Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kusimama hapa. Kwanza, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia uzima wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile leo ni mara ya mwanzo kusimama katika Bunge lako hili, napenda nitoe shukrani kidogo kwa wanaostahiki. Kwanza, nawashukuru kwa dhati kabisa wananchi wa Jimbo la Konde kwa kunipa kura za kunirudisha tena hapa Bungeni. Naamini kabisa maamuzi yao yalikuwa ni sahihi na nataka kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu anijalie niwawakilishe kwa usahihi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka nitoe shukrani za dhati kwa chama changu cha ACT Wazalendo kwa kuniamini kunipa fursa na wanajimbo wakanichagua kuja hapa. Pia napenda kwa dhati kabisa kutoka ndani ya moyo wangu nimshukuru kiongozi wa chama chetu Mheshimiwa Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa Chama, Maalim Seif Shariff Hamad, niwaombee kwa Mungu awape afya njema wazidi kusimamia mpaka pale haki itakaposimama ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia, nataka niongee kwanza katika hotuba ya Mheshimiwa Rais aligusia habari ya viwanda,nataka hapa kidogo niongelee suala hili, dakika ni chache lakini tutagusa maeneo kidogo kidogo hivyo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuita wawekezaji tuanzishe viwanda ndani ya nchi ni maono yenye lengo la kuleta manufaa kwa nchi yetu na watu wetu, naunga mkono juhudi zote zinazofanywa na Serikali katika kuhimiza wawekezaji kuingia ndani ya nchi yetu. Niseme kwamba tunapoomba wawekezaji waingie ndani ya nchi yetu tunawajibu wawekezaji kuwalinda ili wafanye kazi zao ili kuleta tija tunayodhamiria kuipata. Umezuka mtindo ambao naomba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda awe makini sana, tunakuwa mahodari wa kutaka wawekezaji waingie, wanakuja na viwanda vinaanzishwa, lakini matokeo yake baada ya muda inatokea migogoro au sintofahamu inayoifanya viwanda hivyo vishindwe kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa karibuni mtakumbuka palikuwa na mgogoro mzito wa Kiwanda cha Dangote, uwekezaji ule mkubwa lakini ulikuwa utendaji wake ni wa kusuasua. Kwasababu zozote zile nashukuru nimepata taarifa kwamba sasa kiwanda kile tayari kinafanyakazi, hilo ni jambo zuri na napongeza jitihada zote zilizofanyika kupelekea kiwanda kile kurudi katika uzalishaji. Hongera sana kwa wote waliohusika kufanikisha hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo pale Tanga tuna kiwanda kikubwa sana cha kuzalisha ngano, Pembe Mills, hiki kiwanda sasa kina takriban mwaka wa nne kimesimama na ni uwekezaji mkubwa, ni miongoni mwa viwanda vichache vikubwa vya unga ambavyo vipo katika nchi yetu. Nataka Mheshimiwa Waziri afuatilie na jitihada zilizofanyika kufanya Dangote irudi kufanyakazi na watu wa Tanga wanahitaji Kiwanda cha Pembe Millskirejee katika uzalishaji ili wananchi wa Tanga wafaidike na ajira na mapato yao. Katika suala la viwanda naomba niishie hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi katika suala la katiba mpya, nilibahatika kuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba na wewe ulikuwa shahidi, Mheshimiwa Spika alikuwa ni Mwenyekiti wangu wa Kamati. Maamuzi yale yaliyofanyika ninahakika yalipata Baraka ya Chama Cha Mapinduzi kwa 100% kwasababu Chama Cha Mapinduzi na ndiyo chama tawala na ndiyo chama chenye Serikali, kama jambo lile walikuwa hawakulikubali lisingefikia kuingia kwenye Bunge la Katiba, ninahakika walikubali na walikuwa na dhati ya nafsi zao kulifanya jambo lile lifanikiwe. Kubwa zaidi tulikwenda kwa wananchi Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikwenda kwa wananchi ikazunguka nchi nzima kuchukua maoni ya Watanzania na Watanzania walijibu walichokitaka. Bahati nzuri Bunge la Katiba lilifanyakazi Watanzania waliyoitaka na bahati nzuri zaidi ni kwamba wako viongozi ambao wamepewa nishani kwa kufanikisha kazi ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunachokizungumza hapa si jambo geni wala jipya, ni jambo ambalo liko katika ahadi kwa wananchi wa Tanzania wakupatiwa katiba mpya. Kwahivyo tunapolizungumza hili katika hotuba ya Mheshimiwa Rais lipo, 2015 na kuna ahadi yake mwenyewe, kwahivyo tunapokumbushana ni kwa lengo jema la kujenga. Naomba Serikali ilete majibu Watanzania...

