Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa hii nafasi adhimu ili nami niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, sina budi kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Wakuu. Wizara hii viongozi wa juu wamo Wazanzibari, kwa hiyo, naiangalia kama ni sehemu ya Muungano, naipongeza Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa jinsi alivyowajali Watanzania katika bajeti yake kwa kuwaondolea tozo, ushuru wa forodha na VAT. Hapa tunaiona Serikali inavyowajali raia wake na kuwapunguzia ukali wa maisha katika utendaji na ufanyaji kazi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kutoa misamaha kwa viwanda vyetu vya ndani. Hili ni jambo adhimu na kubwa la kuvisaidia viwanda vyetu vya ndani kupata mapato na kuwezesha Serikali kupata mapato lakini kuwanufaisha Watanzania kwa kuyatumia mapato yao wanayochangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ushuru wa forodha naomba uwakilishi uwe wa pande zote za Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Pia kinachopatikana kiwe ni kwa faida ya pande zote mbili. Kwa kufanya hivyo itasaidia kuonesha jambo hili linafanya kazi kwa mujibu wa makubaliano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia taulo za kina mama. Sipingi maelezo yaliyotolewa kwenye kitabu hiki na Mheshimiwa Waziri, yapo sahihi na tunayakubali lakini bado Wizara izidi kuliangalia tena suala hili kwa sababu vijana wetu hawana uwezo. Wizara itafute mbinu ili taulo za watoto ifikie Sh.300 mwisho Sh.500 kwa box ili mtoto aweze kulinunua au hata mzazi maskini aweze kumnunulia mtoto wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, kuna matangazo ya dawa ya mswaki Colgate, wanaambiana vijana/watoto wadogo Sh.300 tu unaweza ukanunua na meno yako yakakaa sawa. Sasa vitu kama hivyo ukiviangalia na ukivisaidia itapendeza na itawasaidia vijana wetu waweze kujikimu lakini maelezo uliyoyatoa nayakubali na hayana matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kulizungumzia suala la Bandari ya Mpiga Duri. Zanzibar inategemea bandari iliyopo Malindi na bandari ile tayari imeshazidiwa maana ni ya toka ukoloni. Sasa hivi tumeamua kuanzisha Bandari ya Mpiga Duri lakini nguvu zetu sisi bado zipo chini ya dhamana na mikono yako Waziri. Naomba hili Waziri uliangalie tena kwa jicho la huruma na imani maana hivi sasa baadhi ya makontena tumeyatoa Malindi kule tumeweka Darajani lakini kwa mazingira haijapendeza na hayajakaa sawa na ile sehemu si nzuri ukiweka makontena maana kuna vijana wanayavamia, wanakwenda kufanya ufuska pale, haipendezi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa kwa huruma na busara zako Waziri utaweka mkono na kutufanikisha bandari ile ikaweza kujengwa utakuwa umeisaidia Zanzibar katika uchumi wake. Uchumi wa Zanzibar ukikua tayari Tanzania itafaidika, itakuwa tayari Zanzibar inaweza kujitegemea na Zanzibar ikaweza kutekeleza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache, naunga mkono hoja. (Makofi)