Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Mohamed Juma Khatib

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MOHAMMED JUMA KHATIB: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mimi nataka nianze na hadithi ndogo tu. Kuna kijana mmoja kule Zanzibar alifunga safari na kaka yake kwenda Mwanza. Alipofika Morogoro akamuuliza hatujafika, akamwambia bado. Walipofika Singida akaamuliza hatujafika, akamwambia bado. Akasema eeh, kumbe hawa wenzetu wa Bara wana roho mbaya sana yaani kumbe nchi yao ni kubwa kiasi hiki lakini wana hasada na visiwa vyetu vidogo hivi kama chawa tu, kama pua, akaambiwa hiyo ndugu yangu ndiyo ilivyo. [Maneno haya siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli mimi niseme tu kwamba Wazanzibar tunapaswa kupewa pole sana kwa kuwa katika Muungano huu maana tumeungana na watu ambao wana hasada. Binadamu si vibaya kuwa na choyo lakini binadamu mbaya ni yule mwenye hasada. Mwenye hasada hata akawa na mali kiasi gani lakini … [Maneno haya siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mohammed Khatib, kuna kanuni inavunjwa, Mheshimiwa Jenista.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe jambo la utaratibu mchangiaji aliyepo kwa mujibu wa Kanuni ya 64(1)(f) na (g).

Mheshimiwa Naibu Spika, lugha nyingine zinazoongelewa humu ndani hazina ladha ya lugha za Kibunge na ulishatoa utaratibu. Sasa husuda hiyo watu wa Bara tuliyonayo ni husuda gani?

MBUNGE FULANI: Hasada.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Hasada. Kwa
kweli mchangiaji atoe hoja, lakini lugha nyingine zinaudhi. Sisi wa Bara na Wazanzibari ni wamoja lakini anazo hoja zake na uhuru wa kibunge achangie kwa kutumia uhuru wa Kibunge wa kuzungumza lakini lugha nyingine kwa kweli, hapana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, amesimama Mheshimiwa Jenista kwa mujibu wa Kanuni ya 64(1)(f) na (g) akieleza kuhusu lugha ya mchangiaji aliyepita kwa maneno anayoyatumia katika kuonesha kwamba upande mmoja wa Muungano una namna unavyoutazama upande mwingine wa Muungano.

Waheshimiwa Wabunge, jana nilisema na nirudie tena kuwakumbusha matumizi ya maneno. Nilikuwa nimekusudia kuzungumza baada ya michango yote ikiwa imekwisha na wakati mwingine inasikitisha kidogo Waheshimiwa Wabunge wanapopiga meza kuashiria kukubaliana na jambo ambalo kama lingetokea upande ambao siyo wangelikataa sana. Kwa mfano, maneno aliyokuwa anayatumia Mheshimiwa aliyekuwa anachangia sasa hivi kazungumza kwa kinywa chake kwamba visiwa vile ni vidogo kama chawa, angezungumza mtu mwingine hapa ndani sasa hivi pangekuwa hali ni mbaya lakini anasimama Mbunge anazungumza kuita sehemu ya Zanzibar kwamba visiwa vile ni vidogo kama chawa. Maneno kama haya angeyatumia Mbunge mwingine sisi humu ndani tungeona kuna shida na hata pia wenzetu ambao wapo nje ya Bunge hili wangeona kuna shida kwa nini Zanzibar inaonekana imewekwa kama chawa. Kwa hiyo, maneno kama haya ambayo yanaleta uchochezi usio na maana yoyote tusiyatumie Bungeni.

