Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu katika Bunge hili la Bajeti.

Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, kwa kuniteua katika kipindi hiki kifupi kuwa Naibu Waziri Kivuli kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Namshukuru sana kwa kuniamini na namwahidi sitamwangusha na sitawaangusha wenzangu. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Hawa inaelekea safari hii wamepewa wanawake watupu. Inakuwaje hii?

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Yah! Inaonesha kwamba ni kwa namna gani wanawake tunaweza kufanya kazi vizuri na kwa uaminifu mkubwa na tukipewa majukumu tunaweza kuyatekeleza kwa uaminifu. (Makofi)

SPIKA: Kwamba Mheshimiwa Mbowe ana imani sana na akina mama, ahsante sana. Endelea tu. (Makofi/Kicheko)

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, naanza kuzungumzia kwa upande wa suala zima la afya na kipekee kabisa nizungumzie suala la Corona, suala linaloendelea katika nchi yetu kwa sasa. Corona imefika, ipo Tanzania, nami naomba sana pamoja na wenzangu wengi kulielezea vizuri sana suala hili la Corona. Napenda sana niwakumbushe akina mama wenzangu, akina baba kuona ni namna gani tunafuata maelekezo ya wataalam wetu wa afya. Tusidharau jambo hili kwani lipo, tutakufa tutaacha watoto wetu; watoto wetu watakufa watatuacha wazazi, inaumiza sana. Tunaoa kwa wenzetu, kwa hiyo, tunaomba sana tujitahidi kufuata maelekezo ya wataalam wetu wa afya.

Mheshimiwa Spika, watu wengine wameshauri kwamba kuwe na angalau mambo mbadala ambayo yanaweza yakafanyika. Hata hivyo kuna mambo ambayo yanaendelea kwenye mitandao ya kijamiii ambayo ni mbadala yanatisha. Yaani unakuta mtu anakwambia chemsha sijui miarobaini, weka tanganwizi, weka ndimu, ukichemsha mpaka unaona yale mapovu yanatoka, mtu anatia kwenye kikombe anakunywa. Jamani, tutauana.

Mheshimiwa Spika, ningeomba sana kwa sababu Mheshimiwa Dkt. Ndugulile unafahamu kabisa pele Muhimbili kuna chuo maalum cha tiba asilia tusaidieni ndugu zangu tutakufa. Kuna mtu juzi alikuwa ana-blend kabisa zile Ndimu anachukua anaweka kwenye Blender ana-blend ameweka pamoja na Tangawizi mule ndani katia kwenye glass na akatoa tahadhari kwamba jamani hii dawa ni chungu kweli kweli lakini Mtu akisikia kwamba inasaidia anafanya anachoweza kukifanya. Tunaomba sana mtusaidie hili janga linatisha na kila mtu anaogopa tunahitaji kupona ndugu zangu na tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu tumuweke kwenye maombi kila mtu kwa dini yale ili janga hili liweze kutuepuka lisije likafika kama walivyofikiwa wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna namba ambayo imetolewa katika kipeperushi cha Mheshimiwa Waziri wa Afya. Namba ile unaweza ukapiga leo ikapokelewa kesho, hii ni hatari sana. Hizi namba watu wanapopiga hii namba ambayo imetolewa kwenye kile kipeperushi ni muhimu sana pengine wana taarifa sahihi kuhusiana na suala la watu ambao wako kwenye maeneo yetu tayari wana maambukizi, tayari wanaonesha dalili lakini hawataki kujitokeza. Kwa hiyo, tunaomba sana kama hii namba inakuwa haiwezekani kupokelewa ziwekwe hata tatu, nne, tano ili angalau kuwe na watu wanaoweza kupokea na kuweza kusaidia nduguzanguni lakini vinginevyo hii namba moja haipokelewi na malalamiko yamekuwa mengi. Kwa hiyo, ningeomba sana Wizara iangalie jambo hili, Serikali iangalie jambo hili, jambo hili ni muhimu, jambo hili ni nyeti, tutakwenda kupona kama tutaambizana ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba ya Waziri Mkuu kuzungumzia masuala mazima ya afya lakini kuna changamoto nyingi sana katika sekta hii ya afya; kwanza bajeti inayotoka huwa ni ndogo pamoja na changamoto zilizopo lakini pili; tumekuwa tukiambiwa zaidi kwamba bajeti inaongezwa kwenye dawa, kwenye dawa, kwenye dawa lakini mgonjwa utampa vipi dawa kama hajapimwa na kugundulika ugonjwa wake? Kwa hiyo, nilidhani hasa kwenye hospitali zetu za rufaa tujitahidi sana Serikali kupeleka vifaa vya kupimia kwa sababu unakwenda wkenye hospitali, unafika kwenye hospitali ya rufaa.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano; nikitolea mfano hospitali ya Kitete-Tabora, unafika pale kuna mgonjwa ana matatizo ya moyo unambiwa machine ya ECO imeharibika ukimuuliza tangu lini imeharibika? Ina mwaka haifanyikazi, mashine ya ECG imeharibika ukimuuliza imeharibika tangu muda gani mpaka leo kabla sijaja humu ndani ya Bunge nimempoigia simu Daktari na kumuuliza mashine imepona ama haijapona? Kaniambia imepona sasa kama imepona kweli ama alikuwa ananidanganya lakini ukweli ni kwamba mashine ilikuwa ni mbovu. Mtu anapewa rufaa kutoka Urambo, kutoka Kaliua, kutoka Ulyankulu aende Kitete, akifika Kitete nako hapati ile huduma anapewa tena rufaa ya kwenda hospitali ya Bugando sasa kuna maana gani ya hospitali kuiita ya rufaa kama haina hata vifaa vya upimaji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo hayo nimeyaona katika hospitali ya Mwananyamala. Nimefika pale nimekwenda kutibiwa nimekuta wazee wengi sana wamekaa pale wakienda kupima moyo. Roho iliniuma sana nimefika pale ilibidi niondoke kabla sijafanya chochote kwa sababu wangeona mimi natangulizwa kuanza kuingia mule ndani wangeumia sana nikajisikia vibaya. Imefika muda wangu kuingia nafika kuna mashine tatu zote zimeandikwa tarehe mpaka na mwaka mashine zile zilipoharibika. Mashine imeharibika tarehe 09.05.2016 ya ECG machine, ya ECO mpaka leo mashine ile haijatengenezwa. Kipo kimashine kidogo tu ambacho ndiyo kinatumika kwa msururu ule na ile ni hospitali ya Mkoa sasa kwa kweli hali ni mbaya. Tungeomba sana pamoja na bajeti mnazoziongeza kwenye dawa ongezeni basi na bajeti kwenye vifaa vya kupimia kwa sababu hizi hospitali zetu za rufaa watu ndiyo tunazozitegemea. Hali ni mbaya kuliko ambavyo tunaelezwa, kwa hiyo niseme tu pamoja na dawa lakini na vifaa hivi viongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la utoaji wa dawa pia limekuwa na changamoto sana. Hospitali ya Kitete ni hospitali ya rufaa lakini ni hospitali inayohudumia Wilaya mbili; inahudumia Wilaya ya Uyui, inahudumia na Wilaya ya Tabora Manispaa ambazo Wilaya hizi hazina hospitali za Wilaya. Bajeti ya hospitali ya Wilaya ya Tabora Mjini imetengwa lakini bado haijatoka hiyo milioni 500 mwezi huu ninavyozungumza. Angalau Uyui wameshapata na wameanza lakini hospitali ile ya Kitete inapokea wagonjwa wengi kutoka Tabora Manispaa pale pale na wengine wanatokea Uyui.

