Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Masasi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kunifanikisha kuwa hapa leo. Pili nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa imani yake kubwa aliyokuwa nayo kwangu kunipa utumishi wa kusimamia jukumu la Wizara yetu ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nisisahau chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa imani kubwa waliyokuwa nayo wajumbe wetu wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Masasi Mjini. Pia niwashukuru wananchi wa Masasi kwa kunipa kura nyingi na kunipa jukumu la kuwawakilisha kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuishukuru sana familia yangu akiwemo mke wangu Tumaini Jasson Kyando na watoto wangu King King, Caren, Catherine kwa imani kubwa waliyokuwa nayo na kunivumilia kwa kipindi kirefu cha utumishi wangu ambapo muda mwingi nakuwa nje ya nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza kabisa tumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Kimamlaka presidential speech is a policy speech. Rais anapata absolute powers kutoka kwenye Katiba, ana mamlaka yote. Mamlaka ya mwananchi mmoja mmoja yote yamekusanywa kupitia kura wakampa yeye. Kwa hiyo, tamko lake ni tamko la wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sisi watumishi ambao tunatumikia kwa nafasi zetu za kuongoza Wizara kwa niaba yenu, ni maelekezo na ni maagizo. Kwa hiyo, mwanzo kabisa napenda kusema kwamba naunga mkono hoja na sisi tumejipanga kutekeleza. Kazi yetu kubwa ni kutekeleza na tumeshaanza kuifanyia kazi hotuba hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri sana napenda nikumbushe kwamba hotuba ya Mheshimiwa Rais zote mbili ikiwemo hii ya terehe 13 Novemba 2020, zinawiana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025. Yote ambayo ameyaongea ni yale ambayo yako kwenye kurasa 303 ya Ilani ya CCM ambayo wengi wetu hapa tulikuwa tunainadi na bahati nzuri pia kila mmoja humu ndani hakuna ambaye amesema kwamba hotuba ile kuna maeneo hakubaliani nayo isipokuwa msisitizo ni namna sisi kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mlituambia wiki ijayo tutakuwa na mjadala wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitatu ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Rais inajikita huko pia. Baada ya Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ambao tulikuwa tunajikita kwenye kutengeneza miundombinu ikiwa ni kama capillaries za uchumi, wa pili tukasema tujenge viwanda lakini Mpango wa Tatu tunachukua sasa mafanikio ya kipindi cha kwanza na cha pili tunaunganisha kwenye mpango huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukipitia hotuba ile ukurasa wa 10 – 26 kuna maeneo mengi ambayo Mheshimiwa Rais ameyaelekeza ambayo yanagusa kwa namna moja au nyingine maeneo ya viwanda na biashara. Hivyo napenda kupitia hotuba hiyo kuangalia michango mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge ili tuweze kujua namna ambavyo sisi kama Wizara ya Viwanda na Bishara tumejiandaa. La kwanza, ni utekelezaji wa blue print. Kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walionesha kama vile tunahitaji tuanze kutekeleza lakini naomba niwahakikishie kwamba blue print tumeanza kuitekeleza tangu mwaka juzi na baadhi yenu mnafahamu hata ile iliyokuwa TFDA, sasa hivi inaitwa TMDA kutokana na utekelezaji wa blue print. Kwa hiyo, tutaenda kuhakikisha kwamba ile comprehensive action plan ya blue print tunaitekeleza ipasavyo na kuja na mbinu mpya zaidi ya kuweza kutekeleza vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa upande wa masoko imezungumzwa sana hapa kwamba bidhaa nyingi zinakosa masoko. Naomba niwahakikishie tunaenda kuiboresha taasisi/ mamlaka yetu ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) ambayo kimsingi imebeba jukumu la Board of Internal Trade (BIT) and Board of External Trade (BET). Bodi hizo mbili ziliunganishwa zikatengeneza TANTRADE, lengo lake kubwa au majukumu yake makubwa ni kutafuta masoko ya mazao yetu na bidhaa zetu kwa masoko ya ndani kuunganisha kutoka mkoa mmoja na mwingine, masoko ya kanda na masoko ya Kimataifa kupitia multilateral trading system ambayo sisi ni Wajumbe. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwenye hili tutaenda kupambana kuhakikisha masoko ya bidhaa zetu yanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna maboresho ya taasisi zetu. Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kiko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, nimewaambia kwamba tuangalie course content. Tusingependa na kwa kipindi hiki sio vyema kutengeneza business administrators yaani tunatengeneza wasimamizi wa biashara, biashara ya nani? Mimi nimewaambia wakae, waje na mpango mpya tutengeneze course content ambazo zinamjenga asilimia 70 yule mtoto yeye ndiyo akawe mfanyabiashara halafu asilimia 30 iwe ndiyo kusimamia biashara. Unakuwa business administrators wengi wanasimamia biashara ya nani? Kwa hiyo, tunaenda kuiboresha hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama WIzara ya Viwanda na Biashara, tutakuja na Programu ya Miliki Kiwanda ambayo nitaomba sana Waheshimiwa Wabunge kwa sababu Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake ametamani nyie muwe sehemu ya mabilionea mshiriki. Tutakuja na Programu ya Miliki Kiwanda ili kokote ulikokuwa kwenye Jimbo lako, wilaya yako tutengeneze utaratibu wa kuanzisha kiwanda wewe Mbunge ukiwa ni champion kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna masuala ya sekta binafsi. Sekta binafsi yetu ni changa sana tunahitaji kuijenga kwenye maeneo mawili. La kwanza, kuwapa fursa ya kuweza kufanya biashara. Hii tumezungumza mara kwa mara na nashukuru pia Mheshimiwa Waziri Mpango mara baada ya kuapishwa tu alikutana na uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania aliwasisitizia, kufunga biashara au kiwanda cha mtu iwe ni baada ya Commissioner General kutoa kibali. Biashara zote ziko chini ya leseni za viwanda na biashara, napenda kusisitiza sana, tuilee sekta binafsi lakini pia tuwaelimishe kwa upande wa integrity, lazima na wao wawajibike upande wao kuwa na integrity kwa Serikali ili iweze kuwaamini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)