Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi nami ya kuchangia bajeti, makadirio ya bajeti ya Wizara ya Fedha, mafungu yote saba ya Wizara hii. Na nitakuwa na maeneo matatu ya kuchangia, kama nitapata muda nitaongeza eneo la nne na ningependa kuanza na upande wa makusanyo ya kodi.

Mheshimiwa Spika, kwa muda wa miaka minne sasa tumekuwa tukielezwa kwamba tumeongeza sana uwezo wetu wa makusanyo ya kodi, lakini ukitazama takwimu za Serikali yenyewe kuhusiana na uwezo wetu wa kukusanya kodi ukilinganisha na huku ambako tunatoka story hii sio story ya kweli. Ni story ambayo inapaswa tuelezwe upya, ili tuweze kuona changamoto ni nini na tuweze kutatua namna gani.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani mwaka 2015, kipimo cha makusayo ya kodi kwa kutumia Pato la Taifa, yaani tax GDP ratio ilikuwa tumefikia asilimia 15 na lengo letu na Waziri Mpango atakumbuka kwamba katika Mpango wa Maendeleo wa Kwanza ilikuwa na lengo la asilimia 16 ambalo ndio sasa lengo la bajeti ambayo inakwisha sasa hivi na Mpango wa Maendeleo wa Pili tufike asilimia 19 ya pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali tax GDP ratio ya mwaka wa fedha 2017/2018 ni asilimia 12 tu. Na hii inatuweka sisi kuwa hata chini ya nchi kama Burundi ambayo tax GDP ratio ni asilimia 13, Kenya asilimia 18.1, Uganda asilimia 16, Rwanda asilimia 16. Katika nchi za Afrika Mashariki sisi ni wa mwisho ukitumia kiashiria cha kupima makusanyo ya ndani kulingana na Pato la Taifa yaani shughuli za uchumi katika nchi. Hii inathibitisha ya kwamba hatuendi mbele katika makusanyo ya kodi, bali tunarudi nyuma, lakini kwa sababu tunaangalia tarakimu tumetoka bilioni 800 mpaka trilioni 1.2 au trilioni 1.3 tunajiona kana kwamba tunakusanya sana, lakini ukiangalia bilioni 800 ya Pato la Taifa kwa mwaka husika na trilioni 1.3 ya Pato la Taifa la mwaka huo maana yake ni kwamba tunashuka sana.

Mheshimiwa Spika, nimepita library asubuhi, nimejaribu kuangalia miaka mitatu ya mwisho ya Serikali ya Awamu ya Nne ongezeko la makusanyo ya kodi lilikuwa ni asilimia ngapi kulingana na miaka mitatu ya mwanzo mpaka huu mwaka wa fedha tunaoumaliza sasa ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Spika, miaka mitatu ya mwisho ya Serikali ya Awamu ya Nne wastani wa ongezeko la makusanyo ya kodi lilikuwa ni asilimia 16. Wastani wa makusanyo ya Serikali ya Awamu ya Tano toka wameanza mpaka bajeti hii ambayo tunaimalizia ni asilimia 11.3; kwa hiyo, hakuna sababu yoyote ya kujidanganya kwamba tuna makusanyo makubwa ilhali makusanyo si mazuri.