Mheshimiwa Spika, changamoto inapokuja bajeti ya dawa inayopelekwa hospitali ya Kitete ni ile ile ambayo inapelekwa kwenye hospitali zingine za rufaa bila kuangalia kwamba Kitete inapokea wagonjwa wengi ambao wanatoka kwenye Wilaya ya Tabora na kwenye Wilaya ya Uyui. Kwa hiyo, niombe sana bajeti ya dawa iongezwe katika hospitali yetu ile ya rufaa ili iweze kuendana na mahitaji ya watu wanaohitaji.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kuhusiana na suala zima la Msajili wa Vyama; Msajili wa Vyama majukumu yake yanaeleweka lakini yapo mambo ambayo yanatokea katika Nchi hii hatuoni akiyakemea. Kuna baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanatoa kauli ambazo hazipendezi kauli ambazo zinataka kututengenisha, kauli ambazo zinataka kuleta hali ya sintofahamu katika Nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiongozi wa Chama cha siasa anapotoka na kujinasibu kwamba yeye anayo Dola, anaweza akatumia Dola ili aweze kupata Dola hii kauli kwa kweli siyo nzuri. Tumekaa muda mrefu hatujasikia majibu yoyote ama neno lolote likitoka kwa Msajili wa Vyama lakini na sisi tumkumbushe Msajili wa Vyama kwamba sisi tunao Wananchi na tunaamini kwamba wananchi hawa watakwenda kutusaidia na sisi tutakwenda kuingia kwenye Dola kama yeye anaamini katika Dola na sisi tunaamini katika wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimuombe sana Msajili wa Vyama vya Siasa atumie nafasi yake kuhakikisha kwamba anatulinda badala ya kutuvuruga. Kama mtu anatoa matamshi iwe ni kwenye Dola, iwe ni sisi huku wa watu wote kila mmoja anatakiwa afuate Sheria na taratibu za Nchi yetu. Kwa hiyo, ningeomba sana hizi kauli zinazotolewa na viongozi wa vyama vya siasa hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi zisiangaliwe tu kwenye vyama vingine hasa vyama vya upinzani lakini viangaliwe hata kwenye Chama Tawala. Hawa viongozi wa Chama Tawala na matamshi yao yanakuaje na yanaathiri namna gani hapo baadaye baada ya uchaguzi mkuu.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka nizungumze kidogo kwenye suala zima la Tume ya Uchaguzi; hizi kelele zinazoendelea za Tume huru, Tume huru, Tume huru nashukuru juzi ulisema kwamba utakaa na sisi pembeni ili tukuambie kwamba hii Tume huru ni nini, nini ambacho kinatakiwa.

SPIKA: Nataka mseme hapa hapa.

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA Mheshimiwa Spika, muda hautoshi tuna mambo mengi lakini ni vizuri tukikaa tukakueleza nini hasa tunachokitaka katika kuhitaji hii Tume huru siyo kwamba tunasema lakini tuna mambo ambayo tunayaona kwamba hayaendi sawa katika Tume ya uchaguzi kwa hiyo tunataka yawekwe sawa ili mambo yaweze kwenda sawa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, leo tunakwenda kwenye uchaguzi, wanawake tunakwenda kugombea…

SPIKA: Ahsante sasna, kengele ya pili.

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.