Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Mpango wa Maendeleo. Awali ya yote nipende kumshukuru Mwenyekiti Mungu aliyenijalia kusimama katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiusoma Mpango wa Maendeleo, ukichukua Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi na ukiangalia hotuba za Mheshimiwa Rais, nyaraka zote hizi zinajielekeza katika kukuza uchumi wa nchi yetu, kupunguza umaskini na kuondoa ukosefu wa ajira nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakubaliana sote hapa Serikali ya Awamu ya Tano imejizatiti katika kukuza uchumi wa nchi yetu na hili linajidhihirisha pale Serikali ya Awamu ya Tano ilipoamua kwa makusudi kuanzisha miradi ama kujenga miradi ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ule ambao unaenda kutupa megawatt 2,115 nini tafsiri yake? Tafsiri yake ni kwamba viwanda vilivyopo na viwanda vitakavyojengwa vinaenda kupata umeme wa uhakika, vinaenda kupata ambao hauna kusuasua katika suala zima la kuchakata, kusindika, kuzalisha bidhaa na kupeleka sokoni, jambo ambalo linaenda kuleta mzunguko wa fedha. Bidhaa zinazozalishwa ni kwa ajili ya soko la ndani na zile zinazozalishwa kwa ajili ya kupelekwa nje exportation, jambo ambalo litatuletea forex, ni kitu ama ni chachu inayochochea ama inayochagiza uchumi wa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ujenzi wa reli iendayo kasi, ujenzi wa miundombinu ya barabara na ununuzi wa ndege mpya 11 vyote hivi kwa pamoja vinachagiza, vinachochea ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiuangalia Mpango, nitapenda kujielekeza jicho langu litaenda katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Uwekezaji pamoja na Wizara ya Mifugo. Nikianza na Wizara ya pacha, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Uwekezaji, ndani ya Mkoa wetu wa Pwani, lipo eneo linajulikana kama Kata ya Kwala, ama linajulikana Kwala. Kwala ni potential sana katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, ninapoizungumza Kwala ndio kule ambapo kuna biggest dry port, tuna bandari kavu kule, lakini pia tukiizungumzia Kwala, kuna sub-station kubwa ya umeme inayotoka Stigler’s kuelekea Chalinze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia i ukiizungumzia Kwala umepita pale Mto Ruvu, tunapoizungumzia Kwala kuna reli ya TAZARA pale, tunapoizungumzia Kata ya Kwala kuna central railway line ama SGR na measuring yard. Tutakubaliana halipo eneo katika Tanzania hii linalofana na Kata ya Kwala ndani ya Mkoa wa Pwani, lina vitu vyote, lina vichocheo vyote ambavyo mwekezaji yeyote akifika ndani ya nchi yetu leo hatashindwa kuwekeza pale kwa sababu lina vitu vyote ambavyo vinatakiwa ama niseme mwekezaji anavihitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kuwaomba Waziri mwenye dhamana ya viwanda na biashara na Waziri mwenye dhamana ya uwekezaji, kuhakikisha wanatenga eneo katika Kata ya Kwala kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. EPZA niwaombe sana tuache kuhangaika na maeneo ambayo yanahitaji fidia kwa wananchi, tunapozungumzia Kata ya Kwala pale wala hamuhitaji fidia, lile eneo lipo chini ya Serikali ambayo iko chini ya Wizara ya Mifugo, kwa hiyo Wizara ya Mifugo, Wizara ya Uwekezaji pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara ni watoto wa baba mmoja, wakae chini wazungumze waone namna bora ya kutenga eneo kwa ajili ya viwanda pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana tena sana Mawaziri niliowataja waangalie namna gani wanahakikisha wanalitangaza eneo la Kwala kwa sababu lina kila kitu ambacho leo mwekezaji akija anapata kwa mara moja, maji yapo, umeme upo, barabara ipo, kila kitu kipo, kwa hiyo, nataka niwaombe sana tuliangalie eneo hili kwa sababu linaenda kuleta uchumi wa haraka sana, matokeo ya uchumi tutayaona haraka sana litachochea ongezeko la uchumi na kupunguza umaskini kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri, Waziri mwenye dhamana ya uwekezaji, Jimbo lake ni Ubungo ambapo kimsingi akienda jimboni lazima atakatisha Mkoa wa Pwani na Waziri mwenye dhamana ya Viwanda na Biashara, Jimbo lake Masasi kimsingi akienda jimboni lazima atakatisha Mkoa wa Pwani. Kwa hiyo, niwaombe sana wakati wanaelekea jimboni wakatishe pale kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani awapatie hiki kitu Pwani Regional Investment Guideline, ambayo imeeleza kwa undani, thamani na ubora na jinsi gani Kwala itakavyoenda ku-boost uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wizara ya Mifugo ambayo kimsingi nimesema eneo kubwa la Kwala liko chini yao, nidhahiri Wizara ya mifugo wamehodhi eneo kubwa pale. