Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Yosepher Ferdinand Komba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niunge hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani taarifa au hotuba yao ambayo wameitoa hapa wakiwa wanaishauri Serikali kwa mambo mengi na naomba ieleweke kwamba Kambi ya Upinzani haipingi miradi ambayo inaanzishwa ndani ya nchi hii lakini Kambi ya Upinzani imekuwa ikishauri namna bora ya kutekeleza miradi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Kama Kambi ya Upinzani hatupingi kwa sababu tunaamini miradi ikisimamiwa vizuri itakuwa na manufaa kwa wananchi wote, kwa hiyo wale ambao wanadhani tunapinga, hatupingi tunashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nianze na sura ya bajeti, nimesoma Kitabu cha Waziri kwenye ukurasa wake wa 86 ukiangalia sura ya bajeti ina vyanzo mbalimbali ambavyo vinaweza kutengeneza trilioni 33.11 kwanza kuna mapato ya kodi ambayo kwa mwaka jana ilikuwa ni trilioni 17 vyanzo vya ndani vya kodi, mwaka huu imefika trilioni 16.1 lakini tuna mapato yasiyo ya Kodi ambayo ni trilioni 3.18. Tuna mapato yanatokana na Halmashauri ambayo ni bilioni 765.5 kuna mikopo ya masharti nafuu, kuna misaada kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi tumekuwa tukisema humu ziko bajeti ambazo zinalenga watu na ziko bajeti ambazo zinalenga vitu, nimechambua kidogo kwenye Bajeti ya Maendeleo, nimeangalia sekta ambazo zinaajiri au zina watu wengi sana zaidi ya asilimia 70, sekta ya afya, elimu, viwanda, kilimo, maji, mifugo na uvuvi. Hizi ni sekta ambazo Watanzania zaidi ya asilimia 70 wanapatikana humo, sekta ya afya imetengewa bilioni 500 sawa na asilimia Nne ya bajeti yote ya maendeleo, elimu imetengewa bilioni 663 sawa na asilimia Saba, lakini viwanda imetengewa bilioni 51.5 sawa na asilimia 0.4, Kilimo imetengewa bilioni 143 sawa na asilimia 1.2 kuna maji na mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukijumlisha hizi Wizara ambazo ndizo zenye watu wengi unakuta ina jumla ya trilioni 2.1 ambayo ni sawa na asilimia 17 tu ya Bajeti yote ya Maendeleo, lakini hizi Wizara ambazo zina miradi ile mikubwa zina zaidi ya asilimia 55. Kwa hiyo, tunaposema bajeti ilenge maendeleo ya watu na siyo maendeleo ya vitu hatupingi miradi ambayo inaanzishwa lakini hatuwezi ku-compromise afya za wananchi kwa sababu tunajenga Stiegler’s, hatuwezi ku-compromise elimu za Watanzania kwa sababu tunajenga SGR. Hivi ni vitu ambavyo vinatakiwa viende sambasamba tunaambiwa tufunge mikanda wananchi wajikaze mazuri yanakuja, kufunga mikanda tulianza kufunga tangu mwaka 1976 kipindi cha vita ya Uganda, Mwalimu Nyerere alituambia tufunge mikanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba Waziri akija ku-wind aniambie vyanzo vipi mmeviandaa vya kodi ambavyo vita-push kodi za ndani kutoka trilioni 17 ambayo mwaka jana mliikusanya kwa mbinde kwa wafanyabiashara kwa nguvu kwa mitutu na hekaheka mpaka kufika trilioni 19, mmeandaa vyanzo gani rafiki kwa wafanyabiashara ambavyo mtakusanya kodi bila kuwasumbua, ambavyo hamtawa-discourage katika kufanya zao ili muweze kufikia lengo la trilioni 19. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu suala la Pedi, yamezungumzwa mengi mwaka jana tulishangilia sana, Serikali ilipotoa VAT mwaka huu yamerudi tena VAT imerudishwa, niseme jambo moja, wakati Serikali inatoa VAT kwenye pedi wafanyabiashara wa jumla au importers wakubwa walishusha bei, ambao hawakushusha ni wafanyabiashara wa rejareja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Serikali hamkutimiza wajibu wenu katika hili, kama wafanyabiashara wakubwa na importers wakubwa walishusha bei, rejareja ndiyo hawakushusha bei, naamini kwa sababu rejareja ukifuatilia mnyororo wao wa thamani wao wana zaidi ya profit margin asilimia 40 na hata wakishuka asilimia 20 ya profit margin au 25 bado hawapati hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba Serikali Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itoe bei elekezi hamna haja ya kutoa VAT kwenye hili suala, watoto wetu wa kike wanapata shida tuendelee kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara itoe bei elekezi, halafu tuone huyo mfanyabiashara ambaye atakiuka hiyo bei ambayo imetangazwa na Serikali, lakini kitu kingine hili suala, siyo suala la kiuchumi ni suala la kutoa tamko, kama nchi tunaona watoto wetu wanapata shida, wanakosa raha, wanakosa masomo tuwape nafasi, Serikali itoe tamko hapa. Naomba VAT itolewe kama ilivyotolewa mwaka jana wananchi wetu wafurahie.(Makofi)