Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuweza kuniona. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya njema. Kipekee sana napenda kuwashukuru baba na mama yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nakishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniamini mimi kama binti na kama kijana kuweza kuwawakilisha akinamama wa Mkoa wa Katavi. Pia napenda sana kuwashukuru akinamama wote wa Mkoa wa Katavi na UWT kuanzia ngazi ya Mkoa mpaka Taifa. Pia kipekee naomba nimshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi anavyoendelea kuchapa kazi na jinsi anavyoendelea kulipeleka Taifa letu la Tanzania mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeisoma sana hotuba ya Mheshimiwa Rais, hotuba hii imebeba maono na dira ambayo inaonyesha ni jinsi gani Tanzania itakwenda mbele katika uchumi endelevu; kutoka uchumi wa kati mpaka uchumi wa juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana nijikite katika sekta ya afya. Naishukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa jinsi ambavyo inaendelea kupambana kuhakikisha kwamba huduma za afya zinaboreshwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii adhimu kuiomba sana Wizara ya Afya, watuboreshee Hospitali ya Wilaya ambayo kwa sasa inatumika kama Hospitali ya Mkoa wa Katavi, kutokana na kwamba mkoa wetu una fursa nyingi sana ikiwemo kilimo, biashara ambazo zinasababisha kuwepo na mwingiliano wa watu wengi. Hivyo, tunaomba sana Serikali yetu sikivu itusikie kwa kutuboreshea Hospitali ya Mkoa wetu wa Katavi ili iweze kuwahudumia wananchi wanaoingia kwa wingi kufuata fursa nyingi za kibiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile napenda sana nichukue nafasi hii katika kuchangia suala la kilimo. Katika hotuba hii Mheshimiwa Rais ameelezea kuhusu suala la kilimo kwamba atahakikisha kinasonga mbele katika nchi yetu ya Tanzania. Nikiwa kama mwakilishi wa akinamama Mkoa wa Katavi, wananchi wamenituma kwamba katika sekta ya kilimo, kumekuwa na sintofahamu kuhusiana na wakulima wetu. Wakulima wamekuwa na changamoto ambapo wanailalamikia Serikali kuhusu mambo ya Stakabadhi ghalani. Mheshimiwa Makamu wa Rais alipokuja mkoani kwetu alisema Mkoa wa Katavi wakulima wake hatujakidhi vigezo vya kuungwa katika Stakabadhi Ghalani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sekta ya kilimo iweze kutoa maelekezo na tamko: Je, wananchi wa Mkoa wa Katavi tumefikia hadhi ya kuungwa katika Stakabadhi Ghalani? Kama sivyo, basi waweke utaratibu ili wananchi wetu wa Mkoa wa Katavi ambao ni wapiga kura wetu waliotuamini sana waweze kuondokana na sintofahamu hiyo, kwa sababu wanategemea sana kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kuchukua fursa hii kuipongeza Wizara ya Elimu kwa jinsi ambavyo inaendelea kupambana. Namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi ambavyo anapeleka elimu yetu mbele kwa kutoa elimu bure kuanzia form one mpaka form four. Katika Mkoa wetu wa Katavi nasi tungependa kuwa na vyuo vingi kama ilivyo katika mikoa mingine. Vyuo hivyo vimwezeshe mtoto wa kike katika Mkoa wa Katavi aweze kwenda kupata elimu kwa ukaribu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nawakaribisha sana Waheshimiwa wenzangu mje mwekeze katika Mkoa wa Katavi wenye fursa nyingi zikiwemo za kiutalii na kilimo. Karibuni sana, Katavi imenoga jamani, karibuni. (Kicheko/Makofi)