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib kuna taarifa.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST:Nashukuru naomba nimpe taarifa muongeaji kwamba suala la katiba mpya lipo katika hotuba ya Rais ukurasa wanane, akiahidi kwamba atahakikisha analitimiza.

NAIBU SPIKA: Ngoja ngoja tuelewane vizurikwasababu wewe tulikuwepo wote hapa, yeye kashasema ipo kwenye hotuba ya Rais, wewe unampa taarifa kwamba ipo kwenye hotuba ya Rais, ni taarifa gani unayompa maana kashasema…

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Nasaidia kumweleza.

NAIBU SPIKA: Hebu soma kanuni yako inazungumza nini kuhusutaarifa,ni taarifa gani unayoweza kutoa, siyo taarifa ambayo yeye anaijua hapana, taarifa ambayo yeye hajaisema, sasa yeye kashasema, ni taarifa gani unampa.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: kwenye floor kuna mtu alitaka kujua ipo wapi ina maana kuna mtu wa...

NAIBU SPIKA: Nani aliyekuuliza Mheshimiwa siyo wewe unayechangia? Yeye kashasema ipo, sasa wewe unasema taarifa, lazima umpe kitu ambacho yeye pengine amepitiwa ama hakifahamu. Mheshimiwa Khatib endelea na mchango wako.

MBUNGE FULANI: Hicho ni kiherehere.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kwamba imani ya Watanzania ni kwamba itakapopatikana Katiba mpya pia katika katiba mpya moja ya tunda muhimu la katiba mpya itakuwa ni Tume huru ya Uchaguzi. Ndani ya nchi hii tunaamini, ni imani yetu sisi na imani yetu hailazimishi imani yangu mimi kuikubali mtu mwingine, tunaimani na tunaamini hivyo kama katika nchi yetu ya Tanzania hatuna Tume huru ya Uchaguzi, whatever wengine tumerudi, lakini kurudi kwetu kama mnavyotuona hili benchi loote lilikuwa letu enzi zile za CUF na hili loote lilikuwa la CHADEMA, Tume ya Uchaguzi imetufanya tumekuwa maskini, tumekuwa mayatima, tumerudi kajipande hiki tu, Wabunge wa Majimbo tuko watano wanaume tuliobakia wote tuna wanawake humu jamani haki hii? (Kicheko)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatibu kuna taarifa nyingine kutoka kwa Mheshimiwa David Ernest Silinde.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Khatib wakati wa mchakato wa Katiba mpya na mimi wakati huo nilikuwa upande wa pili. Kwahiyo mimi nilikuwa sehemu ya ule mchakato na bahati nzuri sana tangu wakati tume inaundwa ilikuwa bado ni Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ndiyo ilitengeneza ile tume na tume ikakusanya maoni. Serikali ya Chama Cha Mapinduzi wakati huo niko upinzani, ilipounda tume ikaleta mchakato ule wa maoni yote ukaletwa ndani ya Bunge na mimi niko ndani ya Bunge, mchakato ukaanza tukaushiriki, sasa baada ya kuona kwamba ile ngoma ngumu, wakati huo na mimi niko upande wa pili, sisi tukaingia mitini umenielewa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwahiyo wakati ule wa mchakato siyo CCM waliokwamisha, wakati ule ni sisi tuliokimbia ndani ya Bunge na uzuri ni nini? Jambo hili Tanzania nzima inajua siyo kwamba lilikuwa la kificho, Bunge lilikuwa liko wazi, lilikuwa linarushwa, sisi ndiyo tukagoma, tukakaa kule ndani kwa mashinikizo na shinikizo kubwa lilikuwa kwamba tunataka Serikali tatu, ndiyo sababu iliyotuondoa ndani ya Bunge.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwahiyo nilikuwa nataka nimpe tu taarifa kwamba malengo ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi yataendelea kubaki kuwa sahihi, isipokuwa mwisho wa siku sisi na ilitakiwa wakati Mheshimiwa Khatib anachangia hapa ilitakiwa aseme kwa kweli sisi tulikimbia, kwahiyo tunaomba kwa kukimbia kwetu kule Mheshimiwa Rais atusamehe. Ahsante sana.(Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib unapokea taarifa hiyo?

