Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Gimbi Dotto Masaba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu na mimi kwa kunipa nafasi hii kuweza kusimama katika Bunge lako hili ambalo naamini kabisa kwamba tuko katika Bunge la mwisho kwa kipindi hiki na mkataba wetu unakwenda kuisha wa miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, naomba nitumie nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti wa Chama cha Upinzani Kikuu hapa Nchini kwa kuchaguliwa kwa mara nyingine kuongoza Chama hiki kwa umakini mzuri sana. Pia nimshukuru yeye pamoja na timu yake kuhakikisha kwamba yote yale ambayo yalikuwa yanapita katika nyuso zao, nawashukuru na kuwapongeza kwamba wameweza kuyashinda yote. Mungu awasimamie, tunaendelea kuwaombea, naamini katika harakati za kutafuta Dola yote hayo lazima tuyapitie.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza hotuba ya Waziri wa TAMISEMI; katika hotuba yake mambo mengi yamejikita sana kwenye kuboresha mambo mazuri, hakuna sehemu ambayo amezungumzia changamoto. Sasa nilikuwa najaribu kupata masikitiko pamoja na kwamba amezungumza kuhusu Halmashauri, makusanyo, mapato na mengine, lakini sikuona popote alikozungumza kwamba Halamshauri zetu ziko taabani. Leo nakwenda kuzungumza kwa mara ya mwisho kutetea Halmashauri hususani Halmashauri ninazotoka mimi. Kwa kweli inaleta masikitiko makubwa sana na nikirejea kauli ya Spika wakati juzi anabariki hotuba ya Waziri wakati anahitimisha Waziri Mkuu alisema; “ifikapo tarehe 30 Juni atahakikisha malipo ya Wabunge yote yako tayari”.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninasikitika kusema Mheshimiwa Jafo anapenda kufunga Halmashauri zake zikiwa zinaongoza kwa madeni makubwa kwenye Halmashauri zake kwa Madiwani kudai posho nyingi. Sasa sijajua wakati anahitimisha hotuba yake, nataka kusikia ni kauli gani ambayo ataitoa kuhusu madai ya Madiwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na Halmashauri ninayotoka Wilaya ya Itilima; Madiwani mpaka sasa hivi wanadai posho milioni 502. Madeni ya Benki hayalipiki, fedha za Bima hazilipiki, Madiwani hawawezi kutibiwa na Bima zao hakuna malipo yanayofanyika. Sasa ni ishara tosha kwamba Mheshimiwa Jafo anaongoza idadi kubwa ya Watanzania waishio bila furaha yoyote katika Taifa hili. Haiwezekani Diwani akaitwa Diwani hana chochote, madai ya kuanzia Mwaka 2016 mpaka leo ninavyoongea madeni ni makubwa, ni makubwa. Sasa sijui tunakwenda wapi.

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masaba kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mwanne Mchemba.

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mchangiaji; ni kwamba juzi tu tumetoka kumaliza kukagua hesabu za mikoa yote na halmashauri zote nchi nzima. Kamati yangu asilimia 96 ya madeni ya Waheshimiwa Madiwani wamekamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kumpa taarifa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba umeipokea taarifa hiyo?

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei na ndiyo maana sikutaka kurejea kwenye halmashauri yoyote, zaidi ya halmashauri ninayoingia mimi, umenielewa? Kwa hiyo nimeongea hivyo nikiwa na uhakika na ukitaka documents za madai naweza kukabidhi kwenye meza yako. Hili jambo siyo ndiyo naanza kuliongea, nilishamfuata Naibu Waziri zaidi ya mara moja.

MHE. DKT. SAADA MKUYA. SALUM: Taarifa

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masaba kuna taarifa nyingine kutoka kwa Mheshimiwa Saada Mkuya Salum.

MHE. DKT. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Tunamsikia mzungumzaji anavyosema na Makamu Mwenyekiti ambaye tuko Kamati moja ameelezea situation ilivyo. Sasa ikiwa anachukua sehemu ndogo ya jambo lililokuwepo halafu analitapakanya inaonekana ndiyo situation ilivyo huo ni upotoshaji. Kwa hivyo, tunaomba wakati anachangia aji-confine katika sehemu ambayo yeye yupo na aweke specific area ya kile anachokizungumza kwa sababu sisi tuko kwenye Kamati na situation iko vizuri kama ambavyo Makamu Mwenyekiti ameelezea. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba uneipokea taarifa hiyo?

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei. Itilima siyo Zanzibar, kwa hiyo mimi nazungumza hapa kama Mwakilishi wa Itilima

