Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kidogo. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa mambo makubwa ambayo ameyafanya. Baada ya hapo nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Naibu wake. Mimi niseme, imenitia moyo sana baada ya kuona upande mwingine unapigwa madongo. Ukiona upande mwingile ule unasifiwa ujue kazi huwezi. Sasa maana yake kazi yako ni nzuri, wewe endelea kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo amefanya katika kubadilisha baadhi ya Watendaji wa TRA ambako muda mrefu kumekuwa kukilalamikiwa. Sasa hivi mmeboresha, kuna mabadiliko makubwa ambayo tunayaona sisi ambao tuna macho, yanaendelea kufanyika. Kilio cha watu ambacho walikuwa wanalia cha jinsi ya style ya ukusanyaji bila kutumia mfumo imeanza kupungua na malalamiko ya watu yamepunguza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana utakuta fedha ambazo zitakusanywa mwezi huu zitakuwa zimeongezeka kiasi kikubwa sana. Hata ushauri aliompa Mheshimiwa Rais akutane na wafanyabishara, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, utamsaidia sana. Kwa sababu walikuwa wanakosa sehemu ya kwenda kuzungumza shida zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, kuna Wizara ambazo zimefanya vizuri hasa tukienda kwenye nchi ya viwanda. Mimi nianze na Wizara ya Ardhi. Niseme Wizara ya Ardhi, wamefanya kazi kubwa sana, kwa sababu ukisema unataka maendeleo, unaanzia kwanza kwenye ardhi. Kesi, malalamiko kwenye Wizara ile sasa hivi yamepungua. Watu wamepewa hati na zimeonyesha thamani, wanaweza kukopa na kuzungusha fedha ambazo baadaye zinarudi kwenye mzunguko wa uchumi. Wizara ya Madini baada ya kukutana na Rais, kuna mabadiliko makubwa yameonekana na kodi sasa zinakwenda kukusanywa.

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kuwa na nishati ya uhakika siyo rahisi pato la Taifa likaongezeka. Tumeona wenyewe, kama tunalalamika, basi ni vijiji vichache ambavyo havijafikiwa. Kikubwa zaidi naomba tu kwaMheshimiwa Waziri wa Fedha, ukizungumza nishati unazungumza habari ya usambazaji umeme vijijini na unazungumza habari ya nguzo; na ukizungumza habari ya nguzo ujue asilimia 45 zinatoka Wilaya ya Kilolo ambako barabara zake ni mbovu. Kwa hiyo, namwachia Mheshimiwa Waziri, tutaongea maana yake leo hatuji kuomba fedha, tutajua jinsi ya kuzungumza naye.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vitu ambavyo inabidi tuzungumze, kama nilivyosema, ukiwa na ardhi, umeme, watumishi, maji na usafirishaji, unazungumza habari ya kuinua uchumi. Nimesema Wizara ya Ardhi inakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa umeme, bwawa la maji tunajenga, litaongezea nguvu kule. Tutakuwa tunaongeza nguvu kwenye umeme, lakini kwenye umwagiliaji. Kwa upande wa maji, naishukuru Serikali na Bunge letu kwa kuamua kuunda Wakala. Tukipata Wakala wakawa na bodi yao wamejitegemea kama ilivyo TANROAD, tutafanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika usafirishaji, kama ambavyo tumeona standard gauge na ndege, kazi inaendelea. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo imefanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii, niwapongeze sana timu yetu ya Taifa ambao jana wamefungwa kule Misri. Ukiangalia tathmini, walicheza na timu ya Senegal. Timu ya Senegal, thamani ya timu ile kwa wachezaji ni pound milioni 380. Timu yetu thamani yake ni pound milioni 14. Sasa unaona tofauti yake. Maana yake timu ya Senegal thamani ukizipeleka kwenye fedha za Kitanzania ni trioni 1.1, wakati thamani ya timu yetu ni bilioni 44. Hii inakuja vipi?

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Cecil Mwambe.

TAARIFA

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimpe taarifa msemaji kwamba kama haya tuliyajua, sasa kwa nini tuliamua kupeleka timu yetu badala ya kujipanga na sisi tukafikia hapo walipotaka wengine? (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwambe, ungemwacha amalize hoja yake ili uelewe. Sasa hajamaliza hata hoja, naamini hujamwelewa ndiyo maana unampa taarifa.

Mheshimiwa Mwamoto, endelea na mchango wako.

