Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Lucy Simon Magereli

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nianze kwa kumshukuru mwenyezi mMungu muumba wa Mbingu na ardhi aliyetujaalia uzima wa kuwepo ndani ya nyumba hii, kujaribu kusema kwa niaba ya Watanzania, kushauri na kuwasaidia wenzetu wa Serikali kuona pale ambapo macho yao hayajaweza kufika au kuona yale ambayo wameyatazama katika namna ambayo Watanzania wengi hawayatazami.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wamechangia na bahati nzuri leo tunakaribia mwisho wa bajeti ya Serikali, wamezungumza mambo mengi kuhusu sekta ambazo zinaajiri Watanzania wengi na namna ambavyo hazijatazamwa. Hata hivyo mimi leo nataka nianze kwa kuwazungumzia ndugu zangu wengine ambao wanachangia sana ustawi wa nchi hii lakini hawapewi kipaumbele, watu hao ni waandishi wa habari.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ninyi ni mashahidi wote kwamba bila waandishi wa habari nchi hii ingelikuwa iko gizani. Ninyi kama watu wa Serikali mnajua kabisa namna ambavyo mnaongozana nao masaa 24 ili yale mnayoyatekeleza yawafikie wananchi, lakini mpaka leo maslahi ya waandishi wa habari ambao wanasaidia na kuchangia maendeleo na upashanaji wa habari mikataba yao ya ajira na maslahi bado ni duni sana. Bahati mbaya Waziri wa Habari hayupo lakini Naibu Waziri yupo, hebu rudini Wizarani mkaangalie namna ambavyo mnaweza mkasaidia tasnia ya habari muwasaidie ndugu zetu wanaotoa mchango wao nao wafaidi na wajisikie Watanzania ndani ya nchi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la usiri ambao unalinyonya Taifa. Mwaka 2017 tulipitisha sheria ya ulinzi wa rasilimali za nchi. Sheria hiyo ililetwa Bungeni kwa mbwembwe, tena ikajadiliwa ndani ya muda mfupi, ikapitishwa, ikaungwa mkono kwa nguvu. Hata hivyo hatimaye mpaka leo ninavyozungumza bado kuna usiri mkubwa sana katika mambo yanayohusu leseni, mikataba na malipo ya Serikali yanayotokana na madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulijua ya kwamba sheria ile ilipopitishwa basi ilikuwa ndio mwarobaini na chanzo cha ulinzi wa rasilimali zetu, na ya kwamba katika katika kifungu cha 12 cha Sheria ya Milki ya Kudumu ya Utajiri na Rasilimali za Asili ya mwaka 2017; katika kifungu kile kinaruhusu ya kwamba mikataba yote inayohusu maliasili na madini na utajiri wa nchi hii kuletwa na kujadiliwa Bungeni lakini mpaka tunavyozungumza leo mikataba hiyo haijawahi kuja na hata hakuna dalili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri wetu, hiki ndicho kati ya vyanzo vya uhakika kabisa vya mapato, lakini hatujapata fursa ya kujadili na kuona ya kwamba Serikali inapata kiasi gani katika mirahaba na mambo mengine yanayohusiana na maliasili na utajiri wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye suala la viwanda. Katika ukurasa wa 31 wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ameelezea vizuri mipango yake. Nilipoanza nilisema nitakusaidia kuona pale ambako haujaona. Mheshimiwa Waziri wa Fedha hatuwezi kujenga viwanda wala hatuwezi kushindana na nchi zinazochipukia kiuchumi kwa mkakati huu tulionao. Tumekiacha kilimo nyuma sana, lakini hata viwanda vyenyewe bajeti kiduchu tunayowapatia haiwezi kuwasaidia kutoka walipo.

Mheshimiwa Mwenyekti, mfano halisi ni bajeti ya mwaka 2018/2019 ambapo waliidhinishiwa shilingi 90 bilioni lakini wakapewa shilingi bilioni 5.4 tu ambayo ni asilimia sita. Mnazungumza habari ya uchumi wa viwanda wa nchi hii utokee wapi kwa asilimia sita ya fedha ya maendeleo unaotolewa? Namwelewa sana Mheshimiwa Mwijage na kilichomkuta, kwa sababu kwa asilimia sita unafanya nini? Bora utumbuliwe ukae benchi kama alivyo leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kuuliza swali; tunazungumzia Tanzania ya viwanda na uchumi wa viwanda; hivi ni nani katika nchi hii leo anayehangaika na kuangalia manpower, labour force, aina ya ajira na kazi tunazozizalisha kwenye vyuo vyetu ambavyo hatimaye vitakwenda kuchangia kuwa rasilimali watu katika Tanzania ya viwanda? Hatushughuliki na hilo kabisa. Vyuo vya VETA vinasuasua, havina fedha havina utaratibu, hata na mitaala yao nayo ni ya kuungaunga wanafundisha mapishi, wanafundisha vitu ambavyo kwa kweli tukizungumza Tanzania ya Viwanda bado mkakati wetu hauwezi kutufikisha tunapotaka kwenda

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala lingine la miradi mikubwa ambayo inasifiwa sana hapa ndani, ya Stiegler’s Gorge, SGR na vinginevyo. Kuna namna ambavyo hii miradi inakwenda kuifilisi nchi na tunakwenda kuibiwa mno kupitia hii miradi mikubwa. Nimesema leo nitawaambia yale ambayo hamja yaona. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Waziri wa Miundombinu hawa wawekezaji ni wajanja sana, wanatuletea BOQ ambazo zina specification za vifaa ambavyo hapa kwetu havipatikani. Nasi kwa sababu tunaharakia tunatafuta 10 percent tunasaini mikataba haraka wanachukua kazi. Mnajua kabisa ya kwamba sisi hatuwezi kujenga na hiyo Stiegler’s Gorge. Reli yetu tukijenga pesa zinakwenda nje, Stiegler’s Gorge pesa zinakwenda nje, upanuzi wa viwanja vya ndege pesa zote zinakwenda nje, ndege tunazonunua pesa zinakwenda nje. Kwa hiyo hii miradi mnaposimama na kuisifia fikirini ya kwamba Tanzania yenyewe inanufaika namna gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, na bahati mbaya sana hii ni miradi ambayo haina ile inaitwa high rate of return siyo miradi ambayo inakwenda kurudisha ile fedha yetu haraka ni miradi ambayo itachukua muda mrefu sana, na pesa zote zinakwenda nje. On top of that fedha tunayojengea hiyo miradi tunakopa kutoka nje na hatima yake hata tukianza kuzalisha au kutokana na kuwakamua wananchi wetu tutawalipa tena watu wale wale ambao waliojenga ile miradi. Kwa hiyo mimi naiita miradi ambayo inaiibia taifa na kututia hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la ujasusi wa kiuchumi. Unajua kuna jambo ambalo tukijaribu kuliangalia nashangaa sisi hatuwezi kuyaona kama ambavyo wanayaona wengine. Matajiri katika maeneo mengine wanapewa fursa za kuwa matajiri zaidi ili walipe kodi na wazalishe ajira lakini huku kwetu sisi tunataka wawe mashetani. Jama…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)