Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya na kutuweka hai ndani ya miaka yote mitano hadi hivi leo tukishirikiana vizuri Wabunge wote pamoja na Mawaziri na Mheshimiwa Spika katika kutekeleza majukumu ambayo tulipewa na wananchi wetu ili tuje kuwawakilisha humu ndani ya Bunge. Nichukue nafasi hii kumwomba Mungu aturudishe wote kwa umoja wetu ili tuendelee kuwatumika wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri iliyofanya ndani ya miaka mitano. Nampongeza Rais, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Vilevile, nampongeza Waziri, Mheshimiwa Jafo pamoja na Manaibu wake Mheshimiwa Kandege na Mheshimiwa Waitara kwa kazi nzuri waliyoifanya ndani ya Wizara hii. Nawaombea Mungu awarudishe tena na awarudishe kwenye nafasi zao ili waweze kukamilisha yale mambo mengine ambayo wamepanga kuwafanyia wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuwapongeza na kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Njombe hususani akina mama kwa kujitoa kwa moyo wote katika kuchangia masuala mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha kwamba mipango yote na kazi zote zilizopangwa na Wizara hii zinatekelezeka kwa urahisi. Nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sipongezi tu bila kuwa na sababu, nina sababu za msingi. Naipongeza Serikali ndani ya miaka mitano imejenga vituo vya afya 433. Ndani ya Mkoa wetu wa Njombe tunaishukuru Serikali tumepata vituo vya afya zaidi ya 10. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile niendelee kuipongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Magufuli kwa kazi nzuri waliyoifanya kuhakikisha kwamba wamejenga zahanati 368. Ndani ya Mkoa wetu wa Njombe tumejengewa zahanati zaidi ya 10. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali pamoja na Rais wetu mpendwa kwa kazi nzuri waliyoifanya ndani ya miaka mitano ya kujenga Hospitali za Wilaya 98. Ndani ya Mkoa wetu wa Njombe tumepata hospitali tatu, Njombe DC, Makambako TC na Halimashauri ya Wanging’ombe. Vilevile, tumeona kwamba kuna hela zimetegwa kwa ajili ya wodi zetu, Halmashauri ya Wanging’ombe tunashukuru tumepata, Halmashauri ya Makambako TC tumepata lakini sijui mmetusahau kidogo kule Njombe DC muweze kufanya mambo yaweze kukaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya kazi kubwa sana ndani ya miaka mitano. Kusema kweli kwa kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa Rais naomba Watanzania wampe nafasi tena aweze kukamilisha mambo yale ambayo amekusudia kuyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejenga madarasa 19,808, nina kila sababu ya kuipongeza Serikali. Serikali imejenga maabara 227 ndani ya miaka mitano na matundu ya vyoo 7,922. Hongera sana kwa Serikali, hongera sana kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile shule zetu zimeweza kupata madawati 5,070,896, hongera kwa Serikali. Serikali haikuishia hapo imefanya kazi kubwa ya kukarabati shule kongwe 73 zikiwepo baadhi ya shule ndani ya Mkoa wangu wa Njombe. Sisi watu wa Njombe ni wa shukrani, tunaishukuru Serikali na tunaahidi hatutafanya makosa Oktoba, 25. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze pia Serikali imejitahidi, imejenga barabara kilometa 74,940. Hayo yote ni mambo mazuri ambayo yamefanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Jemedari wetu, Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mpango mzuri ambao Serikali imeweka kwa ajili ya bajeti ya mwaka 2020/2021. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Jafo na Manaibu wake na timu nzima pale Wizarani kwa mkakati mzuri waliojiwekea wa kuhakikisha kwamba watakwenda kujenga maabara saba (7) na zahanati tatu (3) katika kila Halmashauri. Mimi sina cha kusema zaidi ya kuwatakia kheri Mawaziri hawa na Rais wetu na timu nzima, Mungu awape afya njema ili waje kutekeleza yale walioyokusudia kuyafanya. Kwa maana hiyo, namwombea Mheshimiwa Rais arudi, namuombea Mheshimiwa Waziri Jafo na Manaibu wake warudi Ubunge na kwenye nafasi zenu ili muweze kuifanya kazi hii vizuri na muikamilishe vizuri ndani ya miaka mitano mingine inayokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nikutakie kheri wewe pamoja na Mheshimiwa Spika na Wabunge wote kila kheri turudi kukamilisha yale ambayo wananchi wetu wametutuma tuje kuukamilisha kwa umoja wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuwashukuru kina mama wa Mkoa wa Njombe kwa kuniamini na kwa kweli nimewatendea haki kama mnavyoniona na kila siku sichoki kuuzungumzia Mkoa wa Njombe. Kwa hiyo, nitumie pia nafasi hii kuwaomba ridhaa wanipe tena miaka mitano ili nije kukamilisha yale ambayo nilikuwa nimepanga kuja kuyazungumzia.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)