Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara hii ya Nishati kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya. Ninapongeza kwa mambo makubwa manne, kwanza kwa kuweza kuzalisha umeme na tukawa na ziada ya megawatt 300, kwa maana kwamba sasa hatuna mgao wa umeme. Jambo lingine ninalokupongeza ni kuanzisha ujenzi wa mradi wa Rufiji hydropower ambao tutapata megawatt zaidi ya 2115. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la usambazaji wa umeme kwa mradi huu kabambe wa REA ambao tunategema kwamba vijiji vyote ikiwezekana vijiji zaidi ya 2,012 vitapata umeme. La mwisho pia nakupongeza kwa kuamua kwamba uunganishaji wa umeme maeneo yote vijijini itakuwa ni 27,000 japokuwa hili lina changamoto hasa pale ambapo wanapaswa wananchi kununua nguzo kwa shilingi 319, kwa mfano kama Mkoa wa Njombe, kwakweli naona kama hii bei ya nguzo kwa mwananchi kuweza kuunganisha umeme ni kubwa. Halafu akiunganisha yeye ile nguzo inakuwa ni mali ya TANESCO wale wengine wanakuwa wanaunganishwa kwa 27,000. Mheshimiwa Waziri, mimi naomba jambo hili uliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika huu mradi kabambe wa usambazaji umeme vijijini mwaka jana nilichangia, kwamba kweli ni kazi kubwa tunapeleka miundombinu katika vijiji 12,000 lakini kujenga miundombinu yake na kufanya matengenezo kuwa na uendelevu wa ile miradi lazima tuwe na mfumo wa taasisi kwa ajili ya matengenezo (Maintenance) kama hakuna mfumo mzuri wa maintenance miradi hii ita-collapse.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikichukuliwa mfano kwa Wilaya ya Wanging’ombe, mwaka jana nilisema, kulikuwa na transformer 30 zimeungua sasa kama huna mfumo wa kibajeti wa kuweza kumsaidia huyu mtu wa TANESCO ina maana kwamba wananchi wataendelea kuwa gizani pamoja na kwamba kazi kubwa mmeifanya. Kwa hiyo naomba sana muangalie mfumo wa kitaasisi wa maintenance. Ukichukulia mfano kwenye TANROADS tumeweka Mfuko wa Barabara katika Mfuko wa Barabara asilimia 90 zinaenda kwenye matengenezo na ndiyo maana barabara zinakuwa nzuri muda wote lakini kwenye kitabu hiki sijaona mfumo wowote wa maintenance wa hii Programu Kabambe ya Usambazaji wa Umeme Vijijini. Naomba jambo hili uliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye Wilaya yangu ya Wanging’ombe, hivi leo ninavyoongea kuna vijiji 54 havina umeme kabisa. Katika programu hiyo inayoendelea kuna vijiji 38 vina matumaini ya kupata umeme. Mkandarasi aliyepo wa Mkoa wa Njombe anaitwa Mufindi Power joint venture na Hagie kwakweli kasi yake ni mbovu na sidhani kama ataweza kumaliza hiyo December ambayo ndiyo mwisho wa mkataba wake kwa sababu mpaka sasa kwenye wilaya yangu ameweza kuwasha vijiji vinne tu na vitongoji vitano. Kati ya viji na vitongoji 48 sasa kwenye miezi sita nina wasiwasi kwamba sidhani kama anaweza kumaliza. Naomba Mheshimiwa Waziri uangalie namna gani mikataba hii ilivyoingiwa na namna inavyosimamiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimeona kuna udhaifu wa usimamizi. Meneja wangu wa TANESCO hana hata gari ya supervision anafikaje kwenda kuona huyo mkandaras anavyofanya? Maeneo mengi nguzo zimewekwa wanasema hawana waya na sehemu nyingine wanasema nguzo ndogo hakuna. Sasa kwa mkoa kama Njombe ambapo tunazalisha nguzo ninashangaa kwanini hili linatokea? Kwenye mikataba najua kuna kipengele kwamba ndani ya siku 30 mtu akileta certificate lazima Seriakli ilipe...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa. Kengele imeshagonga, ahsante sana.

MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.