Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ulanga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mkononi nina kitabu kimeandikwa hivi: Ilani ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, ni wakati wa mabadiliko wa kuondoa umaskini chagua CHADEMA tarehe 25 Oktoba, 2015. Kitabu hiki ukurasa wake wa 13 kimeandikwa hivi: “CHADEMA inaamini maendeleo ya kweli yataletwa na Serikali itakayokuwa na nia na mkakati wa kweli wa kupambana, kuondoa rushwa na ufisadi na siyo kwa maneno kama ilivyozoeleka”.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba waende wakatembelee Keko na Segerea watapata majibu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu hicho hicho ukurasa wa 23 kinasema hivi: “Ujenzi wa miundombinu ya afya lazima uendane na huduma husika. Baada ya miaka 50 ya Uhuru ujenzi wa miundombinu ya afya umeelekea maeneo fulani na machache”. Naomba kuwapa taarifa kuwa sasa hivi vituo vya afya 400 vimeshajengwa vimeisha na hospitali 67 za wilaya zinaendelea kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu hicho hicho, ukurasa wa 53 unasema hivi: “Vipaumbele havijawekwa kwenye uendelezaji wa vyanzo vya uzalishaji wa umeme wa bei nafuu vilivyopo nchini, mfano Stigler’s kwenye banio la Mto Rufiji”. Ilani ya CHADEMA hiyo Rais anafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 40 CHADEMA itafanya nini? Kujenga reli mpya na kukarabati zilizopo kwa viwango vya kisasa na kuzingatia maslahi ya nchi ni pamoja na kujenga uwezo wa kuzalisha mataruma na reli nchini vinafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa huo huo wa 40, CHADEMA itafanya nini? Kuboresha bandari zilizopo na kujenga mpya kuwa vitega uchumi vya Taifa ili kuboresha biashara zilizopotea katika bandari za nchi jirani. Serikali ya CCM inafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa huo huo wa 40, unasema hivi: “Kujenga barabara nchini kwa kuzingatia ubora na hasa zile za vijijini.” Tumeanzisha hadi TARURA tunajenga barabara hadi vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa huo huo wa 40, unasema: “Kujenga Shirika la Ndege la Taifa litakalojiendesha kwa misingi ya faida”. Mpaka sasa hivi tumeshanunua ndege saba (7), shirika linaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa huo huo wa 40, unasema: “Kujenga miundombinu ya kisasa ili kuondoa msongamano wa magari hasa katika Jiji la Dar es Salaam na Mwanza”. Fly over za kufa mtu zinajengwa Dar es Salaam. (Makofi/Vigelegele)
TAARIFA
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mlinga, kuna taarifa, Mheshimiwa Eng. Ngonyani.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kumpa taarifa msemaji wa sasa kwamba kwa kawaida hizi Ilani za vyama mbalimbali tunavyoandaa huwa tunadesa. Kwa hiyo, asishangae kuona Ilani ya CHADEMA anayoisoma ndiyo Ilani hiyo hiyo ya Chama cha Mapinduzi.
(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Goodluck Mlinga, endelea na mchango wako.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Taarifa aliyonipa naipokea nilikuwa naelekea huko. Hii Ilani iliandikwa na mtu mmoja anaitwa Mheshimiwa Edward Lowassa na iliandikwa kwa muda wa wiki mbili kabla ya uchaguzi.
(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, yale ambayo alitoka nayo CCM ndiyo alienda nayo CHADEMA kwa kuamini atatumia kuwashawishi watu. Kwa hiyo, usije ukaona leo hii watu sasa hivi wanakomaa na pedi za kike na mawigi kwa sababu hawana cha kuongea.
