Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia katika hoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo; Tanzania haiwezi kuwa Tanzania ya viwanda kama hatujaimarisha kilimo, viwanda vinavyotegemea malighafi zinazotokana na kilimo. Kilimo chetu ni bado kilimo cha mkono, tunahitaji kuwa na bajeti ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipunguze kodi kwenye pembejeo ili wakulima waweze kulima kilimo cha kisasa na kisicho na kikwazo chochote. Naiomba Serikali itenge bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuwaajiri Maafisa Ugani ambao watawasaidia wananchi kulima kilimo chenye tija ambacho kitatusaidia kupata malighafi za kutosha kwenye viwanda vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi nchini wanafanya kazi kwa kinyongo na bila ubunifu kwa sababu wana madeni yao ya muda mrefu na hasa Walimu, ndio maana elimu inazidi kushuka. Naiomba Serikali ilipe madeni hayo ili kuwamotisha watumishi pia waongezewe mishahara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kodi ya mitambo ya kuchimbia visima; kutokana na uhaba wa maji nchini, naiomba Serikali iondoe kodi kwenye mitambo ya kuchimba visima ili watu wengi wachimbe visima kwani bei ya uchimbaji itashuka na hatimaye tutapunguza tatizo la maji nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuongezeka kodi kwenye nywele za bandia; ni kweli tunahitaji kuongeza pato la Taifa, lakini naomba tungeangalia vile vitu vikubwa kuliko kuangalia kwenye nywele za bandia ambazo ni kama Serikali inawakandamiza wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kodi kukusanywa na TRA; kutokana na kushuka kwa makusanyo kwenye halmashauri zetu na hasa kodi zinazotokana na majengo, naomba Serikali irudishe makusanyo hayo yakusanywe na halmashauri lakini yawekwe moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, taulo za kike, nasikitika kwa kuondoa msamaha wa kodi kwenye taulo za kike. Serikali ifikirie upya uamuzi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya Maendeleo kutokwenda kwenye miradi kwa wakati na pia kupelekwa bajeti ndogo. Katika mikoa yote pesa ya maendeleo imekwenda chini ya asilimia 50, hivyo naishauri Serikali kupeleka kwa wakati na kiasi chote kilichoidhinishwa na Bunge kipelekwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta binafsi, tatizo kubwa ninaloliona ni kwamba Serikali inachukua fedha taslimu kwenda kufanyia miradi kama vile kununua ndege. Nashauri Serikali kutumia sekta binafsi kuendesha miradi hii mikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Liganga na Mchuchuma; naiomba Serikali ifikirie ni namna gani inaweza kuharakisha utekelezaji wa Mradi wa Mchuchuma na Liganga. Kama kuna kikwazo kwa mwekezaji, basi Serikali ibadilishe mwekezaji mwingine atakayekuwa na vigezo vinavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mashine za EFD; mashine hizi ni mbovu kila zikipelekwa kwa fundi unatakiwa kulipa shilingi laki moja na nusu (150,000/=). Naiomba Serikali iangalie upya mfumo wa mashine hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.