Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Tunduma
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kupata fursa hii ya kuweza kuchangia kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kuwapongeza viongozi wangu wa chama hasa Mwenyekiti wetu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa jinsi ambavyo anafanya kazi yake vizuri ya kukiongoza chama hiki lakini pia kuhakikisha chama kinasonga mbele na kinafanya vizuri zaidi na kuwa tishio kwa kweli kwenye Chama Cha Mapinduzi.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nitumie fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru sana wananchi wangu wa mji wa Tunduma kwa jinsi ambavyo wanazidi kuniunga mkono, toka walivyoniamini mwaka 2015 mpaka sasa hivi wanaendelea kunihitaji niendelee kuwa Mbunge wao na mimi nasema kwamba nimejiandaa kuendelea kuwaongoza na kuwahakikishia kwamba nawawakilisha vizuri. Kwa hiyo, mambo yanakwenda vizuri Mheshimiwa Spika hakuna matatizo yoyote.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kikubwa tu…
SPIKA: Hutarajii kuita waandishi wa habari hivi karibuni?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, narudi tu wala usiwe na wasiwasi.Kikubwa tu nilichotaka kuzungumza hapa nilikuwa nimefurahi sana kumsikia Mheshimiwa Rais anasema kwamba uchaguzi utakuwa kama ulivyopangwa na sisi kama Upinzani tulikuwa na masikitiko makubwa sana tulivyosikia kwamba kuna fununu Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi wanasema uchaguzi uhairishwe tulikuwa tunajisikia vibaya kwa sababu tumejiandaa vizuri na tumejipanga vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunafikiri uchaguzi huu ni uchaguzi ambao tunaamini kabisa utakuwa huru na haki lakini pia nimepata moyo zaidi baada ya kuona Mheshimiwa Rais amekutana na wabalozi wa nje na kuwaambia kwamba uchaguzi utakuwa huru na haki lakini Waziri wa Mambo ya Nje amekutana na mabalozi wa nje pia amewaambia utakuwa huru na haki. Nimemwona Simbachawene pia juzi amesema uchaguzi utakuwa hiuru na haki ninaamini uchaguzi huu utakuwa huru na haki watanzania wanahitaji kuchagua kiongozi wanayemtaka na siyo kuchaguliwa kiongozi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme tu zipo tafsiri ambazo zimekuwa ni potofu sana sisi tunasema tunahitaji Tume huru ya uchaguzi wako watu wengine wanafikiri tunavyohitaji tume huru ya uchaguzi tunahitaji kushinda uchaguzi. Sisi hata tungekuwa na tume ambayo si huru tutashinda uchaguzi tu lakini ukweli tunahitaji tume huru ya uchaguzi kwa sababu ya amani ya nchi yetu kwa sababu tunajua kabisa kwamba kama kutakuwa na tume huru ya uchaguzi kutakuwa na uwazi na kila mmoja.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, taarifa
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, atajua kabisa kwamba kura yake aliyopiga
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, na atakayeshinda ameshinda sawasawa…
SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kuchauka.
T A A R I F A
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, nilindie muda wanachosha tu hawa
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji Wabunge wote humu ndani tumeapa kwa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Tume huru imetajwa kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba patakuwepo na katiba na patakuwepo na Tume ya Uchaguzi ambayo itakuwa huru haitaingiliwa na chombo chochote sasa hiyo tume ambayo yeye anaisema kwamba anaidai anataka itajwe vipi kwenye katiba ambayo yeye ataiona kwamba hii tume ni huru.
SPIKA: Taarifa hiyo unapewa Mheshimiwa Mwakajoka.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, unajua hawa ambao sio CCM halisi hawa wana matatizo makubwa sana wanahitaji uhalali wakati CCM halisi wamekaa wanajua nini nachokizungumza tulia kwanza.
