Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makambako
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi kunipa nafasi name niwe miongoni mwa wachangiaji wa bajeti hii iliyoko mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuishukuru sana kwa dhati Serikali ya Awamu ya Tano kwa mwelekeo wa bajeti hii ambayo imegusa kila sekta, nampongeza sana Rais wetu. Vilevile nimpongeze kwa kumteua Dkt. Mpango na Naibu Waziri, lakini pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha. Pia niwapongeze watumishi wote Wizara ya Fedha kwa mwelekeo wa bajeti hii nzuri ambayo imegusa kila mahali, imegusa kila sekta, nampongeza sana Waziri kwa kazi nzuri ambazo mmekuwa mkizifanya hasa bajeti iliyoko mbele yetu. Hongera sana Mheshimiwa Mpango kwa kazi nzuri ambayo iko hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili nizungumzie hizi taulo za kike. Serikali iliondoa VAT kwenye bajeti iliyopita kwa ajili ya kuwasaidia mama zetu, dada zetu na watoto wetu kwa ajili ya taulo hizi za kike. Lakini baadhi ya wafanyabiashara ambao walikuwa sio waaminifu bei haikuweza kupungua. Sasa Serikali imeweka mkakati na mpango mzuri wa kuhakikisha viwanda vyetu vya ndani vinazalisha taulo hizi ili bei ziweze kupungua. Ombi langu kwa Serikali, tusimamie ili lisije likatokea tena kama ambavyo wafanyabiashara kadhaa hawakuweza kupunguza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la wafanyabiashara au wajasiriamali mbalimbali ambao Waziri wakati anawakilisha hapa alisema sasa Serikali haitafunga biashara, haitafunga maduka au biashara mbalimbali za wafanyabiashara hususan wilaya na mikoa kutumia makufuli haya ya TRA. Ombi langu makufuli haya ya TRA, sasa Serikali ihakikishe wilaya na mikoa yatupwe ili kuwapa imani wafanyabiashara, maana Waziri alisema hapa mwenye mamlaka wa kuagiza makufuli haya yafungwe ni Kamishna wa TRA. Sasa ili kuwapa imani wafanyabiashara basi wakufuli haya katika wilaya na mikoa yatupwe kabisa ili kusudi kuwapa imani wafanyabiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la ukusanyaji kodi liko vizuri, lakini ukienda pale Kariakoo kuna maduka mengi sana. Serikali iangalie Kariakoo sasa imegeuza yale maduka kuna watu wanaweka bidhaa mbele ya milango ya wafanyabiashara, hawa machinga na ndiyo inasababisha sasa baadhi ya wafanyabiashara kufunga maduka nao waweke kama machinga, waweke mbele ya milango. Kwa hiyo, Serikali itakosa kodi kwa wafanyabiashara kwa sababu nao wanafunga sasa. Wanaweka mbele ya maduka. Serikali ifanye utafiti wa kutosha ili kuhakikisha hao wanaoweka mbele ya maduka watafutiwe eneo ili wafanyabiashara waweze kufanya biashara vizuri na kulipa kodi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine Serikali imeweka vizuri utaratibu wa magari haya yanayoagizwa kutoka nje. Ukiingia kwenye system unapata bei ili uweze kuagiza kutokana na kodi ambayo utailipa. Sasa kuna jambo ambalo mimi nashangaa tunaweka kwenye system. Mimi ni miongoni mwao, hivi karibuni mimi nimeagiza magari ambayo yameonesha magari haya kwa mwaka 2012 kodi yake ni hii. Wiki iliyopita magari yamefika, kodi ya gari la mwaka 2012, trekta unit IVECO lilikuwa shilingi 10,300,000 ukiacha kodi zingine, tayari limekwenda shilingi 13,000,000 kwa hiyo ongezeko la shilingi 3,000,000 tofauti na bei iliyoko kwenye system linaathiri sana wafanyabiashara. Ombi langu tuhakikishe bei tuliyoiweka kwenye system na ndiyo hiyo inakuja kulipiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la mwisho ni kuhusu Mkoa wa Njombe, tuna Liganga na Mchuchuma, ni uchumi mkubwa sana katika Mkoa wa Njombe na Tanzania kwa ujumla. Tunashindwa kuelewa ni kwa nini haianzishwi, kama tunakuta mipango Serikali iliyoweka ni mizuri mingi, basi tuhakikishe angalau tuanze kwa kuchimba mkaa kwa sababu kuchimba mkaa kule Mchuchuma na Liganga kunahitaji vifaa viwili tu, caterpillar na dozer, tuanzishe kuchimba ili wananchi wa Mkoa wa Njombe na hususan Wilaya ya Ludewa wajue Serikali ina mpango wa kuhakikisha tunachimba mkaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho niiombe Serikali katika makusanyo sasa ambayo tunaendelea kukusanya katika bajeti hii tunapeleka kwenye halmashauri mapema ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa ambayo tumepitisha bajeti hapa ndani Bungeni. Kwa mfano kwenye Jimbo langu Serikali imetupa fedha, tumejenga Kituo cha Afya Lyamkena, niombe na kituo kile kimeisha tupatiwe fedha kwa ajili ya vifaa tiba ili Kituo cha Lyamkena kiweze kuwahudumia wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako. Ninaipongeza sana Serikali kwa mipango mizuri ambayo maji, afya na kadhaika, mmekuwa mkisaidia katika nchi hii na hususan Halmashauri yangu ya Mji wa Makambako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana kupitia Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii ya Fedha. Hongera, chapa kazi na kaza mwendo. Ahsante sana. (Makofi)