Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia. Kwanza kabisa, niendelee kukupongeza wewe kwamba katika kipindi chote ambacho mimi nimekuwa nikikufuatilia kuanzia ukiwa Naibu Spika na mpaka sasa hivi umekuwa Spika, kiukweli nafurahishwa na namna ambavyo unaendesha Bunge hili. Mimi niseme kwamba ni miongoni mwa Maspika bora kabisa Afrika ambao wanapaswa kuigwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais na niendelee kusema kwamba hata yeye amekuwa ni record breaker. Ni miongoni mwa Marais ambao wameingia kwenye historia, hakuna Taifa lolote kwa sasa ambalo unapotaja jina la Dkt. John Pombe Magufuli hawamjui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kuchangia Mpango wa Miaka Mitano na Mpango wa Mwaka Mmoja kwenye eneo la biashara na niendelee kuongelea kwenye eneo la mipaka. Mimi natamani kuishauri Serikali, kama ambavyo ulisema hapo kwamba sisi Wabunge wawakilishi wa wananchi ndiyo watu wa kwanza kabisa na sahihi wa kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali bado haijautendea haki mpaka wa lango la SADC. Napoiongelea nchi ya Kenya ina mipaka zaidi ya minne, kuna mpaka wa Sirari, Namanga, Holili, Tarakea na ule ambapo ukipita Tanga unaenda Mombasa, bado yote ile ni Kenya. Nchi moja tu ina mipaka karibu mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuishauri Serikali kwa kusema kwamba, there is no way Zambia itakuja kupata bahari. Dunia imeumbwa na itaondoka Tanzania ndiyo yenye bahari. Kwa vyovyote vile nchi zote ambazo ziko Kusini mwa Afrika zinategemea bandari ya Tanzania kutoa vitu vyao kutoka kwenye nchi za Ulaya na bado wanatarajia kupita Zambia kwa ajili ya kupeleka kwenye nchi nyingine. Kwa hiyo, naweza nikasema kwenye lile geti moja tu la pale Tunduma ni mpaka ndani ya mpaka. Unaonekana tunapakana na Zambia, lakini nyuma tumebeba nchi nyingi. Je, Serikali haioni sababu ya kupanua mpaka ule ili tuendelee kunufaika nao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea sehemu zile za Tunduma. Kumekuwa na wimbi kubwa sana la ndugu zetu kutoka vijijini, hata kwenye Kijiji changu ambacho mimi natoka, wapo wafanyabisahara pale wanasukuma baiskeli tu kwa ajili ya kupokea mizigo, lakini unapokuwa Tunduma hakuna biashara yoyote kubwa ya nyumba za kupanga kwa sababu hata Mtanzania wa kawaida ambaye hajui kusoma na kuandika kwa biashara ndogo ambayo anaifanya pale kwenye mpaka ana uwezo wa kujenga na kuishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaendelea kulalamika kwamba hakuna ajira. Je, hatuoni sababu ya kuboresha mipaka na sehemu nyingine hata wale wa darasa la saba mipaka itakapotanuliwa watakuja kupokea mizigo ya wageni, watajipatia riziki kwa sababu Mungu hakutuumba watu wote tukafanana ndiyo maana kuna Rais, Waziri, mwalimu wa shule ya msingi na kuna msukuma mkokoteni. Kwa hiyo, tutumie fursa tulizonazo kwa ajili ya kutatua matatizo. Bora kidogo cha halali kuliko kikubwa cha haramu, hata Maandiko Matakatifu yanasema, aliyenacho huongezewa asiyekuwanacho hunyang’anywa hata kile alichokuwanacho, lakini sisi tunavyo hatuvitumii sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee mfano ule ambao nilitaka kutoa nilipoishia, ni kwa namna gani biashara za magendo zinavyotoka zile nchi za Kusini mwa Afrika na hata nchi za Afrika ya Kati mfano Kongo. Kwa mfano, nikiongelea vipodozi, vipodozi vya kutoka Kongo vimekatazwa kuingia hapa nchini Tanzania inachukuliwa ni magendo, lakini ukipita huko Dar-Es-Salaam na sehemu nyingine, bado unakuta carolite zinauzwa, zinapitaje kama pale patrol inafanyika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Jimbo la Momba. Unapokuwa pale Livingstone, Zambia, mtu anapotoka na bidhaa Namibia, Zimbabwe au Botswana, anapoingia Lusaka unafika mji mmoja unaitwa Mpika, pale kuna njia mbili njiapanda. Whether uamue kwenda Ndola ambapo uende border ya Kasumbalesa kule mtu achukue vile vipodozi. Anapokuwa pale Mpika ana uwezo wa kuamua kupita barabara ya Tunduma atokee pale lilipo lango la