Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi jioni ya leo kuchangia hotuba ya Rais. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kuiona siku leo. Pia napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwepo hapa leo katika Bunge la Kumi na Mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kukishukuru Chama cha Mapinduzi kwa kunikubali na kunipokea na kuwa mwanacha wa Chama cha Mapinduzi kwani awali nilikuwa upande ule wa pili. Hivyo, nikishukuru sana Chama cha Mapinduzi kwa mapenzi yake mema kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, napenda kuwashukuru kwa dhati kabisa wananchi wa Jimbo la Ulyankulu ambao walikuwa na imani na mimi wakiamini kabisa ni mwakilishi wao mzuri. Naamini nina deni kubwa kwao na nitahakikisha nawatendea kulingana na uwezo wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nianze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais kama ifuatavyo. Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake amesisitiza jambo kubwa sana kuhusu amani lakini hii amani kwa baadhi ya wananchi wa Jimbo langu hususan kata zile tatu ambazo zilikuwa zikikaliwa na wakimbizi amani inaweza ikatoweka endapo hatua stahiki hazitachukuliwa dhidi yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa mwaka 2015 wakiwa wakimbizi walipewa uraia wa Tanzania lakini bado wanakuwa treated kama wakimbizi. Hakuna jambo lolote la maana linalofanyika kule, shughuli za kimaendeleo hazifanyika lakini bado wanachangia shughuli kubwa za ulipaji wa kodi, wanateseka kwa kiasi kikubwa. Niiombe sasa Serikali kupitia Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Mambo ya Ndani na Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria waweze kuiangalia hii Sheria Na.9 ya Wakimbizi ambayo inawabana sana hawa watu ili waweze kufanya shughuli zao kwa amani na waishi kama wananchi wengine wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa jimbo hili hawawezi kufanya shughuli zozote, hivi sasa hata kujenga nyumba pale hawajengi, hata choo kikidondoka pale ni lazima wapate kibali kutoka kwa mkuu wa makazi ndiyo waweze kujenga. Tunaiona Serikali inafanya jitahada sana kuhakikisha inapeleka maendeleo pale lakini bado sheria ile inazidi kukwamisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetupelekea shilingi milioni 600 kwa ajili ya kujenga nyumba kwenye Chuo cha Ufundi VETA, lakini sheria ile imebana zimekataliwa kujengwa. Pia shughuli za maendeleo kama kujenga madarasa na miundombinu mingine zimekataliwa. Hivyo nawaomba Mawaziri wanaohusika na suala hili mtupe mwongozo leo ili hao wananchi wetu wapate nafuu na wajue hatima yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwenye nishati ya umeme. REA huko vijijini kwetu imekuwa ni mkombozi mkubwa, sasa hivi vijiji vingi umeme unawaka lakini kuwaka kwa umeme huko bado kuna changamoto. Umeme huu umepita kwenye vijiji tu haujaenda kwenye vitongoji. Hivi navyoongea baadhi ya kata zangu kama mbili Silambo na Kata ya Uyowa hazijapata umeme kabisa, hivyo naomba zipate umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikibakia hapo hapo kwenye umeme wa REA suala la nguzo imekuwa ni tatizo, tunauziwa nguzo kwa kiasi cha shilingi laki tatu na zaidi. Mimi mwenyewe ni muhanga wa kuuziwa nguzo kwenye eneo langu. Tunaambiwa kwamba umeme wa REA ni Sh.27,000 lakini tunapohitaji kuingiziwa umeme, nyumba ikiwa umbali kuanzia mita mia moja na kuendelea mwananchi unahitajika ulipie nguzo ya umeme. Hii hali haikubaliki na wananchi walio wengi ni maskini hawawezi ku-afford kununua nguzo hizi. Nimwombe Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana aweze kuliingilia kati suala hili na ikiwezekana kama ni suala la kununua nguzo basi itolewe bei elekezi ambayo ni rafiki kwa hao wananchi ili waweze kumudu gharama hizi na kuingiza umeme kwenye nyumba zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni afya. Jimbo langu la Ulyankulu lina kata 15 lakini vituo vya afya vilivyoko na vinavyofanya kazi ni kituo kimoja tu cha Barabara ya 10, hivyo msongamano ni mkubwa sana kutoka sehemu mbalimbali ambapo watumishi wa ile hospitali wanazidiwa. Niombe sasa bajeti ipangwe ili vituo vingine vya afya kama Kituo cha Mwongozo, Uyowa na Kashishi na vyenyewe viwekwe kwenye mpango ili vipatiwe pesa hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)