Mheshimiwa Spika, tunahitaji tume huru nia na madhumuni ni kuhakikisha kwamba tunafanya uchaguzi ulio huru na haki na tunahitaji watanzania waweze kuona kwamba ndani ya chumba cha uchaguzi yale matokeo yanayotangazwa ni matokeo ambayo yako sahihi na wanaamini kwamba yametangazwa na aliyeshinda ameshinda uchaguzi, tunahitaji tume ya namna hiyo.
Mheshimiwa Spika, sisi hatuna wasiwasi na uchaguzi unaokuja tumejiandaa kushinda kwa asilimia 100 kabisa na safari hii tumesema hatutawaacha ni lazima kwa kweli mng’oke na muhakikishe kwamba mnang’oka kwa sababu zilizo sahihi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina sababu nyingi sana za kuzungumza kwa nini mtang’oka nataka sasa nianze kuchangia mchango wangu kwenye utakelezaji wa bajeti ya mwaka 2019/2020 na uone ni sababu tunasema mtang’oka kwenye uchaguzi unaokuja kwa sababu hamjafanya vizuri.
Mheshimiwa Spika, nakumbuka vipaumbele ambavyo mmeviweka kwenye mpango wa bajeti wa mwaka 2020/2021 mmeweka reli standard gauge, mmeweka Stiegler’s Gorge, mmeweka ununuzi wa ndege na mmeweka bomba la mafuta.
Mheshimiwa Spika, asilimia 75 mpaka asilimia 80 ya watanzania ni wakulima na wafugaji cha kushangaza ni kwamba Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ambayo iliapa kwamba itakuwa ni Serikali ya wanyonge huwezi kuamini kilimo hawaoni kama ni kipaumbele kabisa. Hawaoni ni kipaumbele kwa sababu wanazungumza kwa maneno lakini vitendo hawawezi kutekeleza.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukisoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi, walisema kwamba ndani ya miaka mitano watahakikisha kwamba kilimo kinakua kwa asilimia nane, lakini huwezi kuamini kilimo kimekua kwa chini ya asilimia tatu kila mwaka. Yale ambayo waliyazungumza kwa wananchi wakati wanaomba kura hawajatekeleza hata jambo moja.
Mheshimiwa Spika, nataka nitoe sababu za msingi; angalia Bajeti ya mwaka 2016/2017, tulitenga bilioni 101 wakatoa bilioni tatu peke yake kwenda kwenye kilimo, lakini mwaka 2017/2018 tulitenga bilioni 150 wakatoa bilioni 16 peke yake wakapeleka kwenye kilimo. Mwaka 2018/2019 tulitenga bilioni 95 mkatoa bilioni 42 peke yake.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia miaka yote ambayo tumekwenda kutenga bajeti hizi utaona kabisa kwamba utekelezaji wake miaka yote minne mmetekeleza kwa asilimia 17.55, miaka yote minne. Huu ni utani mkubwa sana kwa Watanzania. Nataka niseme, kama kweli wanataka kuondoa umaskini wa Watanzania ni lazima kuwekeza kwenye kilimo.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukiangalia ukurasa wa 43 anasema Serikali imejikita kuhakikisha kwamba inainua kilimo na kuhakikisha kwamba umaskini unaondoka kwa Watanzania. Sasa kwa uwekezaji wa asilimia hizi ambazo zinawekezwa kwenye kilimo tusitegemee kabisa kwamba tunaweza tukawakomboa Watanzania na tukaondoa umaskini huu. Tunawatania Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachotaka kusema tu; kwa mwaka huu peke yake…
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Frank, pokea taarifa; Mheshimiwa Waziri wa Nchi.
