Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hii hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa tarehe 13 Novemba, 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijasema lolote na mimi kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru Mungu sana kwa kunipa nafasi hii. Pili, nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kunipitisha mimi kuwa mgombea na kunisaidia kushinda kwa kura nyingi sana. Pia nisiache kuwashukuru sana sehemu kubwa ya familia yangu, mke wangu na wanangu kunivumilia katika kipindi cha uchaguzi ambacho kilikuwa kigumu sana. Kwa sababu ya muda niendelee moja kwa moja na nijielekeze katika maeneo machache. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na vipaumbele kadhaa karibu vitano lakini kimoja cha kuimarisha utawala bora wa kusimamia nidhamu kwenye utumishi wa umma, rushwa na wizi niseme machache hapo. Ni kweli Mheshimiwa Rais amefanya makubwa katika kipindi chake cha Awamu ya Kwanza ya miaka mitano. Tumeona wametumbuliwa watu wengi, tumeona watumishi wazembe ambao wamewajibishwa, taarifa inatuambia takriban watu au watumishi 32,555 walichukuliwa hatua mbalimbali. Pamoja na haya, Mheshimiwa Rais katika ukurasa wa tisa nikinukuu amesema ataboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi wote ili yaendane na hali halisi ya maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli katika kipindi cha miaka mitano, watumishi wa umma hawajakaa katika hali nzuri, ukweli hawajaona mishahara lakini hii yote ilikuwa inatokana na jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais alikuwa ana kazi kubwa ya kuona jinsi gani uchumi na hali ya Kitanzania katika mapato inapanda. Tuemona uchumi umepanda takribani kwa asilimia saba kila mwaka. Tumeona Pato la Taifa limepanda kutoka trilioni 94 hadi 139. Tumeona ameweza kudhibiti mfumuko wa bei. Sasa kwa yote haya ninaona kabisa hili ambalo Mheshimiwa Rais anataka kwenda kulitekeleza katika kipindi kijacho kinaenda kuwa bora kwa watumishi wote.
Mheshimiwa Spika, niseme pia juu ya hili la kukuza uchumi na kupunguza umaskini. Pamoja na mambo mengine lakini liko jambo hili asilimia 10 kutoka mapato ghafi ya Manispaa zetu. Wengi wamesema katika eneo hili, lakini mimi ninaliona pamoja wametamkwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa asilimia 4:4:2; lakini naona kundi la vijana kuanzia miaka 35 na wazee wamesahaulika kabisa. Hao ni kuanzia umri kama wa kwangu na kuendelea. Akinamama kuanzia umri wa ujana hadi wanazeeka wanawezeshwa katika asilimia hizi 10. Inajionesha wazi katika sura za usoni wazee au vijana wanaokuja kuwa wazee watakuja kukosa nguvu za kiuchumi na hali mbaya itakuja kwa wakati huo. Hilo niliona likae hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia niseme juu ya fedha hizi zinazotolewa hasa katika kundi la vijana. Sasa tunawapa asilimia nne zao lakini hatuwaoni wanaenda kufanya biashara maeneo gani. Wale vijana wanaowawakilisha wamesema vizuri, lakini mimi nataka kusema katika Mkoa wa Dar es Salaam, Wilaya ya Ubungo hususan katika majimbo haya mawili tumeona upanuzi wa barabara wa njia nane kutoka Kimara mpaka Mlandizi takribani shilingi bilioni 140, Mheshimiwa Magufuli amezielekeza katika ujenzi wa barabara ile na tunatambua hizi fedha ni za ndani. Ni kweli upanuzi huu umetupa taabu sana kwa ajili ya vijana wengi na wafanyabiashara machinga pembeni mwa barabara, leo wanalia sana kuanzia Kimara, Temboni, Stopover, Mbezi yote hata pale Kibamba CCM.
Mheshimiwa Spika, niombe sasa Mheshimiwa Waziri alieleza vizuri. Wakati tunajenga vile vituo vya daladala, vituo vya mabasi basi tutumie sehemu fulani tuanze kuwapunguza hawa wajasiriamali wakiwa wamepata mabanda mazuri kama lile banda pale Mvomero ambalo Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo wakajengewa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nijielekeze kwenye eneo moja la elimu kwa haraka. Wengi wamesema lakini hasa nipongeze sana, lile la King’ong’o ni la kwanza, lakini sasa tayari taarifa inasema yatafanyika mazuri lakini zaidi kutokana na muda niache tu nitajielekeza katika mpango unaokuja niseme vyema juu ya maji na miundombinu yote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho nitumie nafasi hii kukushukuru na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana. (Makofi)