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge tusikilizane kidogo, Waheshimiwa Wabunge tusikilizane kidogo. Naomba make, lakini Mheshimiwa Gimbi Masaba Wabunge wote humu ndani ni Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo nadhani hilo tulimalize kwa namna hiyo, kwa hiyo wewe endelea na mchango wako lakini Mheshimiwa Saada Mkuya Salum ni Mbunge wa Bunge hili kama wewe, kama Mbunge mwingine yoyote.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ninachokizungumza Kiti chako kinanielewa vizuri sana. Sauti niliyosimama hapa ndiyo sauti ya ninapotoka, sasa nisipozungumza matatizo ya maeneo niliyotoka nani azungumze? Mimi ndiyo Mwakilishi yeye kama ana mambo mazuri kule aendelee, naomba niendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Waziri nimepitia kwa ufupi kabisa, lakini sikuona mahali popote ambapo kuna ugatuzi wa Majimbo au Mamlaka ya Miji Midogo, sijaona popote pale. Hii ndiyo bajeti ya mwisho, tulitarajia hivi vitu tuvisikie lakini sijaona popote pale; na ni kwa nini nilikuwa nafuatilia? Nilikuwa nafuatilia kule Mkoani Simiyu kuna Jimbo la Bariadi Mjini. Jimbo la Bariadi Mjini lina Halmashauri mbili, lakini Jimbo hili lina Mbunge mmoja. Sheria inamtaka Mbunge ahudumu Halmashauri moja sasa kama hili Jimbo lina Halmashauri mbili, lina Wakurugenzi wawili, lina Wenyeviti wa Halmashauri, lina Mabaraza ya Madiwani wote na haya Mabaraza lazima kuwe na Kamati za fedha. Mbunge anapaswa kuingia kwenye Kamati moja tu ya fedha, lakini sisi pale Bariadi kuna Mbunge ambaye ana ratibu Kamati mbili za Fedha ilihali wakijua kabisa kwamba Kamati ya fedha ni siri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kujua kwamba kwa nini ajenda ya ugatuzi wa madaraka haijaletwa wakati kuna Majimbo ambayo yana sifa kabisa ya mgawanyo. Ni nini kinachofanyika pale Bariadi, kuna siri gani katika Jimbo hili kutogawanywa? Kwa hiyo, nataka kauli ya Waziri atuambie ni kwa nini Jimbo hili haligawanywi wakati mamlaka zote linazo, kwa nini? Jimbo hili ni kubwa, lina Kata 31, kwa nini Mzee wangu anateseka na mamlaka mbili ambazo hazina sababu yoyote ya msingi? Kwa hiyo, naomba tafadhali sana watuambie siri ya kutogawanywa Jimbo hili, hilo ni la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nina ombi; hapo Mji wa Bariadi katika Mji wa Lamadi, huu mji unahitaji kufanywa kuwa mamlaka ya mji mdogo kutokana na kwamba sifa zote zipo za kufanywa kuwa Mji Mdogo wa Lamadi pale kwa sababu mapato yote yapo, sifa zote zipo, tuna kila kitu, tuna sekondari tatu, tuna shule za msingi saba, tuna vituo vya Polisi, tuna njia kama tatu zinazoingiza mapato katika Mji ule.

Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa atuambie solution ya Mji wa Lamadi kwa sababu yeye mwenyewe unafahamu ule mji ukifanywa kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo utaleta manufaa makubwa sana. Pia utaleta shule kwa watu wengine kuhakikisha kwamba miji mingine inakua, sasa tunavyoendelea kuona miji inakua halafu tunaendelea kuifunga inakuwa siyo sawa. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha atueleze ni nini hatima ya Jimbo la Bariadi Mjini na Mji wa Lamadi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka kuzungumzia ni kuhusu elimu bure; ni kweli kwamba Mbunge ambaye alisimama hapa akasema kwamba yapo mambo mengi waliyoyachukua yaliyotoka upinzani, nakubaliana naye kwa kauli hiyo, lakini namna yalivyochukuliwa sasa na elimu bure.

Waheshimiwa Wabunge hebu tujiulize hivi elimu bure ni nini? Elimu bure tafsiri yake ni nini? Ni kitu gani tulichokuwa tunalipa kikubwa kwenye shule za msingi. Kama leo mwanafunzi anaenda shule amebeba rim, amebeba sijui nini, mita moja ya kitambaa cha skirt ni Sh.10,000 ili aweze kuvaa ni Sh.20,000 mita mbili, yaani yale mahitaji yote yako kwa mzazi. Nilitarajia kwamba, kama ni elimu bure haya majukumu makubwa yaondolewe kwa mzazi, lakini leo haya majukumu makubwa yote yamebaki kwa mzazi.

MBUNGE FULANI: Ream.

MHE. GIMBI D. MASABA: Ream, mlinzi na kila kitu kwa mzazi sasa tafsiri ya elimu bure ni ipi wakati gharama zote ziko kwa mzazi?

T A A R I F A

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mimi nilidhani kwamba mzazi huyu apunguziwe majukumu ili anavyotafuta fedha hizi zikasaidie maendeleo mengine. Sasa ni kitu gani tunachozungumza nafikiri hili limebaba ajenda nyingine ambayo ni ya uwongo kabisa jamani.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masaba kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hakuna sehemu yoyote palipotamkwa elimu bure inaitwa elimu bila malipo. Miongozo ya Serikali ilikwishatoka kwamba wazazi watafanya hiki na Serikali itafanya hiki, hiyo elimu bure ilikuwa ya upande wa kule. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kuna wakati napata masikitiko sana hata Mbunge anavyosimama anapongeza kila kila kitu hii tuamini ni dhambi, kabisa! Huwezi kupongeza wananchi wako kule wanateseka, dakika saba zote unapongeza. Haiwezekani binadamu akakosa changamoto, kwa nini Serikali hii ina mambo mazuri tu? Huyo huyo Mbunge anayenipa taarifa mimi barabara zote hazipitiki, Serengeti haipitiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimesema lazima tuijue tafsiri ya elimu bure; madawati mzazi, kila kitu mzazi halafu na sisi tumebeba kiholela hoja hii tunasema elimu bure, elimu bure tulikuwa tunalipa nini? Hata kipindi cha Kikwete ada ya sekondari tulikuwa tunalipa Sh.40,000, nani mzazi hana 40,000? Halafu mnaleta hapa slogan ya elimu bure, elimu bure, acheni utani jamani kwenye maisha ya Watanzania, siyo sawa. Eti elimu bure, elimu bure, ipi? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)