Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igunga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na nchi, kwa kupata fursa ya kuwa sehemu ya Bunge la Kumi na Mbili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pili nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kunipa ridhaa ya kuwa mpeperusha bendera wa Jimbo la Igunga na hatimaye nikaibuka na ushindi na kuwa Mbunge wa Igunga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatu, kwa umuhimu mkubwa niwashukuru sana baadhi ya viongozi ambao kwa wakati mmoja mlipita maeneo mbalimbali mkitunadi na mkituombea kura, naamini ushindi wetu umechangiwa na uwepo wenu katika maeneo yetu na hapa nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowataja majina kwa uchache; kwanza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais, mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wetu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, wewe mwenyewe binafsi Mheshimiwa Spika, Job Ndugai, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dkt. Bashiru Ally Kakulwa, Wajumbe wote wa Kamati na Sekretarieti ya Chama Cha Mapinduzi, akiwepo Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Humphrey Polepole tunawashukuru kwa kuja kwenye maeneo yetu kutupigia kura. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kwa umuhimu mkubwa niwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Igunga ambao walifanya nipate ushindi wa kishindo na hatimaye leo nimeweza kuingia kwenye Bunge hili, ahadi yangu kwao nitawatumikia kwa moyo mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuwa nina muda mchache kwanza nijikite katika hotuba ya Mheshimiwa Rais, maeneo ambayo ningependa kuchangia jioni hii ni upande wa huduma za kijamii na miundombinu ya kiuchumi. Kwenye huduma za kijamii, Mheshimiwa tunaanza na suala la elimu, katika upande wa elimu Mheshimiwa amesema tutaendelea kutoa elimu bure ya bila malipo, lakini pia na kuboresha miundombinu ya kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, niwashauri Wizara ya Elimu ambao wanamsaidia Rais na Wizara ya TAMISEMI, waje na mipango madhubuti watakayohakikisha tunapata miundombinu ya uhakika na siyo inapofikia mwezi wa kumi na mbili na mwezi wa kumi na moja tunaanza kusumbuana kuhusu madawati, madarasa na upungufu wa vifaa vya kufundishia mashuleni, naamini kwenye mpango utakaokuja watakuja hatua madhubuti kwa ajili ya kuliona hili.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kwenye suala la maji, nashukuru sisi Mkoa wa Tabora tumepata Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria, changamoto kubwa imebaki kwenye usambazaji na hususani kwenye suala la viwango vya bei, naomba Wizara ya Maji waliangalie hili waje na viwango vipya ambavyo vitaweza kuwasaidia wananchi wengi wa maisha ya chini na hili napenda kutolea mfano kwa mfano kwenye suala la umeme, umeme walikuja na ile programu ya REA wanatoa umeme kwa 27,000 vijijini kwa hiyo na Wizara ya Maji tunawashauri waje na programu itakayowezesha
wananchi wengi kuunganishiwa maji ili waweze kutatua tatizo la ukame kwenye majibo yetu.
Mheshimiwa Spika, jambo la nne ni upande wa afya katika upande wa afya pia kuna changamoto kubwa upatikanaji wa madawa na vifaatiba, lakini pia kuna upungufu wa wahuguzi wa madaktari tunaomba pia Wizara ya Afya na TAMISEMI ambao mnasimamia hutowaji wa hizi huduma na sera muweze kuziangalia pia tuweze kutatua changamoto kubwa hili.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulichangia jioni hii ni suala la kilimo kwenye kilimo sisi ukanda wetu sisi tunalima sana pamba, changamoto ambayo tumekuwa tukikabiliana ni suala la wakulima kuchelewa kulipwa na ninaishukuru mwisho wa mwaka tulipokuwa tunaelekea kwenye uchaguzi kulikuwa kuna madeni, lakini Serikali waliweza kukamilisha hayo.
Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Bashe, Mbunge na jirani yangu alinisaidia sana ilikuwa ni changamoto sana wakati wa uchaguzi lakini tuliwasiliana naye akatowa maelekezo bodi ya pamba wakatulipa. Tunaomba safari hii msimu wa pamba utakapofika kipindi cha mauzo Wizara ijipange vizuri tuhakikishe wakulima hawatoki na madeni.
Mheshimiwa Spika, lakini changamoto nyingine kwenye kilimo ni suala la stakabadhi ghalani na AMCOS tungeomba pia hili suala hususani wakulima wa choroko linawasumbua sana tunaomba wizara ijipange mapema itakapofika kipindi cha kuuza mkulima anakwenda kuuza kilo mbili kilo tatu kilo tano haitaji kusubiri mwezi moja miezi miwili aweze kupata malipo yake ili itatusaidia sana kuwasaidia wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, mwisho nashukuru sana ahsante sana kwa kupata fursa hii naunga mkono hoja asilimia mia moja nashukuru. (Makofi)