Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda nikushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi. Pili naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza kwa hadithi moja ambayo inasema: “alamatu-l- munafiq thalatha; idha hadatha kadhaba, waidha’waada akhlafa, waidha’atumina khana; alama za mtu mnafiki ni tatu, akizungumza husema uongo, akiweka ahadi hatimizi na anapoaminiwa hufanya hiana. Hapo hapo kuna msemo kwamba ahadi ni deni na deni hilo utakwenda kulilipa mpaka mbele ya Allah (Subhanahu Wataala). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeanza kwa maneno hayo kwa sababu zifuatazo; napenda kuzungumzia, kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano iliweka ahadi kujenga border post katika Bandari ya Wete mpaka sasa Bandari hiyo haina Border Post. Namtaka Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango akija aje atuambie, kuna kikwazo gani kilichosababisha kutojengwa kwa border post katika Bandari ya Wete? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitazungumzia tena juu ya masuala ya miradi mitatu ya Zanzibar. Huu ni Muungano na tulikubali wenyewe kuungana na kuna ahadi ambazo tuliwekeana kwamba tutatimiza kote kote bila upendeleo. Sasa, sijui katika hadithi hii kama Serikali ya Muungano itakuwa salama na itakwenda kujibu nini mbele ya haki?
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mradi wa barabara ya Wete-Chakechake, hili ni suala ambalo lipo zamani.
Nashangaa, kipindi cha Waziri wa Fedha ambaye amepita, nadhani ni Marehemu, Mheshimiwa Mgimwa, alitia saini mkataba huu wa barabara ya Wete. Sijui kuna chokochoko gani na figisufigisu gani mpaka sasa hivi umekwamisha mradi huu usitekelezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza hili kwa sababu, tunajifanya kwamba watu wa Tanzania Bara na watu wa Zanzibar ni ndugu wa damu. Ni damu gani ambayo inapenda kuangamiza wenziwe? Udugu huu wa makopa hatuutaki wala hatuutamani. Udugu wa kukutana kwenye madishi, huu siyo udugu. Udugu ni kufaana. Tujengeeni barabara hiyo ili mtimize ahadi zenu, siyo kila siku mnasema uongo. Mtu mwongo anajua mahali pake pa kwenda kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumza hili kwa uchungu sana. Barabara takribani kilomita 40 tu zinashindwa kujengwa. Ninyi huku Tanzania Bara mnajenga barabara hata kilomita 1,500 na kuendelea; hivi hamwoni huku ni kuwanyanyasa Wazanzibari? Wazanzibari wamewakosea nini? Wazanzibari mmewafanya, mme, aaah, sijui hata nitumie neno gani! Huku ni ninyi Serikali ya Muungano mnaingia katika alama za watu wanafiki ambazo ni tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuzungumzia suala la mradi wa airport ya Zanzibar. Dar es Salaam mnajenga airport, mmemaliza; terminals zinafika sijui four sijui ngapi? Kule Zanzibar, mnakuona sijui kama kichaka gani? Mpaka leo terminal three imeshindwa kumalizika kutokana na kwamba hamtaki kutia saini. Sijui roho hiyo mbaya mnaipata wapi? Sijui kwa nini mnataka Wazanzibar wasiukatae huu Muungano. Tukisema hivyo tunaambiwa ni wachochezi. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni suala ambalo halikubaliki.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)