Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Spika, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Bajeti ya Serikali, kwanza naomba kwa dhati kabisa nimpongeze Waziri wa Fedha kwa speech nzuri sana, lakini pia nimpongeze kwa kusikia kilio cha Wabunge toka tumeanza kuondoa tozo zote, tozo 54. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimpongeze Waziri wa Fedha kwa mara ya kwanza tumekuja tunafanya bajeti, siyo bajeti ya pombe, siyo bajeti ya sigara, hongera sana ndugu yangu, lakini la pili niipongeze Serikali kwa barabara ya Kigoma - Nyakanazi; naishukuru sana Serikali kwa kutukumbuka watu wa Kigoma, nadhani umefika wakati sasa tuhangaike na barabara ya Mwandiga, Chankere, kwenda Kagunga kwa sababu tutapitia pale gombe ambayo itasaidia sana kwa maana ya utalii nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nimesoma vitabu vyote hivi vya bajeti, nimesoma Mpango wa Taifa kuna maeneo mimi nadhani ningeomba Serikali tuyawekee mkazo unaostahili, tukiyawekea mkazo unaostahili tutapata fedha nyingi sana na mimi leo nataka nijikite kwenye growth na production. Nadhani umefika wakati Serikali tuhangaike na growth na production kwenye kilimo nimeingia Bungeni hapa huu mwaka Mungu akinijaalia mwaka kesho utakuwa mwaka wa kumi na tano, haiwezekani kila mwaka nimechukua mazao machache, kila mwaka uzalishaji wa kahawa, hauzidi tani 50,000; uzalishaji wa chai, tani 19,000; pamba haizidi tani 300,000; mkonge haizidi tani 36,000 na korosho haizidi tani 210,000. Nimeamua kuchukua haya machache. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nadhani Waziri wa Fedha umefika wakati ukae na Waziri wa Kilimo tupeane utaratibu kwamba ili tumpime Waziri wa Kilimo mwaka kesho tunataka aongeze tani za kilimo akishindwa then tujue wewe hutufanyii kazi yetu, sasa yeye ndiyo aseme hili niweze kuzalisha tani hizo nyingi ninahitaji uwekezaji huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naona suala la growth hatuhangaiki nalo, siyo sawa, maana hata hii kodi tunayotafuta kama hakuna growth, hakuna production ni kwamba tutaendelea kushikana mashati tu, wenzetu wanafaidi kwa sababu ya economies of scale kwamba hata bei ya dunia ikianguka kwa sababu umezalisha sana bado hutopata taabu.

Suala la pili ni suala la samaki, ukisikiliza hapa ni suala la Waziri wa Uvuvi anahangaika na wavuvi kuchoma nyavu, kukimbizana nao, toka tunaingia ndio kazi tunafanya, lakini leo wenzetu Kenya na Uganda wameanza namna mpya ya kufanya uvuvi, wanafanya vizimba. Maana yake ni nini kwa kufanya vizimba Uganda wamekwenda wamechukua wataalamu Kenya wamewapeleka Uganda kufundisha namna ya kutengeneza vifaranga na kuvigawa bure kama Serikali Kinachotokea leo Uganda na Kenya wataanza export samaki kuliko sisi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tuna Tanganyika, tuna Lake Victoria, tuna Nyasa kwa kweli kutohangaika na hili hatuhangaiki kuondoa umaskini wa watu, tukihangaika na suala la vizimba (cage) wanasema fishing caging fishing ninayo hakika kama Tanzania tutaongeza fedha nyingi za kigeni kwa ku-export samaki, lakini angalia nguvu zetu zinaenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye kuchoma nyavu, kwenye kukamata watu na vipuri vyao, kukamata watu na mashine zao, huko ndiyo nguvu tumepeleka, huko ambako tungepeleka tupate pesa wala hatuendi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukifanya vizimba niwaambie kitakachotokea uvuvi ndani ya maziwa yetu kwa maana ya samaki wataendelea kuwapo kwa sababu ukishakuwa na cage unalisha pale moja kwa moja vinaanguka chini na samaki wengine kule chini wanakua, haya hatufanyi. Kupata kibali cha kuanzisha caging ni shughuli kubwa sana sasa mimi sielewi tunafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la utalii, hivi leo tuulizane Waheshimiwa Wabunge na hii naisema kwa nia njema kabisa, ukiindoa Zanzibar fikiria tungekuwa hatuna Muungano huu, maana yake tungekuwa hatuna utalii wa bahari, beaches Tanzania hazipo, lakini we have the longest beach kuanzia Tanga mpaka Mtwara tunafanya nini? Beach zipo Mungu ametuumba nazo lakini we do nothing. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, so nadhani umefika wakati watu wa Wizara hii waje na mkakati wa kufanya tuwe na beach hotels, tuwe na beach tourism Mungu ametupa, hajatupa kwa bahati mbaya.

