Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii pia kumshukuru Mwenyezi Mungu, wapiga kura wangu wa Jimbo la Mufindi Kusini na chama changu kwa heshima ya kunifikisha hapa leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwa ufupi mambo machache juu ya Mpango ambao umewasilishwa vizuri sana na Mheshimiwa Waziri. Eneo la kwanza napenda kupongeza Mpango uliopita kwani tumefanya vizuri sana kwenye eneo la diplomasia. Tumefanya vizuri sana kwa maana tumeona matokeo makubwa kama vile unaona sasa uanzishwaji wa zile Kampuni ya Twiga ambapo Serikali ina asilimia 16, bomba la mafuta la kutoka Hoima – Tanga, haya ni matokeo ya sera nzuri sana ya diplomasia ya uchumi na usimamizi makini wa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha Mpango atusaidie. Tunafanya kazi nzuri sana ya kuhamasisha watu wa nje kuja kuwekeza nchini, ni upi mkakati sasa wa sisi Watanzania kuhamasisha wafanyabiashara wetu, kuwapa mikopo na ruzuku waende wakawekeze kwenye nchi zingine? Tungetamani kuona magazeti yetu, vyombo vya habari vyetu na kampuni zetu, kama Clouds na wengine wanakwenda kwenye nchi zingine za nje ili kuweza kuongeza uwekezaji na mapato kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili napenda kuchangia kwa ufupi sana kwenye eneo la kilimo. Tunafahamu asilimia 7 ya ardhi ya China wanaitumia kwenye kuzalisha asilimia 22 ya mazao duniani. Sisi kwetu sekta hii inatusaidia kwa asilimia karibia 63 na mimi nijikite kwenye mazao makuu mawili ya chai na parachichi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba katika mazao ya kimkakati ambayo yametajwa ni vyema tukaweka na sheria kabisa ili kuyatambua na kuyawekea ruzuku maalum. Kwa mfano, kwenye zao la chai ambapo moja kati ya wilaya zinalima ni pamoja na kwetu kule Mufindi Kusini. Ukitazama kwenye zao la chai sisi hapa kama Tanzania tumezalisha karibia tani 37,000 lakini tunazouza nje ya nchi ni kidogo sana. Wenzetu Wakenya wanazalisha karibia tani 432,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza najiuliza, pamoja na diplomasia yetu nzuri katika masoko ya dunia, ni kwa nini chai yetu inapelekwa kwa kiasi kidogo nje ya nchi? Changamoto ni nini?
Kwa hiyo, napenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atusaidie pia Mpango wa kuweza kusaidia zao kama la chai ili ikiwezekana zitolewe pembejeo kwa wakulima, wahamasishwe watu wa kuweka viwanda vya kutosha katika eneo hili lakini zaidi ya yote mkakati wa namna ya kutoa huduma za ugani kwa sababu ndizo zinazoongeza gharama kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni eneo la parachichi. Naomba zao hili liingizwe katika mazao ambayo tunayaita ni ya kimkakati kwenye nchi yetu. Kwa Mikoa kama Mbeya, Njombe mpaka Iringa ni zao ambalo tunaliita green gold yaani dhahabu ya kijani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hapa tunapeleka nje ya nchi tani 8,500. Wenzetu Wakenya peke yao walipeleka tani 68,000 ikawaingizia pesa za kigeni dola milioni 128 lakini ukiichimbua zaidi sehemu kubwa zimetoka nchini kwetu. Ni upi mkakati wa Wizara, kwa sababu hapa haiwezekani maparachichi yanatoka kwenye maeneo yetu yanapelekwa Kenya halafu yanakwenda nje ya nchi inaonekana Kenya ndiyo inazalisha kwa kiasi kikubwa zaidi, shida ni nini?. Napenda kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri anisaidie kwenye eneo hili pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama China asilimia 40 ya soko la China, Kenya ndiyo wanapeleka lakini sisi tunafahamu kihistoria, Tanzania mahusiano yake na China ni makubwa kuanzia uhuru. Tunakosea wapi? Kwa nini watuzidi kete? Ukifuatilia nchini kwetu miradi ya ujenzi wa barabara na ya maji, kampuni za China zimejaa hapa. Kwa nini diplomasia yetu ya uchumi isitusaidie kupeleka mazao kama haya kwao, urafiki wetu una faida gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kwenye viwanda. Kwanza napenda kuomba maeneo ambayo ni nyeti kwenye viwanda kama Mufindi Kusini yatangazwe kama ni ukanda maalum wa viwanda ili pengine msukumo wa kipekee uweze kuwekwa. Nimefurahi commitment ya Serikali asubuhi ya leo na kwa kweli nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi alipotamka kwamba katika bajeti itakayokwenda kuanza sasa tutakwenda kujenga barabara ya Mtwango – Nyololo kilometa 40, Mafinga – Mgololo kilometa 75.6. Barabara hii…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, kengele tayari.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)