Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi walau ya kuchangia mchana huu ili niweze kusema maneno machache ambayo nadhani yatakuwa na faraja sana kwangu na kwa wananchi wa Jimbo la Nyamagana na Taifa zima kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, kwa haraka naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Waziri pamoja na Naibu Waziri na Wizara nzima kwa ujumla kwa namna ya kipekee ambavyo wamekuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano na ushirikiano huu ndiyo ambao umetuletea ahueni ya kutatua migogoro mingi sana kwenye nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakumbuka kwenye bajeti ya mwaka jana tulilalamika sana juu ya vifa avya utendaji kazi kwenye halmashauri nyingi. Waziri aliahidi na ametekeleza hili kwa vitendo na tumeona vifaa na kwenye halmashauri zingine zimefika.
Mheshimiwa Spika, tulisema; mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, tulilalamika sana juu ya uwepo wa kukosekana kwa Bodi ya NHC, nimshukuru sana Waziri kwa kulifanyia kazi na kuhakikisha Bodi inapatikana na sasa kazi inaweza kufanyika vizuri na hata malalamiko mengine yale yaliyokuwa pembeni yanaweza yakaanza kufutika haraka.
Mheshimiwa Spika, nijikite kwenye suala la urasimishaji makazi. Suala hili ni ukweli kwamba ziko changamoto nyingi sana na wananchi wengi sana kwenye Taifa hili waliokuwa wamepoteza amani leo naamini wanayo amani kubwa. Waliokuwa wamepoteza matumaini leo naamini wamerejesha matumaini na wale waliokuwa wanaenda kuwa maskini wa kutupwa, leo wamerudi kuwa na uhakika wa kuendelea na utajiri wao.
Mheshimiwa Spika, maeneo mengi nchi hii yalikuwa yameshachukuliwa yamejengwa na wananchi, wananchi wengi wamekaa kwenye maeneo ambayo hayakupaswa tena kuwa ni maeneo ya makazi na hii inatokana na michoro mingi nchini kutokusimamiwa vizuri pale inapokuwa imeshachorwa. Lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais na Waziri Lukuvi kwa jambo moja kubwa la kuamua kurasimisha makazi. Leo tunazungumza hapa sisi kama Nyamagana pamoja na jiji la Mwanza kwa ujumla, zaidi ya makazi 12,000 wamepata hati za makazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili sio jambo dogo. Nitumie nafasi hii kuwashukuru sana watendaji wa mamlaka na hi ardhi kule Mwanza Jiji pamoja na Manispaa ya Ilemela, kwakweli wamefanya kazi kubwa sana niendelee kuwatia moyo, hakuna kazi kubwa kama kuwatumikia wananchi wanyonge ambao wanahitaji kupewa ahueni kila siku ili waweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala bomoabomoa. Bomoabomoa hii Mheshimiwa Waziri leo tena amesema; mwananchi ambaye yuko kwenye eneo ambalo halihitajiki kuweka barabara, eneo lilotengwa miaka iliyopita kama limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kitu kinachoweza kujengwa eneo jingine tumuache mwananchi huyu asivunjiwe nyumba ili aendelee kuishi na tumrasimishie makazi yake.
Mheshimiwa Spika, zaidi ya yote suala la mpango kabambe. Naenda haraka kwa sababu ya muda. Mheshimiwa Waziri huu mpango kabambe Mwanza umefanya vizuri sana na sisi mwanza kama ulivyosema nah ii ni kazi kubwa inayofanywa na watendaji wa ardhi wa Jiji pamoja na Manispaa ya Ilemela na kile kikosi kazi kilichotengenezwa kwa ajili ya kusimamia mpango kabambe. Yako maeneo Mheshimiwa Waziri, hayana sifa ya kupimwa kwa maana kwamba yanayo sifa lakini yako kwenye maeneo ya vilima. Mheshimiwa Waziri unajua, sisi Mwanza tuna milima mingi na wakazi wengi sana wamejenga kwenye vilima hasa vilima vya kule Isamilo, Mabatini, Igogo lakini hata maeneo ya mbugani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa jambo pekee Mheshimiwa Waziri, maeneo haya hayawezi kupewa hati za miaka 90 kama wengine lakini umezungumza suala la leseni za makazi. Nikuombe, hii 5,000 5,000 kule Mwanza ni nyingi sana. Wakazi kule milimani wanaweza kutoa fedha hii wakati wowote. Nikuombe uje Mwanza, uzungumze na wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya milima uwapatie leseni za makazi ili na wao waweze na uhakika na maeneo yale ili mpango kabambe utakapokuja Mheshimiwa Waziri kusiwe na tatizo tena, mtu awe na uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, anayekuja kwa ajili ya kutwaa lile eneo ajue anazungumza na nani ambaye atakuwa tayari kumuachia lile eneo kwa ajili ya kuendeleza mpango na wananchi hawana tatizo, wako tayari na wamekuelewa sana. Zaidi ya yote Mheshimiwa Waziri, niseme tena, umeondoa umaskini kwa Watanzania wengi, umeondoa unyonge kwa Watanzania wengi na zaidi ya yote endelea kusaidia maeneo mengi bado yanaweza kutaka kubomolewa kwa namna ambavyo unatuongoza maelekezo haya yaende mpaka kule kwenye Kata, mpaka kule kwenye halmashauri ili tuweze kuwasaidia wananchi hawa.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, kujenga nyumba ni miaka 10 na mimi nawashangaa ndugu zangu wanaolalamika. Nilikuwa naona hotuba hii lakini kwa sababu Mheshimiwa Spika alishatos mwongozo mzuri na mimi nisirudie kule lakini niseme maeneo yote ambayo kwakweli yanastahili kuacha njia kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania, leo ukienda pale kwa Mheshimiwa Kubenea pamoja na kwamba kulikuwa na majonzi lakini leo ni faraja na hata eneo linaongezeka thamani Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, ni lazima tuwe tunafika sehemu nyingine wakati fulani tunaona hili ni sawa lakini tunafahamu maumivu yanaingia kwa kasi na yanatoka polepole sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, nikushukuru sana kwa kazi nzuri mnayoifanya, tunaomba muendelee kutusaidia na kulisaidia Taifa hili ili tuweze kusonga mbele. Ubarikiwe sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na Mungu akubariki na jana nimeona umefanya kazi nzuri sana ya kutoa tunzo za Mo Awards kwa wachezaji wa Simba. Ubarikiwe sana, hii ni kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia 100. (Makofi)