Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Najma Murtaza Giga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii na mimi nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote ambayo ametujaalia lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuchaguliwa tena kwa kura nyingi kama ambavyo wametangulia kusema wenzangu na wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika pamoja na Wabunge wote ambao tumebarikiwa kurudi tena kwa awamu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi pia nimshukuru kiongozi wangu wa Umoja wa Wazazi na timu yake yote pamoja na Chama Cha Mapinduzi kwa kuniamini kwa mara nyingine tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Rais imejimwaga katika maeneo mengi ambayo ndiyo mwelekeo na dira ya miaka mitayo iliyopo. Pia mwisho wa hotuba yake aliwaelekeza Mawaziri ambao atawateua ambao tayari wako mbele yangu hapa kwamba warudi wakaisome Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa maeneo ambayo yeye hakuweza kuyafafanua kwa siku ile. Kwa hiyo na mimi nitaenda moja kwa moja katika eneo ambalo hakulifafanua siku hiyo ambalo liko kwenye ukurasa wa 144 hadi 145 ambayo inahusu ustawi wa jamii kwenye suala zima la ustawi wa Watoto na familia.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu bado ina changamoto katika suala hili, lakini nitumie fursa hii kushukuru sana wote waliopanga timu hii ya Ilani iliyotengeneza kwa kuweza kufafanua vifungu ambavyo sasa vitatuelekeza tunaondokana vipi na mporomoko wa maadili unaosababisha kuondoa furaha na amani ya watoto wetu, ndoa zetu ndani ya nyumba zetu na mambo yote yawe yameelekezwa hapo kuanzia kifungu (a) mpaka (n) vya Ilani katika ukurasa huo wa 144 na 145.

Kwa hiyo, nitaomba sana waheshimiwa Mawaziri kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliomba kwamba mfanye kazi hiyo kupitia ilani mimi nitakuwa na ninyi sambamba katika miaka mitano hii kuhakikisha kwamba vile vifungu vyote ambavyo vimeelekezwa kwenye ilani tunavishughulikia ipasavyo. Kama ni kutunga sheria, kama ni kurekebisha sheria, kama ni kutoa elimu kwa jamii basi nitawahamasisha na Wabunge wenzangu tuhakikishe tunakwenda Tanzania nzima kuhakikisha kwamba suala la mporomoko wa maadili ambao unasababisha matatizo mengi mojawapo likiwa ni mimba za utotoni tunalitokomeza Tanzania. Lakini pia, suala la talaka za hovyo nchi yetu imezidi jamani Waheshimiwa Wabunge! Tunashindwa kudumisha ndoa zetu na badala yake tunasababisha kutelekezwa kwa familia zetu na watoto wetu ambao mwisho wa siku ndiyo wanaenda kupata mimba za utotoni. Kwa hiyo, hilo ni janga ambalo kama hatukuliendea vizuri na tukalitilia mkazo basi haya maendeleo ambayo tuanzungumzia huko baadae tutakuja kukosa maendeleo mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sio hilo tu, kuna suala zima la kuwarudisha nyuma watoto wa kike katika kutafuta elimu. Bado ni changamoto katika nchi yetu. Kwa hiyo nitashirikiana na Wabunge wenzangu, lakini pia kuna suala zima la udhalilishaji wa watoto wadogo. Hili jamani mara hii litakuja kwa mwendo mpya. Ninaomba Mheshimiwa Dorothy Gwajima ajiandae kwa hilo. Mimi sitakubali kwa sababu tunashindwa kabisa ni nini tufanye jinsi ambavyo watoto wetu wanaharibiwa katika nchi yetu hii. Hilo ni jambo la kusikitisha, tumelizungumza miaka mingi, lakini safari hii naomba kutokana na haya yaliyoandikwa kwenye Ilani yetu kwenye vifungu hivi 14 nina hakika kabisa kama tutavisimamia ipasavyo na tutaisimamia ipasavyo Serikali katika vifungu hivi vilivyoainishwa kwenye Ilani kumlinda mtoto katika nchi yetu naamini kabisa miaka mitano hii tutafika mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa na hayo tu. Naipongeza kabisa hotuba ya Mheshimiwa Rais na naomba tushirikiane kuitekeleza ambavyo ameelekeza. Ahsante sana. (Makofi)