Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aliyenijalia afya njema hata siku ya leo nikawa hapa. Pia naomba niunge mkono hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma hotuba zote mbili za Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais kupitia Serikali yake ya Awamu ya Tano anapojenga SGR maana yake anafanya capital investment, anapojenga Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere anafanya capital investment; anapojenga na kuimarisha bandari zote anafanya capital investment; anavyonunua ndege anafanya capital investment. Hii tafsiri yake ni nini? Nchi hii miaka ijayo hatuna tena changamoto kwenye suala zima la ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kwa sababu Mheshimiwa Rais ameshatuwekea misingi bora ya kukua kwa uchumi wetu na Taifa letu. Kwa hiyo itoshe kusema katika hili nampongeza sana Mheshimiwa Rais na namwombea Mungu amjalie Maisha mema.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mambo makubwa sana kwenye sekta mbalimbali. Ushauri wangu ni eneo moja ambalo linahusu mgawanyo wa huduma hizi kitaifa. Tukifanya tathmini ya ujenzi wa barabara, huduma ya afya, elimu, kitaifa utaona kwamba kuna baadhi ya watu lugha hii hawaielewi. Nikisema tumejenga vituo vya afya kadhaa kitaifa, mwananchi wa Jimbo la Mlimba ambaye hana kituo cha afya haelewi lugha hii. Ukisema tumejenga lami kiwango cha urefu kadhaa, maana yake mwananchi wa Mlimba ambaye tangu azaliwe hajaona lami hawezi kuelewa lugha hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa rai yangu na ushauri wangu na kwa sababu jukumu langu kama Mbunge ni kuishauri Serikali na kwa kuwa tunakwenda kufanya maandalizi ya Mpango wa Taifa, nashauri Wizara husika, hasa Wizara ya Fedha na Wizara nyingine za kisekta, umefika wakati sasa tutazame mgawanyo na uwiano wa huduma hizi kitaifa ili lugha hii kila mwananchi Mtanzania aielewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu kama walipa kodi ni Watanzania wote. Sasa inaleta changamoto kidogo mwananchi wa Mlimba anayelipa kodi ikaenda kujenga Dar es Salaam na yeye kimsingi ni mwananchi ambaye ana haki ya kupata huduma zote mbalimbali. Kwa hiyo nishauri tunapokwenda kuandaa na ni rai yangu na naamini kupitia Mawaziri hawa mahiri kabisa, hii hoja wataichukua, kwamba tunakwenda kupanga mpango wa kitaifa sasa, tutazame mgawanyo wa huduma hizi kitaifa ili Watanzania wote wanufaike na rasilimali za nchi hii, kwa sababu Serikali yetu siyo Serikali ya majimbo, Serikali ya majimbo ndiyo inahamasisha uneven development.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijikite katika eneo lingine la pato ghafi la Taifa. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Mambo ya Nje; hakika anafanya kazi kubwa sana. Ana spidi kali sana, lakini jamani wakati sisi wengine we are lagging behind. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumzia maendeleo ya Taifa letu lazima Wizara zote tuwe na muunganiko wa pamoja, tuzungumze lugha moja, ili tuhakikishe nchi yetu inakuwa kwa maendeleo kwa kasi zaidi. Kwa mfano, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje anashughulika sana na kuimarisha mahusiano ya nchi yetu na nchi zingine, kupata wawekezaji wa kigeni. Hata hivyo, inapofika Wizara husika kuharakisha mchakato huo ili mwekezaji wa kigeni awekeze kuna masuala ya nenda rudi, njoo kesho, unajua muda pia ni mali; muda ni mali. Leo siyo kesho, siku ya leo haitapatikana tena kesho. Kwa hiyo ni rai yangu kwamba Wizara zingine zina kila sababu sasa ya kuona zinachangia kasi hii ya Wizara ya Mambo ya Nje, hasa kwenye suala zima la uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema nini hapa; ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa tisa utaona ameeleza namna ya ukuaji wa pato la Taifa kutoka trilioni 94.3 kwa mwaka 2015 hadi trilioni 