SADC au aamue kupita mahali kunaitwa Kasama kutokea Mbara Road anaingia upande wa Jimbo la Momba ambapo kutokea inapoanzia Tanzania kuingia tarmac ya Zambia ni kilometa moja tu na nusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niliyesimama hapa ni living testimony, natoka kwenye kata ya mpakani, kipindi chote nikiwa nasoma Mbeya Day, inapofika kuanzia mwezi wa kumi na mbili, wa kwanza, barabara hazipitiki tunapaswa kwenda kupita Zambia ili tuweze kufika Tunduma, mazao na mifugo mingi inatoroshwa kwa kutumia njia hiyo kwa sababu iko wazi, hakuna utaratibu wowote pale. Serikali kama mnasikiliza ushauri tunaona ipo sababu, iko nia na manufaa ambayo tutayapata pale ambapo tutaongeza geti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea kuongezea, kuna soko kubwa la kimataifa ambalo limejengwa ndani ya Jimbo la Momba kwenye Kata moja inaitwa Ndalambo, Kakozi. Ni soko la kimataifa zaidi ya shilingi bilioni 8 Serikali imeweka pale. Kwanza, Serikali yenyewe iliona kwamba ni soko la kimataifa la mazao na mifugo lijengwe kwenye mpaka. Sasa kama limejengwa kwenye mpaka soko hili litachochewa na nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutataka tena kutoa mazao ambayo yanatoka Rukwa, Jimbo la Momba yaende yakapite Tunduma? Hizi halmashauri nyingine zinakuwaje? Zinawezaje kujitegemea kama haziwezi kusimama, mazao yote yanatoka yanaenda Tunduma na hili soko? Pia lilipo soko ndipo ilipo barabara ambayo inapita kwenda kwa baba yangu Mheshimiwa Kandege kwenda kwenye bandari ya Kalemii. Kwa nini kusiwe kuna sababu ya kupata geti? Tunaiomba na kuishauri Serikali tupate geti mahali hapo ili tuweze kuzuia biashara zote haramu na za magendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea, kumetokea migogoro mingi sana ya ardhi, kutokana na kwamba tuko mpakani Congolese na Zambians wengi wanawatumia Watanzania hawa kwa ajili ya kuja kumiliki ardhi kwa sababu ni kwenye mpaka. Tunaiomba sana Wizara yenye dhamana husika jambo hili muliangalie kwa karibu sana. Tunaomba Wizara ya Ardhi ifuatilie hati zote ambapo watu wanaonekana wanapata hati ndani ya Halmashauri ya Momba na muda mwingine ni wafanyabiashara hawa wanavaa uhusika wa Tanzania lakini wanawalinda hawa watu ni wahamiaji. Sheria ya Ardhi ya Tanzania inamkataza mtu yeyote asiyekuwa Mtanzania kumiliki ardhi. Kama anataka kumiliki kama mwekezaji ziko sheria ambazo zina mwongozo mtu huyo ni kwa namna gani anaweza kumiliki ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea hapohapo kwenye suala la ardhi. Sisi watu wa Halmashauri ya Momba na halmashauri nyingine ambao wanapitia changamoto kama hii, hatutamani kuona tunafika kwenye matatizo ambayo ndugu zetu wa Kiteto na Morogoro wanayo. Limetokea wimbi kubwa la wawekezaji ndani ya Jimbo la Momba kutokana na ule mwamko wa lile soko kuwepo na ule mpaka, kuja kumiliki ardhi kinyume na taratibu. Kaka yangu Mheshimiwa Kunambi alisema pale, tunaomba ardhi ambayo inaonekana iko sehemu ambayo ni muhimu, kwa mfano sehemu kama hizi za mipaka, kwa kuwa wananchi wa maeneo haya wengi wao wanakuwa ni watu wa kipato kidogo, Serikali iingilie kati iyapime yale maeneo. Itusaidie kuyapima siku zijazo yatatusaidia kwa sababu tunajua tu lazima mpaka utafunguka, biashara nyingi zitafanyika na ardhi itapanda thamani mahali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji hawa cha kwanza wanamiliki ardhi kinyume na taratibu. Mtu anamiliki ardhi eka 800, lakini amepata hati ambayo amepewa na Kijiji au mtu anamiliki ardhi zaidi ya eka 100, kutoka eka 50 mpaka eka 100 alipaswa angalau apewe na halmashauri, lakini anasema ana hati ya Kijiji. Wanamiliki ardhi kinyume na taratibu lakini hawaziendelezi ardhi hizi pia hawalipi kodi ya ardhi. Wao ndiyo watu wa kwanza kuchukua sheria mkononi na kuanza kuwaweka watu ndani. Wao wameshavunja sheria tatu, lakini wanawaweka watu ndani.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: AHsante sana Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)