Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais iliyotolewa mwezi Novemba, 2020 na mimi nikiwa kama Mbunge, nimesimama hapa kwenye Bunge hili tukufu kwa mara yangu ya kwanza, nianze kumshukuru kwanza Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyetufikisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakishukuru Chama changu cha Mapinduzi ambacho kilinipigania mpaka nimeweza kuingia kwenye chombo hiki muhimu sana. Tatu, nawashukuru familia yangu, walikuwa nami bega kwa bega kupambana katika kuhakikisha mimi nasimama imara kwa maslahi ya Wanaigalula wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo aliitoa ni dira ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano. Nisiende mbali, kwanza naiunga mkono kwa asilimia mia moja kwa sababu sisi wote wana-CCM tulisimama kote kule tukiinadi Ilani ya Chama cha Mapinduzi na hotuba yake yote imepitia ilani, ndiyo maana akaja na mpangokazi wa miaka mitano, nini Serikali ifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa wasaidizi wake, wameanza kazi vizuri. Tangu ametangaza Baraza la Mawaziri, tumeanza kupishana huko majimboni, wanafanya kazi nzuri sana, tuendelee na mwendo huu huu. Mheshimiwa Rais ameaminika na wananchi wote na Watanzania wote wamemwamini, ndiyo maana wakampa kura zaidi ya asilimia 84, na sisi Wabunge tumeaminiwa na wananchi, wana imani kwa kipindi cha miaka mitano wataona mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichangie sehemu chake, kutokana na muda, sisi tunaotoka majimbo ya vijijini, katika Halmashauri yetu ya Wilaya yetu ya Uyui, changamoto kubwa ni barabara, ndiyo kero ya Waheshimiwa Wabunge wote walioko humu ndani, kila utakapoenda, shida ni barabara. Katika mtandao huu wa barabara, kuna baadhi tukiwaachia TARURA hawawezi kutekeleza kwa kipindi cha miaka mitano. Kuna barabara gharama yake na bajeti inayokuja kwenye Halmashauri ya TARURA, ukiipa kwa kipindi cha miaka mitano ika-deal na barabara moja, haiwezi kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kuna barabara yenye urefu wa kilometa 89 ya kutoka Miswaki – Roya kwenda Maguliati mpaka Iyumbu, Mkoa wa Singida. Barabara hii ina madaraja 16 madogo madogo na daraja moja kubwa lenye mita 120. Hii barabara kwa takwimu ya mkandarasi ni zaidi ya shilingi bilioni sita. Halmashauri yetu inapokea shilingi bilioni 1.3 kwa mwaka. Kwa hiyo, ukisema uelekeze nguvu kule, haiwezi ikakidhi kwa kipindi cha miaka sita, barabara nyingi zote zitakuwa zimesimama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine kupiga kelele TARURA iongezewe bajeti ili tuweze kukwamua kero za wananchi wetu, wapate barabara. Kwa sababu na kule kuna wapiga kura, tena wanajitokezaga sana kipindi cha kupiga kura. Naomba sana Serikali itusaidie kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye suala lingine. Sisi Wanasiasa na viongozi mbalimbali tumekuwa tukipita kwenye majimbo tukiwahimiza wananchi wetu wachangie baadhi ya maendeleo, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, muda!

SPIKA: Eeeh! (Kicheko)

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hotuba ya Mheshimiwa Rais, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)