Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa fursa ya kuzungumza katika Bunge lako hili tukufu. Kama ulivyotamka majina yangu naitwa Husna Juma Sekiboko, ni Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Spika, nina na mambo machache ya kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Rais zilizowasilishwa katika Bunge la 2015 na hotuba yake mwezi wa kumi na moja 2020 kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda napenda nitumie kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hotuba nzuri ambayo imetoa mwelekeo wa namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi chake hiki cha pili inakwenda kutekeleza masuala mbalimbali ya kimaendeleo katika nchi yetu. Vilevile nikupongeze wewe Mheshimiwa Spika kwa namna ambavyo umeonesha uhodari mkubwa katika kuongoza shughuli za Bunge hasa kwa sisi ambao ni wapya tunaendelea kujifunza na kuimarika kwa haraka, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya kwanza imezungumzwa sana na Waheshimiwa Bunge waliokwishatangulia kuchangia kuhusiana na uchumi wa nchi yetu. Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ameeleza namna ambavyo Serikali anayoiongoza angependa ipige hatua kubwa zaidi katika masuala mazima ya uchumi. Katika kuelezea hilo Mheshimiwa Rais amekazia katika sekta ya kilimo na ameeleza kabisa kwamba Wizara atakayoiunda ambayo tayari ameshaiunda sasa atatamani ishughulike moja kwa moja na ile mifuko ambayo inasaidia ukuaji wa sekta ya kilimo hasa kwa wananchi wa hali ya chini kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuseme kweli kabisa sekta ya kilimo ambayo ndiyo inaajiri Watanzania walio wengi katika nchi yetu bado haijafanya vizuri kabisa. Namna nzuri zaidi ya kuweza kufanya vizuri ni kuhakikisha kwamba tunaweka mkazo kwenye yale mazao ya kimkakati kama mkonge, mahindi, mazao ya matunda ambayo yanazalishwa kwa wingi sana katika Mkoa wa Tanga, lakini vilevile mazao ya alizeti na korosho ikiwa hayo ndiyo mazao makubwa ya biashara katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namna ya kutekeleza haya nilidhani niishauri Serikali kwamba kwa miaka mingi sasa tumekuwa tunazungumzia namna ya kuboresha kilimo katika nchi yetu lakini yawezekana hatujaona tija kubwa siyo kwa sababu pengine bajeti inayotengwa haikidhi mipango ambayo inapangwa juu utekelezaji wa shughuli za kilimo lakini bado wananchi wetu hawajajuwa kilimo ni fursa na ni ajira ya uhakika. Namna ya kufanya kilimo kuwa ajira ya uhakika ni kutengeneza mipango mikakati ya kuidhinisha maeneo ya mapori ya yaliyojaa kwenye nchi yetu na kupanga mazao ambayo yanaweza yakalimika katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kule Handeni wakazi wengi wa Wilaya ya Lushoto kutokana na Lushoto kule ni milima mitupu wanaenda Handeni kulima mahindi lakini wanapata shida sana namna ya kupata ardhi ya kilimo pale Handeni kwa sababu siyo wenyeji pale na ukifika pale bado kuna tozo mbalimbali kwenye vijiji na Serikali za Mitaa ambayo bado inamrudisha nyuma, inamkatisha tamaa huyu mwananchi mdogo ambaye anahemea kule kwenda kufanya kilimo katika wilaya ambayo siyo ya nyumbani kwake. Pangekuwa na mkakati wa Serikali wa moja kwa moja kuwasaidia wale wote ambao wana nia ya dhati ya kufanya kilimo hata kwenye wilaya ambazo si za nyumbani kwao, wakaenda wakafanya kilimo chenye support kubwa ya Serikali kwa maana ya pembejeo na vifaa vingine vya kilimo pengine tungetoka kwenye hali ya sasa ambayo inaonyesha dhahiri kwamba bado hatujafanikiwa sana kuajiri vijana wengi kwenye kilimo kutokana na mikakati ambayo ipo sasa.

Mheshimiwa Spika, nimejaribu kufanya tathimini, ukiangalia matokeo ya kidato cha nne mwaka 2020, kuna wanafunzi zaidi ya 280,000 walipata division four na zero. Takwimu hiyo ya wanafunzi takribani laki tatu wanaotengenezwa kila mwaka na kutupwa na mfumo kuwa nje ya system nzima ya ajira rasmi baada ya miaka kumi unaweza kuwa na watu wengi sana ambao ni walalamishi kwenye nchi, hawana shughuli maalumu ya kufanya. Kama wangetengenezewa utaratibu maalumu wakawa wanawekwa kwenye sekta za ujasiliamali, sekta za kilimo na wakawa wanapewa mafunzo pengine ingewasaidia vizuri zaidi kupata ajira na kuacha kuilalamikia Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia limeuliziwa katika swali asubuhi na Mheshimiwa Hawa Chakoma Mchafu kuhusiana na vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya. Katika hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa 64 ameelezea namna gani Serikali imefanikiwa kujenga vituo vingi vya afya na zahanati katika nchi yetu ndani ya miaka mitano. Tumejengewa zahanati 1,998 lakini vituo vya afya 487. Hii ni hatua kubwa mno ambayo nchi yetu ndani ya miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini bado tuna shida kubwa katika utoaji wa huduma katika vituo hivi. Baba mtu mzima ambaye anaenda kuhemea huduma kwenye kituo cha afya kilichopo pembezoni takribani pengine kilometa 90 mpaka 100 kwenda kwenye hospitali ya wilaya anashindwa kabisa kupata huduma za msingi kama vile dawa za presha na vipimo vingine ya kawaida ambavyo viwengeweza kufanyika kwenye ngazi ya kituo cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namna pekee ya kuweza kuondoa tatizo hili ni sasa Wizara ya Afya kuamua kubadilisha mfumo wa utekelezaji wa majukumu kutoka kwenye kuyagawa kwa hospitali na baadaye wayagawe kwa kada za watumishi au madaktari ambao wanapatikana kwenye hivyo vituo. Kwa sababu wapo madaktari wazuri na wasomi kwenye vituo vya afya, kwa nini wasipewe jukumu la kuweza kumpima mtu presha na kumpatia dawa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mtu ambaye amepata shida labda ya kuvunjika mkono au mguu, tunavyoenda sasa, kama Serikali itapeleka vifaa tiba kwenye vituo vyetu kama ambavyo mwongozo wa afya unazungumza maana yake utakuwa na X-Ray mashines na vifaa vingi kwenye ngazi za vituo vya afya. Sasa akishapima hapo atakwenda wapi?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Husna.

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)