Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Ni Jimbo la Singida Kaskazini.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote na mimi nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pili niwashukuru wananchi wangu wa SIngida Kaskazini kwa kuniamini na kunipa fursa ya kuja kuwakilisha sauti zao katika Bunge letu hili tukufu. Nikishukuru pia Chama changu cha Mapinduzi kwa imani yake kwangu na mimi naahidi kama nilivyowaahidi kwamba sitawaangusha, nitawatumikia kwa unyenyekevu mkubwa na kwa uaminifu wa kutosha kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukifuatilia mjadala, Wabunge wengi wanazungumzia jambo la TARURA, barabara, afya, maji na kilimo. Haya mambo ndiyo yanayogusa maisha ya Mtanzania. Naomba sana tuzingatie hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo na yenyewe ilijikita kwenye haya haya na mimi siiiti hotuba, naiita yale yalikuwa ni maelekezo. Tuichukue hotuba ile tuitazame neno kwa neno, tuchukue hayo maelekezo itoshe tu kusema Mheshimiwa Rais alitupa maelekezo sisi Wabunge pamoja na Mawaziri na alisema hebu msiogope. Amesema fanyeni maamuzi chukueni hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi mchango wangu naomba ujielekeze zaidi kwenye kushauri kwa sababu mengi yamesemwa, suala la TARURA ni msiba, ukienda vijijini hakuna barabara ni mapalio. Sasa sisi tumechoka kupita kwenye mapalio. Wabunge hapa wanazungumza maisha halisi yaliyoko kule kwenye field. Tumechoka kupita kwenye mapalio, ninashauri kama hii TARURA haipewi fedha ifutwe! Kwa sababu hizo ni kodi za Watanzania, majengo wanayojenga kila Wilaya nchi hii hata lile jengo lao pale Wizarani hizo ni kodi za Watanzania. Hizo fedha badala ya kutumiwa kwenye mafuta, jengo na kwenye viti na mishahara, hizo fedha zichukuliwe zipelekwe zikatengeneze barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze kwa uchache kwenye jimbo langu tu kwenye hili eneo la TARURA kilometa 800 za barabara wanapewa shilingi milioni 600, utatengeneza nini hapo? Si vichekesho hivi? Naomba hili jambo lichukuliwe, Serikali iliangalie tuanche kurudia rudia mambo sio kila siku tunazungumza jambo hili. Kurudia rudia ina maana hawa Wabunge hawaaminiki wanapolalamika suala la barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ningependa pia nizungumzie eneo la viwanda. Mheshimiwa Rais dhamira yake ilikuwa ni kuhakikisha tunakuwa na uchumi wa viwanda na uchumi wa viwanda hatuwezi kuuona endapo sekta ya viwanda haijawa connected na sekta za uzalishaji. Itakuwa ni ndoto! Tuhakikishe tunaelekeza nguvu zetu zote kwenye eneo la uzalishaji. Tuangalie kwenye kilimo, tuangalie kwenye uvuvi, tuangalie kwenye ufugaji, huko ndiko tunakuta Watanzania wengi na ndio wanaozalisha na hao ndio wanaoweza kutuletea raw materials zinazohitajika kwenye viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa sisi leo natoleo mfano tu mdogo kwenye eneo la mifugo, ngozi inaoza na mimi ambaye ni mfugaji mtoto wa mkulima tunahitaji tuone yale mazao kule vijijini yanakuwa processed, yawaajiri Watanzania. Tunalalamika suala la ajira, tunamuajiri wapi Mtanzania kama hatujajikita kwenye eneo la viwanda? (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Ighondo.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, lakini naomba haya machache niliyoyazungumza nione yakitekelezwa. (Makofi)