Waheshimiwa Wabunge, kwa namna hiyo hiyo, tunavyotumia vitabu vyetu vya dini kuhalalisha tunayotaka kuyasema, hii si sehemu ya mahubiri na kwa sababu hatuna sehemu ya kuanza kuelezea muktadha wa dini fulani ilipotumia maneno fulani ilimaanisha nini, hata hayo Waheshimiwa Wabunge tuyaepuke. Nilitoa maelezo jana kwamba unapochukua vitabu vya dini kueleza jambo lililo jema basi ni vizuri lakini unapochukua mstari wa kitabu cha dini kueleza ubaya wa mtu mwingine unaleta jambo ambalo linaleta tafsiri isiyo njema. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, jana mtu alichukua mistari kadhaa kwenye Biblia ambayo kimsingi kile alichotaka kusema kingeweza kuhalalisha watu kuitwa mkia ama watu kuitwa mikia kwa muktadha aliokuwa anazungumza yeye, nikayakataa maneno yale. Leo Mbunge mwingine anasimama akitumia maneno ya dini kuonesha kwamba kuna watu wanaweza kuhalalishwa kuitwa wanafiki. Sasa Waheshimiwa Wabunge tunaenda mbele tunarudi nyumba na wote tunahudhuria humu ndani, tujifunze kutokutumia vitabu vya dini ambavyo tutatumia hivyo hivyo mwingine atataka kusimama na kuona dini yake imedhalilishwa.

Waheshimiwa Wabunge, si jambo zuri sisi humu tuna utaratibu ndiyo maana tumeweka Kanuni. Huu si mkutano wa hadhara kwamba unaweza kutumia maneno yoyote utakavyo, hapana. Yakizungumzwa maneno humu namna yanavyochukuliwa ni kwamba ni kiongozi kasema, sasa kama viongozi tuchukue dhamana hiyo.

Mheshimiwa Mohammed Khatib maneno ya kuita Zanzibar ni visiwa vidogo kama chawa si lugha ya Kibunge na hairuhusiwi. Zanzibar si ndogo kama chawa. Pia kuonesha kana kwamba pengine upande mmoja wa Muungano una hasadi ama maneno yoyote yanayoweza kutumika kuonesha ubaya fulani si sawasawa, wote tupo humu ndani hakuna mtu aliyejaribu kuonesha kwamba pengine yeye kwa haki yake ya kuzungumza anatazamwa kwa udogo wake ama kwa ukubwa wake.

Waheshimiwa Wabunge, kwa namna hiyo, natarajia kadri tunavyoendelea na tunavyojifunza haya tusirudi nyuma tena kwa sababu sisi wote naamini tunaelewana tukipewa miongozo ya namna hii.

Mheshimiwa Mohammed Juma Khatib endelea na mchango wako, hayo maneno uliyokuwa umeyatumia mwanzo yanaondolewa kwenye Taarifa Rasmi za Bunge.

MHE. MOHAMMED JUMA KHATIB: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napokea hayo maelekezo yako lakini niseme kwamba hasada si neno la kidini. Hasada ni neno linalotumiwa na Waswahili lenye asili ya Kiarabu maana yake ni kwamba ni mtu aliye na choyo iliyopitiliza. [Maneno haya siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

NAIBU SPIKA: Sasa huyo mwenye choyo ni nani? Sasa hapo unataka kusema upande wa Tanzania Bara ndiyo wenye choyo dhidi ya Zanzibar? Mchoyo yuko wapi hapo sasa? Mheshimiwa Mohammed Khatib tusiende huko, hilo neno limeondolewa kwenye Taarifa Rasmi za Bunge endelea na mchango wako. (Makofi)

MHE. MOHAMMED JUMA KHATIB: Mheshimiwa Naibu Spika, mambo haya yanatia uchungu sana kwa kweli, haiwezekani hata siku moja wenzetu huku ninyi mnajenga barabara maelfu ya kilomita lakini sisi kwa mfano barabara iliyotajwa ya Chake - Wete wengine wanasema hapa kwamba ni kilomita 40 haifiki, ni kilomita 25. Sasa ikiwa ni watu ambao wanajinasibu kwamba asili ya Muungano huu ni undugu kama ilivyozungumzwa hapa lakini wengine wanajenga barabara ndefu kiasi hicho wakati wengine barabara ya kilomita 25 inazuiwa. Wengine wanajenga Airport kubwa mikoa mingi tu lakini wengine Airport yao moja tu inazuiwa.