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme hivi nimesikiliza taarifa yake, lakini nataka nimfahamishe ndugu yangu Silinde kwamba tuliokimbia ni sisi Wabunge wa CHADEMA na CUF…

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Hawakukimbia Watanzania maana yake nini?

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunti uwe na utulivu kidogo kwasababu taarifa anayoijibia ni hii aliyopewa sasa unataka kuweka taarifa juu ya taarifa utulie kidogo eee mama.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Kama kutoka kwetu sisihakukuondoa majority ya Bunge la Katiba kufikia maamuzi na ndiyo maana ninyi mliendelea kubakia, kama kutoka kwetu sisi kulikuwa na maana kwamba katiba isipatikane? Ninyi mlikaa mkasubiri kufanya nini?Na kwanini mlimalizia? Na ninyi ilikuwa mtoke kuonekana kwamba sisi tulichokataa hakina maana kwaWatanzania, lakini kutoka kwetu sisi na mlichokiamua tumeona bado kama kuna kosa tulilifanya lakini kulikuwa na maana kwa Watanzania. Kwa hiyo ina maana kwa Watanzania madai yao, hayakufa kwasababu ya kutoka sisi. Mheshimiwa Silinde usijisahau leo kwa kuwa uko kwenye kiti kikubwa zaidi, kwasababu una V8, ndugu yangu ni mapito tu hata sisi V8 tutapanda. (Kicheko).

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee nataka nizungumzie habari ya mikopo ya elimu ya juu. Kimekuwa ni kilio cha wanufaika wa mikopo hii na hili ndugu zangu wana CCM wanabunge la kijani, naomba sana tuangalie athari ya makato yaliyoongezwa ya wanufaika wa mikopo, yanawaumiza. Inaanza kujengeka dhana sasa kuona kwamba utajiri ni muhimu kuliko elimu tuondokane na hilo, yaani inaanza kujengeka dhana matajiri wengi siyo wasomi…

NAIBU SPIKA: Endelea Mheshimiwa Khatib.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Kwamba matajiri wengi siyo wasomi umuhimu wa elimu utabaki kuwa muhimu kuliko chochote katika maisha ya mwanadamu, lazima tukubaliane hilo. Kwahiyo tuangalie namna ambavyo wamepandishiwa marejesho yale ya 15% na Serikali badala ya 8% ikiwezekana naunga mkono Mbunge mmoja wa CCM aliotoa hoja jana kwamba ikiwezekana ishushwe mpaka 5% kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu naomba sana hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nataka nizungumzie habari ya utawala bora. Kuna watu wenye mamlaka vyombo vyetu Jeshi la Polisi limekuwa likifanya mambo ambayo siyo utawala bora, juzi iko taarifa inasambaa kwenye vyombo vya habari askari polisi kule Mbeya wamemshusha raia driver kwenye gari na wakamuua, matendo yaliyokuwa yalifanyika Afrika Kusini enzi za Makaburu, ndiyo matukio ambayo vyombo vyetu vya ulinzi baada ya kusimamia usalama wa raia, sasa vinajenga uhasama wa raia. Naomba Serikali itoe tamko kali na zito kuhusiana na kadhia ya raia Yule,driverYule, aliyetolewa kwenye gari, akapigwa akauliwa na askari wa Jeshi la Polisi. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)