Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Mbozi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hii bajeti ya Wizara ya TAMISEMI. Awali ya yote naomba kwanza kuwashukuru viongozi wangu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo ngazi ya Taifa, kwa kuendelea kuwa imara licha ya changamoto mbalimbali ambazo wameendelea kupitia na wafahamu kwamba, siku zote ili dhahabu ing’ae lazima ipite kwenye moto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo, naomba niende moja kwa moja kwenye hoja ambazo nimezipanga kuzizungumza siku ya leo na hoja ya kwanza naomba nianze kwenye eneo lile la TARURA:-
Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA ni chombo ambacho kiliundwa, lakini chombo hiki kimekuwa sasa ni kama pambo tu kwa sababu, chombo hiki hakipewi fedha. Nchi hii ina vijiji zaidi ya elfu 12, leo TARURA inayosimamia barabara zote za vijiji zaidi ya elfu 12, barabara zote za mijini, eti inapewa fedha 30% tu, lakini fedha hizo nazo wakati mwingine haziendi kama ambavyo tumeziidhinisha kwenye Bunge hili. Kwa hiyo, nashauri kwamba kwenye TARURA hapa yafanyike mabadiliko kidogo kwenye sheria, angalau iwe asilimia 50 kwa 50 ili mwisho wa siku TARURA iweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzisha TARURA bila kuwapa fedha maana yake hamna kitu ambacho tumekifanya. Watu wanalipwa mishahara pale TARURA, lakini fedha haziendi kama ambavyo zimeidhinishwa na Bunge. Kwa hiyo, nishauri tu kwamba, licha ya fedha kidogo hizo ambazo hazipelekwi kwanza ziwe zinapelekwa, lakini zaidi ili kuweza kwenda vizuri ni jambo jema kama tutaenda kubadilisha sheria ili iwe asilimia 50 kwa 50 ili mwisho wa siku TARURA iweze kuwa na fungu la kutosha, vijiji zaidi ya elfu 12 ni vingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, hii mvua iliyonyesha kuanzia mwaka jana na inaendelea, katika maeneo mengi nchini karibu barabara nyingi za vijijini na za mijini zimekatika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo langu kuna barabara ya kutoka pale Kijiji cha Ivwanga kwenda Mbozi Mission, Mbozi Mission kule kuna hospitali kubwa ya mission, lakini pia kuna Chuo cha Nursing pale cha Serikali, lakini kuna soko kubwa, lakini barabara hiyo pia inaenda hadi Jimbo la Mheshimiwa Hasunga, Kijiji cha Iganduka. Sasa barabara hii ina hali mbaya sana kuliko Waziri anavyofikiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna barabara nyingine ya kutoka Mloo kwenda Isansa Kituo cha Afya, imekatika, ina hali mbaya kwelikweli, lakini yote haya ni kwa sababu hizi barabara zinasimamiwa na TARURA na TARURA inapewa pesa kidogo, kwa hiyo, mambo yamekuwa ni mabaya kweli na yamekuwa ni magumu. Madaraja mengi yameharibika kwa hiyo, nashauri sheria hapo iweze kurekebishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine nadhani pamoja na mapambano ambayo yanaendelea kuhusu ugonjwa wa corona nashauri kwamba, pia Serikali ingeangalia kutenga fedha kama dharura kwa ajili ya kuweza kurudisha hali ya miundombinu ya barabara ambayo imeharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba nizungumze suala la kuhusu vituo vya afya. Ukurasa ule wa 54 limezungumzwa suala la vituo vya afya na tumeambiwa kwamba, vituo vya afya vimefikia sasa 968; unapozungumza kutoka mwaka 1961 tangu nchi hii ipate uhuru unazungumza vituo vya afya 968 na kata ambazo tunazo kwenye nchi hii ni zaidi ya kata elfu nne na kitu, maana yake tuna upungufu; ukienda kwenye Sera ya Afya, tuna upungufu wa vituo vya afya zaidi ya elfu tatu na kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Afya inasema kituo kimoja cha afya kwenye kila kata, leo unazungumza vituo 968. Yaani leo tukisema tuongeze miaka mingine ya Serikali hii ya CCM kukaa madarakani miaka mingine 59 kwa speed hii ambayo inaenda, maana yake unazungumza kutakuwa na vituo elfu moja mia nane na kitu vya afya, kama ndio watakuwa wanaenda hivi, ambapo maana yake miaka 59 ni mingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vituo vya afya ni vichache kweli, wakati mwingine watu wanakaa wanampongeza Mheshimiwa Jafo tunakupongeza unafanya nini, wakati mwingine mnamharibia Mheshimiwa Jafo kwa sababu mnatakiwa mmwambie kwamba, kosa liko hapa, ili Mheshimiwa Jafo aweze kusonga mbele. Leo vituo 968 ni vichache mno, yaani tuwaongeze miaka mingine 59 au 60 ndio muwe na 1800, bado hamuwezi kukamilisha vituo vyote kwenye kata zote zaidi ya elfu nne na kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huu ni mwendo wa kinyonga, siwezi nikaendelea kumdanganya rafiki yangu Mheshimiwa Jafo, kaka yangu kwamba, anafanya kazi nzuri wakati naona speed ni ndogo. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, ni vizuri Sera ya Afya iweze kutekelezwa, kituo kimoja cha afya kwenye kila kata ili mwisho wa siku nchi hii tuweze kuwa na vituo vya afya kwenye kila kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni jambo ambalo linashangaza sana. Mimi kwangu pale nina kata moja inaitwa Mlowo. Hii kata ina wakazi karibu laki moja, kuna zahanati ya kijiji kwenye kata hiyo; zahanati ya kijiji tu, wakazi zaidi ya laki moja.