MHE. FRANK J. MWAKAJOKA: Atulie kwanza.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
naomba tu nimpe taarifa Mheshimiwa Frank; anapofanya uchambuzi wa bajeti na kuangalia bajeti ya kilimo, asijikite kwenye Wizara ya Kilimo peke yake. Bajeti ya kilimo ni bajeti mtambuka. Ukija kwenye Vote ya Waziri Mkuu tunao Mradi wa MIVARF na wenyewe unaji-address kwenye Sekta ya Kilimo, uongezaji thamani ya mazao, miundombinu ya masoko, lakini kutengeneza mfumo mzuri wa kilimo kwa wakulima mbalimbali. Kwa mfano mradi huo umefanyika kwa pande zote mbili; Bara na Visiwani. Ukienda TAMISEMI wanayo vote pia ambayo ina-deal na masuala ya kilimo kwa hiyo bajeti ya kilimo ni ya kisekta. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa namwomba anapofanya uchambuzi wa bajeti ya kilimo asi-concentrate tu na Wizara ya Kilimo, aende na kwenye sekta nyingine za kiwizara ambazo zina-support pia Sekta hiyo ya Kilimo na ndiyo atapata majibu sahihi ya Wizara ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia naomba nimthibitishie kabisa kwamba Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli ni Serikali ya wanyonge, hayo ya kilimo ni machache tu lakini yapo mengine mengi ambayo yamekwisha kufanyika na mifano halisi imeelezwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu. Tumeshajenga zahanati, vituo vya afya, hospitali, kwa hiyo kwa vyote hivyo unaona kabisa ni Serikali ambayo inawajali wanyonge.
SPIKA: Nakufafanulia Mheshimiwa Mwakajoka, muda wako unatunzwa usiwe na wasiwasi; alichokuwa anasema
Mheshimiwa Waziri ni kwamba ukitaka kuichambua bajeti ya kilimo lazima uiangalie kwa mapana, sio narrowly, kwamba ukiwekeza katika Mradi wa Stiegler’s Gorge ule wa Mwalimu Nyerere wa kuzalisha umeme, umeme ule utaenda kwenye viwanda ambavyo navyo ni katika mnyororo wa kuboresha products za kilimo. Ukijenga reli itasafirisha na mazao ya kilimo; ukichonga barabara ukaweka lami kuelekea kila mahali ndiyo unafungua kilimo huko; maana yake ni hiyo. Kitazame kilimo katika upana wake huo. Ndiyo ujumbe tu anakupa huo. Unapokea utaratibu huo?
MHE. FRANK J. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, nafikiri Mheshimiwa Mhagama angekuwa anatuambia kwanza hicho anachokizungumza ni asilimia ngapi. Sisi tunapitia randama za Kamati, tunaangalia utekelezaji na ndiyo maana tunachangia hapa, sasa Mheshimiwa akianza kutuambia kuna hela nyingine zimejificha, alipaswa kuziweka wazi. Vile vile akumbuke kabisa kwamba hizo fedha anazozizungumza ukienda kuangalia barabara vijijini ambako sasa tunafikiria wakulima wetu waweze kutoa mazao, barabara ni mbovu, hata mazao hayawezi kusafirishwa sasa hivi. Kwa hiyo anakokuzungumza huko fedha kwa kweli hazijaenda ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, tukumbuke Mkataba wa Maputo kwenye Nchi za Afrika, walishauri kwamba hizi nchi ili ziweze kuondoa umaskini katika nchi zao ni lazima wawekeze asilimia kumi ya bajeti zao kila mwaka ili kuhakikisha kwamba wananchi wao sasa wanalima vizuri, lakini pia wanapata masoko mazuri na baadaye wanaondokana na umasikini, lakini Serikali yetu haijawahi kufikia bajeti hiyo hata siku moja, mpaka tunavyozungumza leo.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Mwakajoka; Mheshimiwa Waziri wa Kilimo.
MHE. FRANK J. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Hasunga mbona unaharibu sasa?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru mdogo wangu kwa mchango wake anaoendelea kuutoa, lakini nataka nimwelimishe kidogo, labda pengine anaweza akawa hajaelewa vizuri; tunapozungumzia asilimia kumi ya kilimo hatuna maana hizo fedha zote lazima ziwe kwenye bajeti ya kilimo.