TAARIFA
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Goodluck Mlinga kuna taarifa, Mheshimiwa Selasini.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumpa taarifa kwamba Ilani ya CHADEMA huwa inatengenezwa mwaka mmoja kabla ya uchaguzi. Hata hivyo, nataka nikubaliane na yote aliyosema na ndiyo maana kila mara tunasema kwamba brain ya kuongoza nchi hii itatoka CHADEMA. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Goodluck Mlinga, endelea na mchango wako.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ukitaka uthibitishe kuwa anachoongea siyo cha kweli, waulize kama Ilani inatengenezwa mwaka mmoja kabla Mgombea wa Urais anapatikana kwa muda gani kwa sababu uchaguzi 2015 mgombea alipatikana kwa wiki mbili. Kwa hiyo, sitopokea taarifa yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yote ambayo wao walikuwa wanayapigia kelele Serikali ya CCM inayafanya. Ndiyo maana leo hii hawana hoja na uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaokuja tunaenda kuwapiga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la kuongeza mapato kwa Serikali. Mimi niliwahi kupeleka kampuni moja kwa Mheshimiwa Dkt. Mpango ambayo ilikuwa inalalamika imeshindwa kusajiliwa nchini, kampuni ya betting, kwa sababu ilianza biashara kabla ya muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna makampuni mengi sana ya betting ambayo watu wengi wa Tanzania wanacheza na hayalipi kodi, hiyo inaitwa online betting. Kampuni ile ilipoenda kufanyiwa upembuzi TRA ililipishwa kodi za shilingi milioni 400. Sasa hiyo ni kampuni moja, je, ni kampuni ngapi ambazo zinafanya betting Tanzania online zikiwa nje ya nchi hazilipiwi kodi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya uchunguzi tukagundua kwa nini watu wanacheza online betting kwa kampuni za nje na siyo Tanzania matokeo yake inaikosesha Tanzania kodi. Sababu kubwa ni game winning tax kwa sababu watu wanaamini wanapocheza kamari kwenye makampuni ya nje wanapata zawadi kubwa ambayo haikatwi kodi lakini makampuni yetu ya Tanzania kuna kodi ya GGR asilimia 25 na winning tax asilimia 20. Kwa hiyo, tunaikosesha Serikali yetu mapato makubwa sana kutokana na game winning tax matokeo yake watu wengi wanacheza kamari za nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ameliongea mwenzangu, niliongea mwaka jana, nalo ni suala la plate number. Plate number za magari haiongezi gharama katika uzalishaji wake utakapoandika jina la mtu, yaani utakapoweka namba ya kawaida na ukaandika jina la mmliki wa gari gharama ya uzalishaji ni ile ile haiongezeki. Nashangaa Serikali kwa tamaa mmeenda kuweka shilingi milioni 10, haya nikiwauliza leo hii watu wangapi wamesajili kwa majina yao baada ya kuongeza hiyo kodi, hakuna hata mtu mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini mngeweka kwenye magari kuandika plate number Sh.2,000,000 na pikipiki Sh.500,000, kuna makabila kama Wahaya wangeandika pikipiki zao zote kwa sababu wanapenda kuonekana. Aidha, Wachaga wangesajili magari yao yote kwa majina. Kwa hiyo, hii ni hela ya bure, Serikali mngefanya hivyo mngepata fedha za bure. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu nalotaka kuliongelea ni utalii. Tujiulize kwa nini Morocco wana National Parks kumi lakini wanaingiza watalii zaidi ya milioni kumi kwa mwaka? Tanzania tuna National Parks 16 lakini tunaingiza watalii milioni 1 kwa mwaka. Hii yote ni kwa sababu hatufanyi promotion za kutosha kwenye utalii wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana ya National Parks Tanzania tuna wanyama wengi. Ngedere wako hadi Ikulu wanamsumbua Rais lakini kwa nini watalii hawaji Tanzania? Ni kwa sababu ya mipango yetu mibovu ya ku- promote utalii inasababisha tusipate watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Balozi wetu wa China, shemeji yetu Mheshimiwa Kairuki anafanya kazi kubwa kwa ajili ya kuleta watalii katika nchi yetu. Watumieni Mabalozi wetu kutangaza utalii siyo Mabalozi wanakaa wanakunywa wine tu huko nje, watangaze utalii wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nilijaribu kuliongelea jana ni balaa la UKIMWI katika nchi yetu. Serikali yetu wameshindwa kubuni mikakati inayoendana na wakati kwa ajili ya kupambana na vita dhidi ya UKIMWI. Matokeo yake kila siku iendayo kwa Mungu vijana 80 wanapata maambukizi ya UKIMWI wenye umri kuanzia 14 - 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, athari yake nini? Kwanza vijana hawa wako katika foolish age, wanaamini hawana cha kupoteza na hawana majukumu mazito. Kwa hiyo, sisi tunaposema Hapa Kazi Tu wao wanasema Hapa Zinaa Tu. Matokeo yake baada miaka 10 hatutakuwa na kina Tulia Ackson, Jenista Mhagama na Angellah Kairuki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali isipofanya mikakati ya dhati kwa ajili ya kutokomeza janga la UKIMWI tutakwisha. Jamii imesahau kabisa kama janga hili bado lipo na ugonjwa huu hauna dawa. Zamani Serikali ilikuwa na mikakati, katika vituo vyetu vya radio ilikuwa kila baada ya matangazo fulani kunakuwa na tangazo la UKIMWI lakini sasa hivi hamna hata TBC yenyewe ukisikiliza unaweza ukakaa siku nzima usione tangazo la UKIMWI. Matokeo yake redio na televisheni zimekuwa ndiyo kwanza vyanzo vya ku-promote ngono na mapenzi. Sasa hivi kila redio kubwa na ndogo ukisikiliza usiku wana-promote mambo ya ngono.
Mheshimiwa Naibu Spika, mitandao ya kijamii, sasa hivi kuna ma-group ya WhatsApp ya ngono, Instagram wana- promote ngono, watu tunajiuza hadharani lakini Serikali imekaa kimya wanasema wanapambana na vita dhidi ya UKIMWI, mnapambanaje?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)