanzia miaka 1990.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutekelezwa kwa mradi huu kulitokea baada ya Bunge la China kupiga kura kwamba kama nchi inahitaji mradi huu au haihitaji. Walivyopiga kura theluthi mbili ya Wabunge wa China wakakubali kwamba mradi huu wanautaka kama Taifa. Sasa niseme sisi wameleta bajeti hapa Wizara mwaka jana kuomba bilioni 700 kwa ajili ya mradi huu, sisi Wabunge wa CCM nadhani na wa CUF ambao ni zaidi ya robo tatu, zaidi ya idadi ya ile ya Wachina ambao ilipisha mradi ule tulisema tunahitaji Mradi wa Rufiji Hydro Power. Kwa hiyo niwaambie Serikali, hili jambo lina baraka ya Bunge na ndiyo maana mwaka jana tuliwapa bilioni 700 na nina imani hela zimefanya kazi ipasavyo na tunawaunga mkono katika hilo.

Mheshimiwa Spika, na niseme, lazima Serikali muwe imara, msiyumbishwe na miluzi. Kule China wakati wanajenga mradi huu kuna watu baada ya kupiga kura Bungeni, ilitolewa amri ya Serikali kwamba hairuhusiwi mtu yeyote kupinga mradi huu na mtu aliyekuwa anajaribu kupinga kuna watu ambao walifungwa jela. Sasa mimi siwaambii Serikali mkawafunge wanaopinga mradi huu lakini niwaambieni wapuuzeni chapeni kazi tunahitaji Mradi wa Rufiji hydropower kwa ajili ya manufaa ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ahsante sana.