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nitampa na nauli ili aende akaione kule. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilichokuwa nazungumza ni kwamba tusitake kufurahia kwenda Peponi wakati tunaogopa kufa. Maana yangu nini? Maandalizi, matayarisho ya timu yetu bado. Tunatakiwa sasa tukae tujipange, kwa sababu hawa wamewekeza; hawa wa-Senegal wamewekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, timu nzima ile ya Taifa wachezaji wanacheza nje ya nchi yao, kwa hiyo kwa sababu wamewekeza, fedha zile ambazo zinapatikana sasa thamani yake inarudi kwenye uchumi wa nchi yao na kuongeza pato la nchi. Wachezaji wetu wanne tu ambao ndiyo wanacheza nje ya nchi na thamani yao ndiyo ile ambayo mmeiona. Kwa hiyo, ninachotaka kusema sisi ndiyo Wabunge wa kuishauri Serikali tufanyeje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba, kwa kuwa uwezekano wa kujenga academy kwa nchi yetu siyo rahisi, basi tuwatumie wachezaji aidha wa riadha, ngumi, mpira ambao walifika rank ya Kitaifa kuwasambaza kwenye Shule zote Tanzania hata kwa kuwalipa posho kufundisha michezo baada ya miaka mitatu tutaona nchi nzima itabadilika tutakuwa sawa na wenzetu wengine badala ya kuendelea kulalamika. Kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa ulisikie hilo.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia niwaombe suala la kukuza michezo ya nchi yetu siyo la Serikali peke yake, wadau, TFF na Serikali kama vile ambavyo Mkoa wa Mwanza juzi wamezindua uwanja mzuri ambao Mwenyekiti alikuwa Mzee Kitwanga hapa. Kwa hiyo, haya ndiyo mambo ambayo yanatakiwa yafanyike badala ya kuendelea kulalamika, tusitake tufanye vizuri wakati hatuchangii pia TFF wajikite katika kupanga ratiba vizuri ili mambo yaende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba awe ni Waziri Mkuu au Rais tena akutane na wadau wa maliasili na utalii. Utalii ni sehemu ambayo tunaweza tukapata fedha nyingi sana lakini tumepasahau kidogo. Kwa mfano, juzi kuna Wabunge wamekwenda kuangalia michezo kule, nilitegemea tungewapa hata vipeperushi (brochures), wakaenda navyo wakavisambaza kwa watu kule ili kutangaza utalii wetu, nami tarehe 26 nitakuwa mmojawapo ambae nitakwenda, niombe Waziri husika kama upo kama ni kilo 20 au 30 nibebeshe nitakwenda kufanyakazi hiyo ya kuvisambaza kwa niaba ya nchi yangu ya Tanzania kwa sababu naipenda.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ilikuwa ni nafasi pekee ya wawekezaji, dawati la wawekezaji wangekwenda kutumia fursa hiyo, zile ni fursa kwenda kutafuta wawekezaji kule, dawati likaenda kule lingeweza kutuletea watu kule wa kwenda kupanda Kilimanjaro, Serengeti, Manyara na sehemu nyingine ndiyo fursa zenyewe na sasa hivi ninavyozungumza kuna mechi zinaendelea hapa Tanzania, timu za walemavu za Afrika Mashariki zinapambana pale Dar es Salaam kwa kutumia nembo ya Tembo worriers sasa hizo ni fursa kwamba hata ukichukua wale walemavu ukawapeleka Kilimanjaro wakapanda Kimataifa tunaonekana na watu wanavutiwa kuja kuona mbuga zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nichukue nafasi hii niipongeze Serikali kwa kuwa wametujengea hospitali nzuri sana pale Wilaya ya Kilolo, hospitali ambayo ni ya mfano wa kuigwa ambayo Mheshimiwa Rais huenda akafungua kwa niaba ya nyingine zote. Kwa hiyo, niiombe Serikali muendelee kukusanya mapato kwa kutumia mfumo ambao utakuwa ni mzuri.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika suala la mwisho kabisa niombe kwenye zile mashine za EFD, zile mashine zinazofanyakazi ni chache sana. Ukifanya hesabu, kafanye hesabu ni ngapi unazo na ngapi mabao zinaingia kwenye mfumo wako, utashangaa ni fedha kiasi gani zinapotea nami niko tayari kukupa baadhi ya documents ukihitaji ili uone ambavyo fedha zinapotea. Kwa hiyo ninakuomba huu ni mfumo mzuri kwa sababu kwanza Watanzania sifa yetu kubwa ya Mtanzania ilikuwa ni kukwepa kulipa kodi lakini sasa hivi siyo ujanja. Ujanja mzuri ni kulipa kodi na kuokoka ndiyo ujanja ambao unafaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja.(Makofi)