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatoa maelekezo kwamba na sisi kama Mkoa wa Pwani tumeshaandika barua kuomba ekari 4,000 kwa ajili ya kuweka maeneo wezeshi kwa kupokea wawekezaji na kupokea viwanda. Tunahitaji hilo eneo la ekari 4000 kwa ajili ya ujenzi wa hoteli, benki pamoja na maeneo ya huduma za kijamii. Lengo na tija hapa kwamba once viwanda vinapokuja au wawekezaji wanapokuja wakute kila kitu kiko tayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine upo katika Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Kama ambavyo nimetangulia kusema kwamba Mradi huu unakwenda ku-boost uchumi wa nchi yetu na nipende kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uthubutu, umahiri na ujasiri, kimsingi hapa tuliwekewa vikwazo vingi kwamba kuna environment impact assessment na vikwazo vinavyofanana na hivyo kuhusiana na ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere lakini leo hii Mheshimiwa Rais wetu amefanikisha, hivi tunavyozungumza overall ya Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa upande wa nishati wameshafika asilimia 30. Nampongeza sana Waziri Dkt. Kalemani, lakini pia nampongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa lipo jambo ambalo tunataka kuzungumza kama Taifa, Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere unaenda sambamba na miradi mingine mingine katika Wizara zingine. Nitazungumzia mfano mradi wa kupump maji, Wizara ya Maji hatujasikia chochote mpaka dakika hii katika mradi ule wamefikia wapi na wamefikia hatua gani. Pia Wizara yenye dhamana na kilimo tunazungumzia suala zima la kilimo cha umwagiliaji kwamba ndiyo maana nasema Wizara ya Maji kwa kupitia mradi ule wakiya-pump yale maji inamaana yataenda kuwanufaisha watu wa Kibiti, Rufiji, Mkuranga, Kisarawe na majirani zetu Dar es Salaam. Kwa hiyo, tunapenda tusikie status, mpango ukoje kwa Wizara ya Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wizara ya Kilimo, tunasema kilimo cha umwagiliaji. Imezungumzwa na Wabunge wengi humu ndani kwamba viwanda vinahitaji malighafi sasa kama watu wako tayari kwa ajili ya kilimo kikubwa cha umwangiliaji na mradi wa Mwalimu Nyerere unaenda sambamba na masuala mazima ya kilimo cha umwangiliaji, nini kauli ya Serikali mmefikia wapi katika ule mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yenye dhamana na Ujenzi na Uchukuzi, mradi ule unaenda sambamba na ujenzi wa barabara ya Kibiti - Mloka yenye kilometa 97. Vilevile mradi ule unaenda sambamba na barabara ya Kisarawe - Vikuruti ambayo ina kilometa 167 (The Great Nyerere Road).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yenye zamana na Maliasili na Utalii, Wizara zote ambazo kimsingi kwa namna moja ama nyingine ziko katika Mradi wa Ujenzi wa wa Bwawa la Mwalimu Nyerere tungependa kusikia kauli na mipango kwa sababu mradi ule wa nishati utakapokamilika uende sambamba na hii miradi mingine. Tumesema itakuwa kazi bure kama tutakuwa na viwanda, tutazalisha tutachakata, halafu tutakosa miundombinu ama barabara ya kubeba bidhaa hizo na kuzipeleka sokoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni shukurani, napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa namna alivyotusaidia katika Kisiwa chetu cha Mafia kuhakikisha tunapata gati pamoja na kivuko maana ilikuwa adha kwa wafanyabiashara na kwa watu ambao wanachangia uchumi maeneo ya Mafia. Kwa sasa wamepata usafiri wa uhakika, kwa hiyo, wana nafasi nzuri ya kuchangia uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nipenda kutoa shukrani zangu kwa Chama cha Mapinduzi kwa kunipendekeza kuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwenye Bunge lako la Kumi na Mbili pamoja na kuwashukuru wanaweke wa Mkoa wa Pwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ahsante sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)