Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia kusimama katika Bunge lako hili ninaamini hii ni bajeti ya tano na kwa lugha nyingine ni bajeti ya mwisho kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu wenzangu wengi wamempongeza Mheshimiwa Rais na wamesema sababu mbalimbali. Lakini naamini kwamba ili awe Rais lazima kuna michakato ilianza mchakato wa kwanza Rais alitokana na Chama cha Mapinduzi. Mwaka 2015 Mheshimiwa Rais alikabidhiwa Ilani kutoka kwenye Chama chake cha Mapinduzi, Ilani ambayo ilikuwa imeainisha mambo mbalimbali ambayo yatatekelezwa katika kipindi hiki cha miaka mitano. Naomba niseme kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zaidi ya yote Mheshimiwa Rais ni binadamu kama binadamu wengine anapofanya vizuri ni lazima tumpongeze na kumpongeza ni kumtia moyo ili aendelee kufanya vizuri naomba niungane na wote ambao wanampongeza tulioko ndani ya Bunge lakini na wale walioko nje ya Bunge kwa sababu sote tunaona kazi nzuri ambayo inafanyika na Mheshimiwa Rais hakika tunampongeza na tunaendelea kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kuwatumikia wananchi katika taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nikupongeze wewe ambaye leo umekalia kiti lakini ninaamini kabla ya wewe yupo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii taasisi ambayo umeisimamia ni taasisi kubwa sana mmetusimamia watu wengi wenye tabia tofauti tumekuwa tukiona katika taasisi zingine mbalimbali watu hawamalizi wakiwa wamoja lakini naendelea kuamini kwamba tunamaliza Bunge tukiwa wamoja hongereni sana na In Shaa Allah Mwenyezi Mungu aendelee kuwaweka ili mushike nafasi hizo katika kipindi kijacho. Ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme mambo machache kupitia Wizara hii ya TAMISEMI nafahamu kwamba tunajadili mapato na matumizi katika Wizara hii ya TAMISEMI lakini kabla sijasema yale ambayo nayakusudiwa pia naomba nimpongeze kaka yangu Jafo. Watu wamemsema kwa sifa mbalimbali. Naomba niseme sifa moja miongoni mwa sifa alizokuwa nazo Mheshimiwa Jafo ni msikivu hana unyanyapaa kwa Wabunge wenzake ukitoka ukienda kumpelekea hoja yako anakusikiliza na amekuwa akitusaidia katika kutekeleza mambo mbalimbali katika Majimbo yetu nakuombea kaka yangu endelea kufanya vizuri na In Shaa Allah wananchi katika Jimbo lako watakuona utarudi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la mikopo ya 10% nafahamu kwamba tunazungumza mikopo ya 10% ni pesa ambazo zinatokana na mapato ya ndani katika halmashauri zetu. Hizi 10% tumezitenga katika maeneo matatu 4% vijana, 4% wakinamama na 2% ya walemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo naomba niseme katika eneo la walemavu mikopo hii inatolewa kwa kuunda vikundi mbalimbali sasa nilikuwa naomba nishauri kupitia Wizara hii kwamba katika uundaji na utoaji wa mikopo hii ya 2% kwa upande wa walemavu, ziko changamoto zingine ambazo zinajitokeza katika utekelezaji inawezekana kabisa walemavu wapo katika maeneo mbalimbali unaweza ukakuta kijiji kimoja kina mlemavu lakini kijiji X hakina mlemavu ndani ya kata lakini sifa mojawapo ya hawa walemavu kupata mikopo ni kujiunga katika vikundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba jambo hili liangaliwe kwasababu tumeweka jambo hili mahususi kwa upande wa walemavu ikiwezekana wakopeshwe hata mlemavu mmoja mmoja siyo lazima wakopeshwe kupitia vikundi. Nafahamu kwamba wanapounda kikundi mara nyingi kinatakiwa kikundi cha watu wanaoaminiana sasa huwezi kutoka kwenye kijiji X ukaenda kumpata kwenye kijiji B mlemavu mwingine ili muungane watu ambao hamfahamiani inakuwa haipendezi na kwa namna nyingine inaweka ugumu katika kuwasaidia hawa walemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana sana tuwaangalie sana katika kuwasaidia hawa walemavu kulingana na ile dhamira ya Serikali tupunguze masharti kwa upande wa walemavu. Ikionekana kwamba kuna mlemavu ambaye yuko kwenye kijiji X amekidhi vigezo vya kukopeshwa bila kujali yuko katika kikundi basi ni vizuri Serikali ikamuangalia na nafahamu hili Mheshimiwa Jafo analiweza kwasababu liko ndani ya utekelezaji wake tuendelee kuzishauri halmashauri zetu ili na wale walemavu waweze kupata hii mikopo bila kuwa na masharti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema hivyo kwa sababu mwisho wa siku wakipata mikopo wanatakiwa warudishe sasa kama hawatakuwa watu wanaoaminiana inakuwa ngumu katika kuwafuatilia. Naomba nilisisitize hilo kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu tuwasaidie walemavu kwa kupunguza masharti kama nilivyosema Mheshimiwa kaka Jafo unaliweza liko ndani ya uwezo wako. (Makofi)

Jambo lingine naomba nipongeze Serikali kwa suala la ukarabati wa vituo vya afya. Vimeelezwa hapa vituo vya afya 433 ninaamini ni miongoni mwa vituo ambavyo vipo katika mkoa wangu wa Ruvuma, tumekarabati baadhi ya vituo vya afya na nafahamu kwamba lengo la kukarabati vituo vya afya ni kuweka huduma karibu kwa wananchi na sote tunafahamu tulikotoka ilikuwa siyo rahisi kuona kwamba kituo cha afya kinaweza kutoa hata huduma ya upasuaji kwa mama mjamzito. Lakini kwa vituo hivi vya afya ambavyo kwa sasa vinakarabatiwa vina lengo la kuokoa maisha ya akinamama wajawazito na watoto. Nasema hongera sana kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine pia naomba nizungumzie kwenye suala la ukamilishaji baadhi ya zahanati kaka Jafo umesema kwenye taarifa yako kwamba ni milioni 150 katika kila halmashauri nafahamu ziko halmashauri mpaka ziko zahanati mpaka leo hatujafanya vizuri na kuna maboma, kwa hiyo, ni vizuri tukaziangalia zile zahanati ambazo tayari tulishaanza kuzikarabati lakini zimesimama kwa ukosefu wa pesa, kwa hiyo, pesa hizi zielekeze kwenye kukarabati katika zile zahanati ambazo tayari Serikali ilishapeleka pesa lakini zimesimama kwa ajili ya kukosa pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nimeona mambo mbalimbali ambayo yanaendelea katika mkoa wangu ikiwemo ujenzi wa hospitali katika Jimbo la Madaba ambapo bilioni 1 imetengwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali. Naona umewasha taa naomba nimalizie suala dogo tu kwa ridhaa yako na unafahamu kwamba katika uchangiaji huu mimi ni mtoto wa mwisho. Kwa hiyo, naomba na mtoto wa mwisho anahitaji kuvumiliwa naomba univumilie kama dakika tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala moja suala la milioni 140 kukamilisha maboma katika shule za msingi nasema niliseme hili kwa sababu nafahamu yako maboma mengi yamejengwa kwa nguvu za wananchi, wananchi walifyatua tofali wananchi walisomba mchanga wananchi walikusanya mawe lakini maboma yale hayajakamilika naishukuru sana Serikali niombe pesa hizi ziende zikafanye kazi iliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunivumilia naunga mkono hoja. (Makofi)