TAARIFA

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib, kuna taarifa, Mheshimiwa kuchauka.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba Sera ya Taifa letu nchi yetu ni mikoa yote kuunganishwa kwa barabara za lami lakini sisi na Morogoro haijaunganishwa na mimi kwenye Jimbo langu toka Liwale - Nachingwea, Liwale - Nangurukuru hakuna barabara ya lami. Kwa hiyo, inapokosekana barabara Pemba haina maana kwamba kuna ubaguzi ipo mikoa ya Tanzania Bara haijapata lami kama ilivyo Pemba hana lami. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib.

MHE. MOHAMMED JUMA KHATIB: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara moja tu ya Dar es Salaam - Moshi inaweza kujenga barabara zote za Unguja na Pemba moja tu. Sasa kama wewe Mheshimiwa Kuchauka hujajengewa nadhani ni tatizo lako mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo Wabunge hapa wamemlaumu Mheshimiwa Dkt. Mpango lakini mimi namtetea hili si suala la Mheshimiwa Dkt. Mpango ni la Chama cha Mapinduzi. Chama cha Mapinduzi hakiko tayari kuona kwamba Zanzibar inaendelea na eti siku hizi wana vikao wanajiuliza kwa nini Zanzibar siku zote kwenye uchaguzi tunashindwa na hasa Pemba kwa nini hatupati hata Jimbo moja? Eti wanafikiria mipango ya uchaguzi huu 2020 unaokuja wafanye dawa ya kushinda lakini nawaambieni kwamba haya ndiyo mambo yanayowafanya Wazanzibar wakainyima kura CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kama ingekuwa Wazanzibar wanaikubali CCM wanaipa kura ni sahihi kabisa kusema kwamba akili zako siyo sawasawa kwa sababu huwezi kumbagua mtu kiasi hiki halafu akaenda kukupa kura, haiwezekani. Kwa hiyo, niwahakikishieni kwamba CCM hata


TAARIFA

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib, kuna taarifa, Mheshimiwa Mattar.

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpe taarifa mzungumzaji, Zanzibar CCM wapo na Chama cha Mapinduzi kwa upande Zanzibar kinashinda vizuri na kura tunapata vizuri na hakuna suala la ubaguzi, tunafanya kazi vizuri. Kwa hiyo, nimwambie kaka yangu na mzee wangu anapoongea aweke maelezo mazuri, kwa utaratibu tuliokuwa nao katika Kisiwa chetu Zanzibar Chama cha Mapinduzi kinashinda vizuri na tunafanya kazi vizuri na CCM, inshalaah, kila mwaka inaendelea kushinda, ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mohammed Khatib, malizia muda wako.

MHE. MOHAMMED JUMA KHATIB: Mheshimiwa Naibu Spika, haya ndiyo yanayothibitisha kwamba CCM Zanzibar haikuchaguliwa na nikasema si kosa la Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa sababu juzi Mheshimiwa Waziri wa Fedha pale Zanzibar alivyokuwa anawasilisha bajeti kwenye Baraza la Wawakilishi, tena niseme kwamba lile Baraza la Wawakilishi 100 juu ya 100 ni CCM, lakini walilalamika kwamba Serikali ya Muungano inakataa kusaini mikataba ya barabara, bandari na ujenzi wa airport. CCM wenyewe wamesema.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Zanzibar CCM haiwezi kuchaguliwa na sababu ni wao wenyewe. Kwa sababu Mheshimiwa Makamu wa Rais ndiye anayeongoza vikao vinavyojadili kero za Muungano lakini kero za Muungano kila siku zinaimarika na yeye yupo na wala hakuna mafanikio yoyote yanayopatikana. Hiyo ni kuonesha wazi kwamba wenzetu wengine wako huku kwa sababu ya maslahi yao lakini hawaitetei Zanzibar. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)