Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda wa kuchangia moja kwa moja ni mfupi ninachangia baadhi ya mambo kwa maandishi. Ninaunga mkono hoja. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake, pia ninampa pole Naibu Waziri Mheshimiwa Stella Manyanya kwa kufiwa na mama, Mungu amrehemu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya elimu ndiyo itafafanua mustakabali wa Taifa letu. Kwa hiyo, wote tu wadau. Ninaunga mkono hoja lakini ninatoa maoni na ushauri ambao Waziri akiufanyia kazi itasaidia sana. Nitajielekeza katika maeneo yafuatayo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waraka Na. 6 wa 2015 kuhusu elimu una mapungufu. Wakati ninaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais kwamba elimu ya msingi na sekondari ni bure, kwa maana italipiwa na Serikali ili kumpunguzia mzazi mzigo, ninashauri waraka huo uboreshwe. Ni wajibu wa jamii katika kuchangia elimu ili iwe bure huku miundombinu ikijengwa iweze kutekelezeka.
Hali ilivyo sasa inaonekana wajibu wa kuendeleza miundombinu umebaki tu kwa Serikali jambo ambalo ni mzigo mkubwa. Ushauri wangu ni kwamba wajibu wa kuchanga fedha za miundombinu elimu katika Kata uwe wa lazima katika jamii ili tusirudi nyuma. Momentum ya kuendeleza shule za Kata nazo ziwe na viwango. Duniani kote elimu huchangiwa na jamii, wazazi pekee hawawezi, Serikali pekee nayo ni vigumu kwa nchi kama yetu pamoja na nia nzuri sana ya Rais wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumuunge mkono kwa kuhamasisha jamii ijenge madarasa, hosteli, maabara, ofisi, vyoo na kadhalika. Aidha, jamii ichangie madeski na mahitaji mengine ya kufundishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya walimu wa sekondari katika Wilaya ya Muleba yanaonesha upungufu wa walimu wa sayansi wakati wa sanaa wametosha na kuzidi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba Wizara itafute misaada ya walimu wote nje ya nchi ili shule ziwe na walimu. Mwaka 1960 Baba wa Taifa alitafuta msaada kutoka kwa Rais wa Marekani John Fitzgerald Kennedy walioitwa Peace Corps wakafundisha. Hatuwezi kuacha hii hali ambapo mwanafunzi anamaliza shule sekondari bila kumuona mwalimu wa hesabu. Naomba Mheshimiwa Waziri anisaidie katika jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapendekeza pia walimu wa ziada waondolewe katika shule za sekondari na pia kupelekwa shule za msingi ambazo bado hazina walimu wa kutosha. Aidha, katika manpower planning mahitaji ya walimu wa hesabu na sayansi zipewe kipaumbele. Walimu wanaweza kupewa retrovining program na kufundisha masomo yasiyo na walimu. Pia, unaweza ukaweka mobile teaching teams‟ za vipindi vya sayansi, walimu wachache waliopo wanatoka shule moja hadi nyingine. Pia kwa kuwa umeme na simu umesambaa uwezekano wa kutumia distant learning kutumia mtandao uangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili litasaidia pia kuboresha viwango. Kwa vyovyote vile walimu wasiohitajika shuleni waondolewe. Muleba imekuwa na tatizo la baadhi ya walimu wa Kiswahili na Historia wasio na vipindi wanabaki kwenye majungu na kuvuruga utulivu na nidhamu shuleni. Hii imetokea shule ya sekondari Bureza ambapo baadhi ya walimu wasio na vipindi vya kutosha walivuruga nidhamu, jambo la kusikitisha baada ya ukaguzi kuliona hili na kupendekeza wahamishwe ni Mwalimu Mkuu aliyehamishwa katika mazingira yanayotakiwa kuchunguzwa. District Education Officer aeleze kwa nini ana muadhibu Mwalimu Mkuu anayefanya vizuri katika Wilaya nzima ili kuwafurahisha walimu wasio na nidhamu. Mheshimiwa Waziri afike Muleba aangalie hali duni ambayo tunayo hairidhishi na haitaleta tija wala matokeo mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya kuanza shule kwa hali tuliyonayo vijijini chekechea ianze na miaka 5 hadi 6 na shule ya msingi miaka 7 hadi 8 la sivyo, watoto wanakuwa wengi sana darasani na ukizingatia udogo wa watoto na uchache wa walimu, service ratios hazikubali inakuwa na shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ada elekezi katika shule binafsi, mjadala huu ni wa kushangaza, Wizara ya Elimu ina kazi nyingi na mimi sielewi kwa nini hili litusumbue. Wazazi wapewe elimu ya kutosha kuhusu ubora au mapungufu ya shule binafsi wanapopeleka watoto wao ili wapate value for money. Lakini kuchukulia shule binafsi kwamba ni biashara ni kushindwa kutambua elimu bora ilivyo huduma. Mimi sina mgongano wa maslahi lakini mdau katika sekta ya elimu. Niko katika taasisi ya Barbo Johnson Girls Education Trust- JOHA Trust inayomiliki shule mbili za sekondari; moja Dar es Salaam nyingine Bukoba. Shule hizi siyo biashara kama wengi wanavyodhani; shule hizi ni huduma kuwapa wasichana elimu bora. Shule ina utaratibu wa kutoa ufadhili kwa wasichana wenye vipaji lakini ambao hawana uwezo kulipa ada. Katika shule za JOHA trust ada inatofautiana kati ya wanafunzi kulingana na uwezo wao kiuchumi inaitwa assessed fees. Kuna wanafunzi wanapewa ufadhili wote na kuna wanalipa kinachoitwa fees zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hawa wanapewa ruzuku ya karibu milioni moja kwa sababu gharama halisi ni shilingi milioni 5.5 na full fees ni shilingi 4.5 milioni kwa sasa. Mheshimiwa Waziri awasikilize watoa elimu na kuwasaidia. Ni aibu kwa TRA kushinda kwenye shule kudai kodi badala ya utaratibu mzuri zaidi kwa kodi za lazima kukusanywa.
Hali ya sasa hivi imelalamikiwa sana na siyo rafiki kwa watu wanaosaidia kuelimisha Taifa letu. Kama kuna shule binafsi ambazo hazina viwango wazazi watazigundua. Kazi ya Wizara ni kutoa taarifa za ufaulu wa wanafunzi na hapa NECTA imefanya kazi nzuri ila ninashauri NECTA iwe inatangaza top 100 schools siyo top 10 maana shule zimekuwa nyingi, kwa hiyo top 10 ni kasumba ya mazoea. Tujue shule bora 100 kwa ujumla na katika vipindi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitabu viwe vinafanana. Mwisho ninashauri kuwa elimu pia inasimiko utamaduni, sasa kama vitabu viko tofauti tutajengaje utamaduni wa Taifa, culture harmony. Ninashauri utunzi wa vitabu ubaki kama ulivyo lakini Wizara iratibu na kuchagua vitabu vinavyofanya wanafunzi, kizazi au rika wawe na common reference point kupitia vitabu wavyosoma.
Mheshimiwa Spika naunga mkono hoja.