Kwa hiyo kwa mradi mkubwa kama huu kwa mfano wa ujenzi wa reli ya Standard Gauge maana yake tutasafirisha mazao. Kwa hiyo hela zote zilizoko kwenye uchukuzi zinakwenda kusaidia kilimo. Ukiangalia fedha zilizopo kwenye nishati zote zinasaidia kilimo.
Mheshimiwa Spika, lakini zaidi ya hapo, nataka nimpe taarifa kwamba sisi kama Wizara hatulimi, kazi yetu ni kutengeneza miundombinu na kutengeneza sera za kilimo. Utekelezaji wa bajeti ya kilimo unafanywa kwa kiwango kikubwa na Sekta Binafsi. Kwa hiyo ukitaka kujua kwamba ni kiasi gani kimewekezwa kwenye kilimo maana yake tujue Sekta Binafsi imewekeza kwa kiasi gani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kumjulisha tu mdogo wangu kwamba uchambuzi wa bajeti kama ulivyokuwa umempa anatakiwa achambue kwa undani; ni zaidi ya asilimia 7.5 sasa hivi tumefikia na Tanzania ni nchi ya tatu katika Nchi za Afrika katika kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwenda kwenye Sekta ya Kilimo, ukiangalia katika upana wake kwa kuziangalia sekta zote ambazo zimetenga bajeti.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kumpa taarifa hiyo.
MHE. FRANK J. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, mimi nasema hivi; Serikali ilitenga bajeti ikaja Bungeni tukaipitisha Bungeni hapa. Hizi bajeti ninazozitaja mimi ni bajeti ambazo zimepitishwa ndani ya Bunge zikatekeleze shughuli za maendeleo kwenye Wizara ya Kilimo. Bajeti hizi hazijafanya kazi yoyote, ziko chini ya kiwango. Kuna moja imetekelezwa 2016/2017 kwa asilimia tatu; 2017/2018 kwa asilimia 11; 2018/ 2019 kwa asilimia 16 na 2019/2020 asilimia 15.
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Taarifa iko wapi?
MHE. FRANK J. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, tunazunguka nini badala ya kuzungumza uhalisia…
SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka kuna taarifa, ipokee.
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Spika, namheshimu sana mzungumzaji, Mheshimiwa Mbunge Mwakajoka, lakini nataka nimpe taarifa. Anaonekana anapambana sana kwa kile anachodai kwamba Chama cha Mapinduzi kinakwenda kuondoka 2020.
Mheshimiwa Spika, nimwambie Chama cha Mapinduzi hakiwezi kuondoka kwa takwimu hizo, lakini Chama cha Mapinduzi wamehama mbele hapa, akina Mwakajoka wamekwenda kukaa nyuma kabisa kule, mbele wamewaacha akinamama hawa akinamama mnaowaachia chama hapa mbele peke yao hawawezi kukiondoa Chama cha Mapinduzi madarakani hawa akinamama. Akina Mwakajoka sogeeni mbele hapa maana yake chama kimeachiwa akina mama peke yao…
MHE. ESTHER N. MATIKO: Kuhusu Utaratibu.
MHE. MAULID S. A. MTULIA: …mchanganyike, peke yenu chama hakiwezi kwenda.
MHE. FRANK J. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, unamwachia anaropokaropoka huyo.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.
SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, Kaimu Kiongozi wa Upinzani amesimama, subiri kidogo; Mheshimiwa Halima nimekuona. (Kicheko)
KUHUSU UTARATIBU
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu; najua Kanuni zetu za Bunge zinakataza kutumia lugha za kuudhi, lugha za dharau, lugha za kibaguzi, lugha za kudhalilisha. Sasa nakuomba, kwa sababu tunakuheshimu kama Kiongozi wa Mhimili, kuna maeneo unaweza ukatania, halafu kuna maeneo mengine yanakera na yanachefua.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba umtake Mbunge wa Kinondoni aliyetangazwa kwa utaratibu anaoujua yeye, afute kauli yake.