Mheshimiwa Spika, na makusanyo si mazuri kwa sababu biashara zinafungwa; sekta binafsi ndio inayotengeneza kodi, sekta ya umma haitengenezi kodi. Zaidi ya asilimia 95 ya watu wanaoajiriwa, ajira rasmi katika nchi yetu, wanatoka sekta binafsi, kwa miaka mitatu iliyopita tumeinyonga sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, leo tunavyozungumza, nitakupa mifano tu ya siku za karibuni; Kampuni ya Mwananchi imepunguza wafanyakazi zaidi ya 100 ndani ya wiki mbili zilizopita. Kampuni ya New Habari Corporation ya akina Mheshimiwa Bashe imepunguza kutoka wafanyakazi 300 wamebakiwa na wafanyakazi 43. Tunavyozungumza sasa Kampuni inayonunua tumbaku asilimia 40 ya tumbaku ya nchi hii, Kampuni ya TLTC, Kiwanda cha Morogoro wamefunga na wame-retrench wakati wa season watu 3,000 walipoteza kazi. Katika mazingira kama haya mtapata wapi kodi? Kwa sababu sehemu kubwa ya kodi ni kodi za wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, wala tusijidanganye tukadhani kwamba wenye mitaji wanalipa kodi kubwa, angalieni takwimu za Serikali 2/3 ya makusanyo ya kodi za mapato ni kodi za wafanyakazi. Kwa hiyo, ni lazima mjenge mazingira ya kazi watu wapate kazi ili Serikali ipate pesa, lakini Serikali inanyonga, biashara zinafungwa, wapi Serikali itapata pesa? Ndio maana takwimu hizi zinaonekana hivi kwamba tax GDP ratio imeshuka na hata ongezeko la hizo kitarakimu ambazo tunaambiwa bado ukilinganisha na Serikali iliyopita, zimeshuka sana ni lazima tufanye marekebisho ya uhakika ya kuhakikisha ya kwamba, tunakusanya kodi ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo nataka nilizungumzie nalo kwa kina kidogo ni usimamizi wa Deni la Taifa. Siendi kwenye mjadala kama deni ni himilivu au si himilivu, usimamizi wa Deni la Taifa ni tatizo. Tazama record za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa miaka miwili iliyopita, wanatoa maelezo yanayoonesha ya kwamba moja, kuna upotoshaji mkubwa katika taarifa za Deni la Taifa kwa sababu mfumo wa malipo ya Deni la Taifa na mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu za Deni la Taifa havisomani. Matokeo yake ni kwamba tuna madeni ambayo hayako recorded.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye Taarifa ya CAG ya mwaka jana kuna zaidi ya shilingi trilioni mbili ambazo record yake haionekani, lakini Mdhibiti amekwenda kwa waliotukopesha, kuna fedha ambazo waliotukopesha wanasema tumezitoa, ukienda Hazina wanasema hizo mbona hatujazipata kwa sababu ya mfumo mbovu wa usimamizi wa deni. Kwa hiyo, hata deni ambalo tunaambiwa hapa na Mheshimiwa Waziri Mpango ndugu yangu kwamba, ni kiasi hiki, ni asilimia hii ya Pato la Taifa sijui ya mauzo nje, na kadhalika, ni deni ambalo record yake sio sahihi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba kwa ruhusa yako, for the first time in the history of this country, ruhusu Ukaguzi Maalum wa Deni la Taifa tuweze kupata takwimu sahihi kwa sababu takwimu za sasa hivi sio sahihi na mimi hapo nimesoma ripoti mbili tu ya mwaka jana na ya mwaka huu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo inaonesha kuna tatizo kubwa sana katika utunzaji wa kumbukumbu; wanatunza kumbukumbu za deni kwenye madaftari ya shule, ma-counter book, unawezaje kutunza kumbukumbu za deni kwenye ma-counter book? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aah, ndio ukweli huo Mheshimiwa Mwakyembe na Mheshimiwa Spika, mwambie Mheshimiwa Mwakyembe tumeingia wote Bungeni humu, tuko sawa kwa hiyo, aniheshimu wakati naongea kwa hiyo, atulie kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba hili jambo uruhusu Ukaguzi Maalum wa Deni la Taifa kwa maslahi ya nchi tuweze kujua kwamba tunadaiwa kiasi gani na tunadaiwa na nani? Kwa sababu inawezekana tukawa tunalipa madeni ambayo ni hewa, hayapo. Kuna kitu kinaitwa odious debts, debts ambazo zimekuwa created, hazipo na hii inawezekana kabisa ipo katika mfumo wetu kwa sababu haufanyi kazi sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni jambo ambalo naishukuru sana Kamati ya Bajeti na naipongeza sana imefanya kazi nzuri sana ya Bunge. Kuna fedha ambazo zinakusanywa kinyume na Katiba na sheria. Kwa mujibu wa Ibara ya 138 ya Katiba, Bunge lako hili unaloliongoza ndilo lenye mamlaka ya kutamka kodi. Ibara ya 138 ya Katiba; hakuna kodi ya aina yoyote itakayotozwa isipokuwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge au kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa kisheria na uliotiliwa nguvu kisheria na sheria iliyotungwa na Bunge.

Mheshimiwa Spika, lini hapa Bungeni tulikaa tukapanga ushuru wa vitambulisho vya wamachinga? Wapi kwenye revenue book unaona hayo mapato? Tutawa- account namba gani hawa? Haipo kwenye sheria…

SPIKA: Ahsante sana, muda hauko upande wako.

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, naomba dakika moja tu ya kiti, dakika moja ya kiti. Ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, haipo kwenye sheria ya utaratibu wala kwenye revenue book, hakuna mahali ambapo fedha zinazokusanywa kwa wananchi wetu zimo, sasa tunatuvunjaje sheria na Katiba namna hii? Kwamba Bunge halijakaa kutunga, Serikali inatekeleza, watu wetu wanaumizwa, nimesikia Tunduma huko leo wafanyabiashara wameshindwa kufanya biashara kwa sababu wameambiwa hawana vitambulisho, haimo kwenye revenue book, kwenye sheria, tunavunja Katiba kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba maoni yaliyotolewa na Kamati ya… (Makofi)

SPIKA: Nakushukuru sana.