Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti ya Serikali kwa mwaka huu wa 2019/2020. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa vyote kwa kutuwezesha hatimae kuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali na ninampongeza Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Mpango kwa mipango thabiti kutuletea bajeti hii ambayo ni bajeti ya wananchi. Nikupongeze pia Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Ashatu Kijaji kwa ushauri mzuri ambao kwa pamoja na watumishi wote, Katibu Mkuu na pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha kwa ujumla kwa kweli kwa kazi nzuri. (Makofi)
Nampongeza kwa kiasi kikubwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa kwa moyo na uzalendo wake ambao ameweza basi kuita watu mbalimbali na kufanya Ikulu kuwa kweli Ikulu ya wananchi na hasa kwa wafanyabiashara ambao tumeona ni kwa kiasi gani wameweza kueleza changamoto mbalimbali zitakazoisaidia Serikali, nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu nakupongeza kama kiongozi wetu Bungeni, lakini pia kwa mipango thabiti ambayo kupitia Wizara yako Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli bajeti hii na hasa kilimo-biashara nina imani kabisa kwamba kazi inayofanywa kupitia Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu basi tutaweza kilimo kitakachofanywa na vijana pamoja na Wannachi wengine basi kitakwenda malighafi zile kutumika kwenye viwanda.
Mheshimiwa Waziri Mkuu nakupongeza sana na pia Katibu Mkuu na dada yangu Jenista Mhagama hongereni sana, pacha wangu pia Stella Ikupa ninakupongeza sana kwa ushauri mzuri unaompatia Waziri hatimae basi hata yale masuala ya watu wenye ulemavu kwa kweli jitihada zako tunaziona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuchangia katika sekta ya viwanda; tunafahamu kwamba ajenda ya nchi hivi sasa ni viwanda na ili viwanda iweze kufanikiwa hapandipo tunapouona uwezo na nafasi kubwa ya Mheshimiwa Rais wetu kutokana na jitihada anazofanya basi tutaelekea uchumi wa kati kwa mwaka 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kufanikiwa kwenye viwanda ni lazima tuzingatie uwepo wa malighafi na hizo malighafi viwanda vyetu vitakuwa na faida kubwa endapo malighafi hizo zitatumika za hapa hapa nchini na tunaona katika bajeti hii wameeleza kwamba malighafi zaidi zitakazotumika ni kutoka hapa hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na mipango hii ya Mheshimiwa Mpango, Serikali tunaona kabsia kwamba ujenzi wa umeme wa Stiegler’s pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, lakini pia ujenzi wa barabara vyote hivi vitasaidia kwa sababu mkulima atakaelima mazao yake, reli itakapokamilika ni dhahiri kabisa anaweza kufika katika soko la Kariakoo kwa muda mfupi ambapo atakwenda kuuza mazao yake, lakini wale wa vijijini pia ujenzi wa barabara ambako hivi sasa tumeunganishwa maeneo mengi bado Mkoa mmoja tu wa Kigoma na jitihada bado muda mfupi tu hatimae zile kilometa 300 zitakwisha, ninaamini kabisa dhamira hii ya Serikali ndiyo ambayo itakayotufikisha katika uchumi wa kati mwaka 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kiwanda kiweze kufanikiwa ni lazima basi hizo malighafi kama nilivyoeleza, lakini je, katika hizi malighafi Serikali inajipanga vipi kuhakikisha kwamba upatikanaji wake, kilimo hiki kitakuwa ni kilimo chenye tija. Kwa mfano, katika kilimo cha sasa tunaona kabisa kwamba mabadiliko ya tabianchi ni tatizo pia. Katika haya mabadiliko ya tabianchi ni dhahiri kabisa kwamba mvua hizi ambazo tunategemea za msimu basi kama Serikali isipojipanga hatutaweza kufanikisha kwa zaidi, lakini ndipo hapo basi nikasema kwamba Ofisi hii ya Waziri Mkuu na hasa kupitia kilimo cha kisasa ambacho Serikali imejipanga ni dhahiri kabisa malighafi hizi zitakwenda kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango mizuri kupitia kilimo cha kitalu nyumba ambacho ninaamini kabisa, kwa mfano, malighafi ambazo zitahitajika kwenye viwanda vya kutengeneza tomato sauce, nyanya zitapatikana kwa wingi lakini siyo hiyo na vingine vingi vitapatikana. Lakini tatizo kubwa ninaloliona na hapa napenda kuishauri Serikali yangu tukufu kwamba kuzingatia kwa mfano, malighafi ya ngozi hatuna wataalam wazuri wa kuweza ku-process hizo ngozi na hapa ndipo tunapoona umuhimu wa vyuo vya ufundi kama VETA kuona ni kwa jinsi gani vitawafundisha vijana wetu ili basi waweze kuajiriwa kwenye viwanda ambavyo ngozi zinapatikana kwa wingi hapa nchini kufanya basi kazi hiyo na hizo ngozi hata kama zitasafirishwa zisafirishwe zikiwa tayari zimekwishaongezewa thamani kwa ule utaratibu wa kuweza kushughulikia hizo ngozi. (Makofi)
Mheshimoiwa Naibu Spika, lakini pia malighafi nyingi vifungashio bado mni shida. Tunaona kwamba vifungashio vingi bado tunaagiza kwa nchi jirani na hasa wenzetu wa Kenya. Tunawaandaaje vijana wetu na hasa Chuo cha VETA kuona kwamba ni kwa jinsi gani kwa kushirikiana na SIDO ili basi waweze kuboresha zaidi vifungashio katika malighafi zitakazotengenezwa hapa nchini na kwa kutumia viwanda vyetu ili basi tuweze kila jambo liweze kufanyika hapa nchi tusafirishe vikiwa na ubora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunapozungumzia kwamba kilimo, kilimo hiki bado kina changamoto nyingi. Ninaiomba sana Serikali mbali ya kusema kwamba tutawashirikisha zaidi vijana katika Halmashauri zetu tuone tunawasaidiaje hasa wanawake kwasababu asilimia 80 ya wanawake ndiyo wanaofanyakazi zaidi na hasa kule mashambani. Mikopo ikiwepo na kuwawezesha Wanawake waweze kujiingiza kwenye kilimo chenye tija, basi ni dhahiri kabisa kwamba malighafi hizo zitaweza kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza Serikali kwa utaratibu ambao sasa wameona ni vyema uamuzi wake wa kuwa na kitengo ambacho kitasikiliza kero mbalimbali za watu ambao kwa namna moja au nyingine wanashughulikiwa na TRA na hii itaweza kusaidia sana kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema ukweli kutoka moyoni mwangu, TRA wametukwamisha na hapo ndipo ambapo tunaiomba kwa kweli Serikali iweze kuwabaini hawa baadhi ya watumishi wa TRA wasio waaminifu ambao wametufikisha hapa na ikibidi kwa kweli sheria ichukue mkondo wake kwa sababu hawa ni wahujumu uchumi. Tumesikia kero mbalimbali za wafanyabiashara ambazo zimedhihirisha, zimeeleza wazi, wakishughulikiwa hawa ninaamini kabisa nidhamu itakuwepo na kwa nini tusichukue hata ikibidi wakati mwingine kuweka jeshi mfano, kule bandarini tukaweka jeshi ambalo litaweza kusimamia kwa ukamilifu kwa kushirikiana na wafanyakazi wa TRA mapato yakaongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni soko la Kariakoo; tumeona ni kwa jinsi gani ambavyo wengine wameweza kuzungumzia soko hili la Kariakoo. Kilikuwa ni kitovu cha biashara, lakini leo hii siyo ile Kariakoo ya awali, wanasema kujikwaa ndipo ambapo unanyanyuka na kuangalia ni kitu gani kimesababisha wewe uanguke, kwa maana hiyo ninashauri sana Serikali kuona ni kwa jinsi gani tunairudisha Kariakoo, ile Kariakoo ya zamani ambayo ilikuwa ni kitovu cha biashara na hatimae wananchi turudishe imani kwa nchi ambazo zilikuwa zinakuja kununua biadhaa mbalimbali hapa nchini. Kwa mfano Uganda, sasa hivi wafanyabiashara wengi kwa kweli wanakwenda Uganda kwa ajili ya kununua malighafi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mwisho kabisa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa ahsante sana.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga hoja mkono, ninashukuru sana, naitakia kila la heri Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ahsante. (Makofi)