Sasa kwa mazingira kama haya unaweza ukawa ni Mbunge mwendawazimu pekee ambaye unaweza ukaanza kupongeza mambo kama haya, wakati watu zaidi ya laki moja hawana kituo cha afya wana zahanati; kwa hiyo, nishauri jambo, Sera ya Afya itekelezwe, kituo cha afya kwenye kila kata, hapo nadhani tutakuwa tumetatua tatizo la vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa ule wa 141 wa hotuba ya Waziri amezungumza kuhusu kwamba, mwaka huu wa fedha 2020/2021 TAMISEMI imepanga kusimamia shughuli za utawala bora, kukuza demokrasia, ushirikishwaji wa wananchi na kadhalika. Kwenye nchi hii kumetokea tatizo kubwa sana, leo wale Mameya au Wenyeviti wa Halmashauri waliochaguliwa kidemokrasia kabisa hasa kupitia Vyama vya Upinzani wanaondolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Meya mmoja wa Iringa pale anaitwa Alex Kimbe ameondolewa kinyume kabisa na utaratibu. Sheria inasema ili kumwondoa huyu Meya inatakiwa angalao 2/3 ya kura iweze kupigwa; Manispaa ya Iringa yenye Madiwani wote kama 24 ilitakiwa wafikie angalau Madiwani 17 kumwondoa Meya wa Iringa. Wameingia madiwani wa CCM 14, walihitajika Madiwani angalao wafike 17 ndio waweze kumuondoa Meya, leo Madiwani 14 wamevunja sheria, wamemwondoa meya kisa anatoka CHADEMA, hilo tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini tu kwamba, yote haya, huu mpango wa Serikali kwamba, wanataka kusimamia shughuli za utawala bora, hilo jambo haliwezekani. Nimwambie jambo Mheshimiwa Jafo rafiki yangu kwamba, ameshawahi kuongea Desmond Tutu, ameshawahi kusema naomba nimnukuu: “if you are neutral in situation of injustice you have chosen the side of the opressor.”
Mheshimiwa Naibu Spika, hiki kinachofanyika kwenye nchi hii hawa watu wanaondoolewa kinyume na utaratibu kwa kweli, huku ni kunyanyaswa na huo ni uonevu na Mheshimiwa Jafo kama amenyamazia uonevu huu, maana yake na yeye anaungana na Wakuu wa Mikoa wote wanaosababisha uonevu uendelee kwenye nchi hii. Ninapozungumza hapa Meya wa Dar es Salaam, Isaya Mwita, aliondolewa kinyume na utaratibu. Kabisa wanaingia kupiga kura hawana 2/3 wamemwondoa kinyume kabisa, kihuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwambieni ukweli kabisa mambo haya yanaumiza na Mheshimiwa Jafo kunyamazia mambo haya maana yake naye anaungana na yule ambaye anaenda kufanya matendo ya uovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme tu kwamba, haya mambo yanaumiza sana. Nchi hii hata siku moja haitakaa kikae Chama cha Mapinduzi peke yake, lazima vyama vya upinzani viwepo na vitaendelea kuwepo tu. Sasa mazingira kama haya ni mazingira ambayo yanatia hofu sana na utawala bora kwenye nchi hii umeingia katika majaribu makubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine pia, hapa ambalo naomba nizungumze kidogo kuhusu suala la ahadi ya milioni 50 kwenye kila kijiji. Nawakumbusha tuambieni kijiji gani ambacho milioni 50 imepelekwa? Kwa sababu, hapa tumeona watu wanajigamba, wametekeleza, vituo vya afya, sijui vitu gani, lakini milioni 50 iliyokuwa imeahidiwa kwenye kila kijiji wamepeleka shilingi ngapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu nina vijiji karibu 121 na nahitaji bilioni sita karibu na milioni 50, maana katika vijiji 121 vya Halmashauri ya Mbozi hawajapeleka kwenye kijiji hata kimoja. Watekeleze ahadi hiyo na ahadi ya laptop kwa kila Mwalimu; wamepeleka laptop ngapi kwa Walimu wa… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)