139.9 mwaka 2019. Tunampongeza Mheshimiwa Rais, lakini swali langu na hoja yangu ya msingi hapa, tunapopima ukuaji wa uchumi wa nchi turudi tujikite kuona hasa kwenye suala zima la export na import. Tuone ni kwa kiwango gani tunauza bidhaa zetu nje na kiwango gani tunaagiza bidhaa ndani ya nchi. Kwa mfano, import ikiwa kubwa kuliko export matokeo yake unakuwa na unfavorable balance of payment. Hoja yangu; tuongeze uzalishaji kwenye sekta za kilimo, kwenye sekta za mifugo, kwenye sekta mbalimbali ili tuweze kukuza pato letu la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite kwenye Sekta ya Ardhi. Ardhi tuna fursa kubwa; nishauri tu, tuna kila sababu ya kupima nchi hii kwenye halmashauri zote na jambo lenyewe ni dogo sana. Watanzania wakipata hatimiliki Serikali itaongeza tax base na mwananchi wa kawaida anaweza kukopesheka benki na hii ikasaidia uchumi wa nchi yetu kukua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapokwenda kuhitimisha naomba niende moja kwa moja kwenye Sekta ya Barabara. Bado nisisitize Mkoa wa Morogoro ni mkoa wa kimkakati, ni mkoa ambao unalisha Taifa letu, hasa Jimbo la Mlimba. Barabara inayounganisha Mikoa ya Morogoro na Njombe kutoka Ifakara, kilometa 125, ni barabara ya muhimu sana kitaifa. Kwa hiyo rai yangu barabara hii ikijengwa itafungua uchumi wa nchi yetu, lakini pia wananchi wa Mlimba watanufaika na barabara hii. Kwa hiyo kwa kuwa barabara hii imeelezwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi Ibara ya 76, ombi langu, Wizara husika ya Ujenzi tunapokwenda kwenye Mpango sasa wa Taifa ni vyema kwenye bajeti yetu tukaanza ujenzi wa barabara hii ili Watanzania hawa wanufaike na barabara hiyo kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalize kwenye Sekta ya Elimu. Jana mzee wangu, Mheshimiwa Dkt. Kimei ameeleza hapa, lakini changamoto kubwa hatuwezi kuboresha elimu, hasa kwenye Sekta ya Ufundi kwa kuanzia kwenye tertiary education. Wenzetu Wachina wana kitu kinaitwa industrial culture na kupitia All Chinese Youth Federation, ukisema uanzie kwenye tertiary education kuimarisha elimu ya ujuzi au ufundi mchundo, hatuwezi; tuanze na level ya shule ya msingi. Kuanzia shule ya msingi kuwe na study maalum tuwekeze kwa watoto wadogo, anapokua anakuwa na industrial culture, anavyokua inamsaidia yeye kukuza kipaji chake. Tunapoendelea kuwekeza kwenye sekta ya elimu ya juu, sisemi haina umuhimu, lakini maana yake tunatengeneza Taifa lenye mameneja wengi kuliko wazalishaji. Matokeo yake hawa mameneja hawana wa kuwasimamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kwamba tujikite, Wizara ya Elimu mama yangu yupo hapa, naomba atusaidie. Ikiwezekana vyuo vya VETA nayo iwe elimu bure, wasilipe chochote na ujenzi wa vyuo vya VETA, vijengwe kwenye ngazi ya tarafa, hasa Jimbo langu la Mlimba, Tarafa za Mngeta na Mlimba. Naeleza haya ili kuona namna gani tunaweza kuona Taifa letu linakwenda mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina hoja moja ya mifugo. Ni kweli tumekuwa nchi ya pili kwa ufugaji, lakini Mheshimiwa Rais ameeleza kwenye hotuba yake kwamba hataki kuona wafugaji, wakulima, wanahangaika. Leo hii unaona mfugaji anayefuga mifugo anaambiwa apunguze mifugo badala ya kumpa njia mbadala kwenye mifugo yake anayofuga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo hali kadhalika; kilimo chetu bado kinahitaji kuongezeka thamani.
Kwa mfano pale Mlimba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Kengele ya pili?
MBUNGE FULANI: Endelea.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kaka yangu, Mheshimiwa Bashe nisikilize hapa kidogo…
NAIBU SPIKA: Muda wako umeshaisha Mheshimiwa.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Umeisha?
NAIBU SPIKA: Ndiyo. Ahsante sana.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kuwasilisha. (Makofi)