Mheshimiwa Spika, kutotumia ni dhambi na mimi nataka leo ni-suggest Serikali tuna mbuga nyingi sana Spika wewe hili unalijua sana, mimi nataka niishauri Serikali tuamue kwamba Ngorongoro na Serengeti ukitaka kwenda kule tuweke kwa watu wenye fedha, tuseme ukiingia kule ni dola 1,000, dola 2,000; tutapata pesa tutashangaana hapa, wale ambao hawana uwezo, hawana fedha iko Mikumi, Selous, Tarangire, iko wapi waende huko, kwa sababu wanyama watawaona, iko Katavi, Ruaha waende huko, lakini ukitaka kwenda Serengeti, Ngorongoro tuseme ni for high and kitakachotokea na mimi nasema hii imetokea Rwanda. Rwanda hawana vitu vya maana, wana nini, wana chimpanzee peke yake, walianzisha dola 750 kwa ajili ya kwenda kuona, ikawa over subscribe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kagame amekwenda Marekani kakutana na watu pale seekerville wakamwambia unaweka hela ndogo ndiyo maana wengine hatuji, wameweka dola 1,500 bado kunajaa, maana yake nini, matajiri hawapendi kubanwa, matajiri hawapendi kuzungukwa na watu wengi. Kwa hiyo bado unaweza ukasema kwa mbuga zetu hizi mbili nitaweka tu hawa na nina hakika watajaa na tutapata pesa nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la biashara, nimemsikia rafiki yangu hapa amesema vizuri sana Mbunge wa Gairo.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Shabiby.

MHE. PETER J. SERUKAMBA: ...Mheshimiwa Shabiby na mimi nataka niende kwenye angle moja, juzi Mheshimiwa Rais alifanya jambo kubwa la kihistoria alikutana na wafanyabiashara, moja ya mambo muhimu sana Rais amesema sijui kama naona hamna anaye-pick up, Rais amesema anatamani akimaliza muda wake atengeneze mabilionea 100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais anatamani Watanzania waende kuwekeza Kenya, waende kuwekeza kwenye SADC, waende kuwekeza kote Afrika, sasa ukitaka kwenda kuwekeza leo nje ya Tanzania, kupata vibali pale BOT ni shughuli kubwa mno, leo una fedha zako kwenye bank account, there is a business unataka kwenda kuwekeza Burundi, brother kupata vibali BOT ni shughuli kubwa mno, kuna over regulation, ukiweka over regulation huwezi kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizi nchi ambazo bado tunakua lazima kuwe na flexibility, leo hapa amesema habari ya magari yote yanakwenda yanaji-register Rwanda na Zambia, nikwambie ukiwa na magari ya transport Rwanda unalipa kodi hii, moja tu shilingi milioni moja basi, hakuna Corporate Tax, hakuna nini, ni shilingi milioni hii mmemalizana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ukiwa na magari 100 wana milioni yao mia moja unaenda unalipa shughuli imeisha, wewe ungekuwa mfanyabiashara utaacha kwenda huko, njoo hapa kwetu, kuna Corporate Tax, kuna OSHA, kuna nani, kuna service levy yote haya ni huyo mwenye magari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa maana ya mfanyabiasha yeyote atakwenda huko, nataka kusema kama tunataka kwenda huko lazima tufanye kama wenzetu, lakini nataka nipendekeze na amesema hapa Mheshimiwa Shabiby suala la VAT kwenye petrol stations mimi niwaombe Serikali na Waziri naomba hili ulitafakari sana, hakuna mwenye petrol station ambaye anajiuzia mafuta? Wote mafuta wanachukua kwenye depot, kama wewe ni mtu wa PUMA unachukua PUMA, kama ni TOTAL unachukua TOTAL. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo leo Serikali ukienda pale PUMA ukamuuliza swali moja tu una petrol stations ngapi atakwambia 50, nipe sales zao au walivyoagiza mafuta kwa mwaka anakupa list yako, akishakupa anakupa na cost unaijua kwa sababu una EWURA, maana yake ni nini, unajua kwa kituo hiki kwa mafuta aliyouza labda lita milioni moja kwa mwaka alipata faida kiasi hiki, atakuonesha cost zake analipa kodi, rahisi tu, rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hii tunaweka, haya amesema naweza mafuta yasifike kwenye petrol station na bado hiyo EFD mashine wala isifanye kazi, so mimi ninachosema tutafakari umefika wakati tupunguze gharama za kukusanya kodi, kwa sababu gharama za kukusanya kodi nazo kubwa sana, kwa hiyo niombe hilo watu wa Wizara ya Fedha mtusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niseme, namshukuru Rais na amesema vizuri sana, tunahitaji tuwe na marafiki na wafanyabiashara, naombeni sana unajua kwa miaka minne hii, nimekuwa namsikiliza sana Naibu Waziri wa Fedha akiwa anajibu hoja Bungeni hapa, siku zote suala la biashara kufungwa halijawahi kumshtua huyu mama hata siku moja, anasema biashara zitafungwa, tunafungua zingine. Ni sawa, lakini jamani hivi kuna nyongeza mbaya? Kama biashara ipo halafu ukafungua zingine hivi ni dhambi? Kwa nini ujidai kwa kufunga? Kama unaona ni faraja nimefunga why? Lakini tunasahau biashara inayoanzishwa leo haileti kodi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tunasahau, biashara ikianzishwa leo haileti kodi hiyo, biashara ikianzishwa leo hailipi kodi, lakini yule aliyekuwepo huyu tuna historia naye. Kwa hiyo mimi ningewaomba sana Waziri ndugu yangu tujitahidi tusifunge biashara na hii habari na mimi naomba sana, hii habari ya kuwa-involve TAKUKURU, watu wa vyombo vya ulinzi kwa ajili ya kodi siyo sawa. Kodi tuwaachie wafanyakazi wa kodi, kodi tuwaachie watu waliosoma kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana leo unasikia pale Wizara ya Fedha wamepangishwa foleni wafanyabiashara, kwani ungemuita Ofisi ya TRA akaenda akakutana na mtu wa TRA kuna dhambi gani, why uwatishe, saini hapa, tunakupa siku saba, uwe umelipa, hii siyo sawa, hii siyo sawa na naamini Mheshimiwa Rais hili halijui, kwa sababu Rais anataka dialogue kwamba wewe njoo ufanye biashara na mimi nifanye biashara na wewe. Naombeni watu wa kodi tubadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho naomba sana suala la Marekani kuna kitu wanaitwa Small Business Act, Waziri wa Fedha naomba utafakari kuleta Small Business Act, kwamba Corporate Tax ni thirty percent, inawezekanaje ACACIA alipe thirty percent na Serukamba Company alipe thirty percent ni watu wawili tofauti hawa, tutengeneze utaratibu kulingana na mitaji ya watu. Tunasema kuanzia mtaji wa milioni mpaka milioni 20 blacket yake iwe hii, kutoka milioni 20 mpaka milioni 100 iwe hii, kutoka milioni 100 mpaka bilioni moja iwe hii, bilioni moja and above iwe hii, maana yake ni nini, watu wana- graduate akifanya vizuri zaidi anapanda kule, on doing this tutawa-incoporate watu wote wataingia kwenye wigo wa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema na mimi hii nairudia tena, Watanzania wengi wote, Watanzania wote wanalipa kodi, tofauti yetu kuna anayelipa direct tax kuna anayelipa indirect tax. Mtu yeyote anayenunua sukari analipa kodi, ukinunua soda unalipa kodi, ukinunua mkate unalipa kodi, wote na ndiyo maana nchi zilizoendelea kama kuna eneo wanahangaika nalo ni suala la employment. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Spika, ukihakikisha watu wako wana kazi, maana yake wana purchasing power, wakishakuwa na purchasing power watatumia, wakitumia watalipa kodi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo na mimi namshukuru sana Waziri wa Fedha, nampongeza sana yeye na watu wake Wizarani kwa kazi kubwa wanayofanya, nakushukuru. (Makofi)