Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Segerea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kwanza kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Segerea kwa kunirudisha kwa awamu ya pili lakini shukrani za pekee ziwaendee wajumbe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika Mpango wa Miaka Mitano ambao Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameweza kuuwasilisha hapa. Napenda niweke mawazo yangu katika huu Mpango; napendekeza kwamba kuwepo na mpango kwa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye suala la miundombinu. Nasema hivyo kwa sababu ukiangalia kwa sasa hivi Mkoa wa Dar es Salaam unachangia mapato makubwa katika Taifa na ni mkoa wa kibiashara lakini pia ndiyo Mkoa ambao una Manispaa sita katika mikoa yote ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu ni kwamba katika Mkoa wa Dar es Salaam miundombinu iliyopo sasa hivi mvua ikinyesha kwa nusu saa Dar es Salaam nzima inasimama. Katika kusimama huko mapato mengi yanapotea kwa sababu watu wanapokuwa hawafanyi kazi wanasubiri mvua iishe au kuna mafuriko ambayo yametokea, hakuna mama ntilie ambaye anapata wateja, hakuna bodaboda ambaye anatembea lakini pia kunakuwa kuna mambo mengi ambayo yanasimama kutokana na miundombinu ya Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mapendekezo ni kwamba katika huu Mpango wa Miaka Mitano Serikali ije na mpango wa kuhakikisha kwamba Mkoa wa Dar es Salaam unatengenezewa miundombinu ambayo itakuwa ya permanent. Kwa sababu kwa sasa hivi kila mvua inaponyesha Mkoa wa Dar es Salaam lazima tuchukue siku tatu au nne tunahangaika na mafuriko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika bajeti yetu hii ya mwaka. Mfano bajeti ya TARURA, kwa Manispaa ya Ilala wanapata bilioni tano, bilioni tano inatengeneza barabara moja na ukiangalia Wilaya ya Ilala kilometa 1,200 bado hazijawekewa lami. Kwa hiyo, tukifuata hii bajeti ambayo ni ya mwaka kwa mwaka katika Mkoa wa Dar es Salaam, hatuwezi kufikia malengo ambayo tunataka kuyafikia. TARURA wakipewa shilingi bilioni tano, wanatengeneza barabara moja. Mfano sasa hivi kuna barabara moja ambayo inatengenezwa; barabara ya Vingunguti – Barakuda ambayo ina kilometa 7.6. inatengenezwa kwa shilingi bilioni 7.8. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama TARURA wanapata shilingi bilioni tano kwa mwaka kwa majimbo matatu, nikimaanisha Jimbo la Ilala, Segerea pamoja na Ukonga, ina maana haya majimbo mengine yote mawili yatakuwa yamekaa hayafanyi kitu chochote na wala hawana fedha za ukarabati. Ukiangalia Mkoa wa Dar es Salaam, Kata ambazo ziko pembezoni mwa mji, water table yake iko juu sana. Kwa hiyo, barabara yoyote ambayo inatakiwa kutengenezwa na iweze kudumu, basi hiyo barabara inatakiwa iwe imepangiwa fedha nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie ni jinsi gani italeta mpango ambao unaweza ukaenda kufanya kazi katika Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa sababu ukizungumzia Dar es Salaam, siyo sawa na Bukoba, siyo sawa na Kigoma na wala Shinyanga.
Kwa hiyo, sisi watu wa Dar es Salaam na wananchi wetu ambao wako Mkoa wa Dar es Salaam, wanachangia mapato makubwa katika Taifa. Kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali, ili tumalizane na hili jambo la mafuriko, maana kila mwaka tunapata mafuriko zaidi ya mara mbili au mara tatu. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Kweli kabisa.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ili tumalizane na hili jambo la mafuriko, tunaomba Serikali ije na mpango ambao utaweza kumaliza mafuriko ya Dar es Salaam kwa mara moja. Hili jambo linaweza likatusaidia, wananchi wetu waweze kuendelea kufanya kazi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililokuwa nataka kuongelea ni kuhusiana na Miradi ya DMDP ambayo inaboresha makazi. Hii miradi phase ya kwanza imemalizika, sasa tunaenda phase ya pili, lakini mpaka sasa hivi hii miradi imesimama. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali iweze kufanya mpango hii miradi iweze kuendelea kwa sababu ndiyo inayoleta matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi. Kwa hiyo, naomba sana katika huu Mpango, Serikali ije na mpango maalum katika Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)