SPIKA: Aliyefanyaje? (Kicheko)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa, tulieni basi… Mheshimiwa Spika, naomba mtulie…
Mheshimiwa Spika, naomba umtake Mbunge wa Kinondoni afute kauli yake aliyoisema kwamba CHADEMA kwa kuwa hapa viti vya mbele kuna wanawake kwa hiyo hakina uwezo wa kushinda uchaguzi. Kwa hiyo anatuambia Mama Samia Suluhu, Makamu wa Rais wa Nchi hii, anatuambia Mheshimiwa Jenista Mhagama, Mnadhimu wa Kambi ambaye yuko kiti cha mbele hana uwezo wa kukisaidia chama chake kushinda uchaguzi. Naomba umtake afute kauli yake. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana Kaimu Kiongozi wa Upinzani.
Kama nimemsikia vizuri, tusubiriane kidogo, kama nimemsikia vizuri Mheshimiwa, amesema akina Mwakajoka mmerudi nyuma, mmeacha front bench yote akinamama watupu na kweli nikitazama naona akinamama watano wako mbele wao peke yao, akina Mwakajoka wamerudi nyuma, sasa ndiyo alikuwa anazungumzia hicho tu.
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
SPIKA: Mheshimiwa Mbunge wa Kinondoni, weka sawa bwana ili tuweze kuendelea. (Kicheko)
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
SPIKA: Eeh, weka sawa tu bwana tuendelee.
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Naamini umenielewa vizuri kwelikweli kwa sababu mimi ninachojua chama cha watu wote na sio wakati wa mapambano wanaume wanarudi nyuma. Nilichotaka wanaume wasiwe wakati wa mapambano wanakimbia wanarudi nyuma, wanawaacha akinamama peke yao, sikusema kwa nia mbaya, nimesema kuwataka rafiki zangu akina Mheshimiwa Mwakajoka waje mbele washikane mkono kwa mkono, bega kwa bega pamoja washirikiane, isiwe wakati wa mapambano wanaanza kurudi nyuma taratibu mwisho watatoka kabisa. Ndiyo hicho tu nilichokisema, sikuwa na lengo la kubagua akinamama wala nini, nilikuwa nahimiza akinababa nao washirikiane na akinamama kuwa-support, sikusema kwa nia mbaya.
SPIKA: Ahsante. Amerekebisha jamani, amesema anataka bega kwa bega.
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, endelea, dakika zako karibu zinaisha, weka sawa.
MHE. FRANK J. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba unajua wanasema kwamba unapokuwa kiongozi ni vizuri sana ukawa na hekima. Sasa nina wasiwasi sana na Mbunge wa Kinondoni na inawezekana huyu Mbunge ndiyo maana alikimbia majukumu akatangazwa kwa njia anazojua yeye. Kwa sababu maneno haya sio ya mara moja, ni mara ya tatu sasa.
SPIKA: Sasa hapo na wewe unaharibu. Katoa wito tu kwamba uje mbele na wewe. Basi, hakusema zaidi ya hilo; endelea na hotuba yako ili umalize muda umeisha.
MHE. FRANK J. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ngoja niendelee tu kusema kwamba, hiki ambacho nilikuwa nakizungumza humu ndani ya Bunge ni utekelezaji hafifu kabisa wa bajeti uliofanyika na Serikali ya Awamu ya Tano kwenye kilimo; hilo lieleweke hivyo.
MHE. MWIGULU L. N. MADELU: Taarifa.
MHE. FRANK J. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, lakini lingine, wakati huo kila mmoja…
SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, kuna taarifa; Mheshimiwa Mwigulu.
