Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa nafasi hii hapa leo. Pia nimshukuru Rais wetu kwa ushindi wa kishindo, Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii ya leo kuchangia hotuba ya Mhesimiwa Rais, nimepata nafasi ya kuisoma, hotuba ni nzuri sana na inakwenda kuakisi sifa kuu za kiongozi, kiongozi sharti awe mcha Mungu, awe na maono na awe na utekelezaji wa haya ninayoyapanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiisoma hotuba hii nitaangalia maneno machache, mfano ukurasa wa 26 unazungumzia viwanda, naomba nifungamanishe viwanda pamoja na miundombinu. Rais wetu ametupa sifa kuu tatu ya aina ya viwanda wanavyovitaka; moja, viwe ni viwanda ambavyo malighafi zake zinapatikana nchini; pili, viwe ni viwanda ambavyo vinatumika bidhaa zake na Watanzania walio wengi; lakini tatu, viwe ni viwanda ambavyo vinatoa ajira na alisema ikiwezekana asilimia 40 za ajira zote nchini zitokane na viwanda hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama kweli tukiamua kujenga viwanda, kazi ambayo najua Mawaziri wetu mnaifanya vizuri sana lazima tuangalie maeneo ya kimkakati. Naomba nitazame kipekee eneo kama la kwetu pale Mufindi Kusini kuna viwanda zaidi ya tisa, kikiwemo kiwanda kikubwa cha Mgololo, barabara zake mpaka sasa hivi bado sio za lami, magari yanapita maelfu kwa kila siku na kodi tunalipa zaidi ya shilingi bilioni 40.
Mheshimiwa Spika, nadhani kama tunataka tukuze sekta hii tunapotazama maeneo ya barabara na mikoa, barabara za wilaya za nchi, lakini maeneo kama haya ambako ndiko kuna wale ng’ombe wetu ambao kimsingi wanatoa maziwa mengi, tutaweza kusaidia nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nipongeze pia kwa kazi kubwa ambayo imefanywa kwenye nishati, sote ni mashahidi vijiji vilikuwepo 2,108 vyenye umeme wakati huo leo vijiji 9,184 tulikuwa tunazalisha megawati 1308 leo tunazungumza megawati 1601. Tuna mradi mkubwa wa Stigler’s Gorge ambao unakwenda kutuzalishia karibia megawati 2115 hii ni kazi kubwa sana ambayo amefanya Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu maeneo yaliyobaki sasa ni vema Wizara ikaweka mkakati kwa kuzingatia maeneo matatu; moja, baada ya kukamilisha vijiji vilivyobakia vile sasa twende kwenye maeneo ya taasisi iwe ni mkakati kwamba kila shule, kila zahanati, kila ofisi ya kijiji ikawe na umeme, vitongoji vilivyobakia pia vikapate umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda ni mdogo nigusie kidogo eneo la maji, maji ni uhai, tumeona na tumeshuhudia kipindi hicho ambacho kimsingi miaka mitano. Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli amewaza kumuvuzisha nchi kutoka kwenye asilimia 41 maji vijiji mpaka asilimia 70 sasa. (Makofi)
Ombi langu sasa tuongeze bajeti ikiwemo maeneo yetu ya Jimbo letu la Mufindi Kusini, ambapo kulikuwa na miradi kama ya Himayi, ilikuwa ni miradi mikubwa ili angalau tukapate maji kwa wingi zaidi. Sekta hii iongezewe maji kwa sababu kama ni wataalam inayo wazuri, Waziri wa Maji ni mzuri, mchapakazi, anakesha kwenye site, na tukitatua tatizo la maji Watanzania walio wengi zaidi watakuwa wameanza kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ningependa kuzungumzia ajira. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuliona hilo, ametueleza kwamba atakwenda kuunganisha mifuko 18 ya vijana na ndiyo ilikuwa kazi ya kwanza aliyomkabidhi Waziri wetu Mkuu akaifanye, pamoja na jambo hilo lakini naomba tukatazame kwenye mitaala yetu. Je, mitaala tuliyonayo ina reflct mahitaji halisi huko mtaani? Hatusemi kwamba kusoma zinjanthropus na sokwe sio jambo baya, lakini kama vijana wanakwenda kujiajiri kwenye kilimo, pengine kwenye ujasiriamali, kwenye biashara, hayo ndiyo masomo ya lazima kwa sababu walio wengi wanakwenda huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tutazame pia kwenye sekta ya utalii sote ni mashahidi nchi yetu hii mwaka 2015 watalii waliokuwa wanakuja nchini ni milioni 1.2 leo wako milioni 1.5 mkakati ni kupata watalii milioni tano ikifika mwaka 2025.
Tumetoka kwenye kupata dola za kigeni karibu bilioni 2.6 leo tunakaribia bilioni sita, lazima tunapofikiria kupata watalii milioni tano tutazame maeneo mengine kwa sababu leo karibu asilimia 80 ya watalii upande wa Kaskazini, hapa tuna Mbuga yetu ya Ruaha...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)