MHE. MWIGULU L. N. MADELU: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mwakajoka ameendelea kusemea kwamba utekelezaji ni hafifu na anafanya reference ya Azimio la Maputo. Nataka nimwekee kumbukumbu sawa kwamba Wakuu wa Nchi walipokutana Maputo, asilimia kumi walizokuwa wanazisemea, aende akalisome lile Azimio, zinaongelea kilimo kwa maana ya agriculture, forestryand fisheries. Ukichukua hizo components za agriculture in the broad sense ya kilimo, misitu na mifugo, sisi hapa Tanzania tulishavuka hiyo asilimia kumi na hiki anachokifanya Mheshimiwa Rais na kama alivyosema Mheshimiwa Jenista, ukienda mpaka ngazi ya halmashauri tumeshavuka muda mrefu mno na tunaelekea kwingine kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wenzetu hawa wasiwe na hii temperate ya uchaguzi, kwa haya mambo ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeshafanya hata ile kusoma namba, sasa hivi hata number plate hamtaiona kwa sababu gari ya Dkt. Magufuli itakuwa mbali mno. Kwa maana hiyo hebu twendeni kwenye facts zilizopo kwenye data na tusiweke blah blah zingine hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilitaka nimpe tu taarifa hiyo ili asiendelee kutumia vibaya muda wake.
SPIKA: Kabla sijairudisha mic kwa Mheshimiwa Mwakajoka ninayo mapendekezo kutoka kwa baadhi ya Wabunge. Wanasema kwa kuwa inaelekea uchaguzi ujao huenda hata Mbunge mmoja wa Upinzani asipatikane, patengwe viti maalum, tutengeneze utaratibu fulani maalum tuuandike kwenye Katiba pale ili tuweke hata viti kumi hivi kwamba hivi sasa tuwape bure, maana sasa kuna hatari kwamba itakuwa hakuna hata mmoja. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Mwakajoka, malizia bwana. (Kicheko)
MHE. FRANK J. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, kwanza sipokei taarifa ya Mheshimiwa Mwigulu kwa sababu naye ana stress sana, Kitila Mkumbo yuko anampumulia mgongoni. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa tu kingine ambacho nataka nimwambie ni kwamba Mheshimiwa amezungumza kuhusiana na ujumla wake kwenye bajeti ya kilimo, akiangalia kwenye mambo ya uvuvi ni miaka yote minne fedha hazijakwenda kabisa kwenye uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Ilani ya Chama cha Mapinduzi pia mliahidi meli tano ndani ya miaka mitano lakini mpaka leo meli ya uvuvi kwenye Bahari ya Hindi haijanunuliwa hata moja. Kwa hiyo yote anayozungumza tunajua nini tunachokizungumza ndani ya Bunge hili. Kwa hiyo kwa kweli utekelezaji ni hafifu sana.
Mheshimiwa Spika, niende kwenye afya; Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye ukurasa wa 26 ameonesha bilioni 256 zimetengwa badala ya bilioni 300 ambazo zilikuwa zinatengwa kipindi cha awamu ya nne lakini anasema utekelezai ni mzuri. Ukweli tu ni kwamba fedha iliyotengwa kwa mwaka huu ni bilioni 544, ndiyo iliyotengwa kwenye bajeti, lakini fedha iliyopelekwa sasa hivi ni bilioni 83 peke yake ambayo ni sawa na aslimia karibu 13. Sasa ukiangalia unaona kabisa fedha zinatengwa lakini haziendi na Serikali hii inasema inakusanya. Juzi Waziri wa Fedha wamesema TRA kwamba wamekusanya 1.7 lakini hatuoni, utekelezaji wa bajeti umekuwa chini ya kiwango kabisa. Sasa nashangaa kama kweli wana uhakika wa kurudi mwaka 2020 kwenye uchaguzi unaokuja.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika,taarifa.
MHE. FRANK J. MWAKAJOKA: …mliowaona mwaka 2015 sio… niwaambie tu ni kwamba…
SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Mwakajoka, nakushukuru sana kwa mchango wako; muda umeisha Mheshimiwa Goodluck Mlinga..