Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa ili niweze kuwa sehemu ya wachangiaji katika Rasimu ya Mpango. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya, maajabu ambayo nimetendewa kati ya Wabunge ambao 28 waliopita bila kupingwa ni pamoja na mimi, nina kila sababu ya kuwashukuru wannachi wa Jimbo la Kalambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Bajeti kwa hiyo nilitoa mchango wa kutosha. Hata hivyo, leo nitajielekeza katika masuala mawili; la kwanza itakuwa upande wa kilimo na la pili kama muda utatosha litakuwa upande wa local contents.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kimekuwa sio cha kuvutia kwa sababu hakuna incentive ya kutosha ambayo imewekezwa ili mwananchi ambaye analima aone tija katika kilimo. Nawe ni shujaa unajua kabisa yaliyotokea miaka ya nyuma, leo nikipita nauliza hivi yako wapi mafuta yaliyokuwa yanatokana na karanga? Siyaoni, yako wapi mafuta ya kula yanayotokana na pamba? Siyaoni. Iko wapi Tanbond? Siioni, iko wapi Super Ghee siioni, iko wapi samli iliyoboreshwa, sioni. Yako wapi mafuta ambayo yanatokana na mahindi ambayo yamezalishwa Tanzania? Sioni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufike wakati sasa ili wananchi wanaotoka Rukwa, Ruvuma, Iringa na maeneo mengine ambayo wanazalisha mahindi wasipate tabu ya kutafuta soko, wanafanya kazi kubwa sana katika kulima, si wajibu wao kutafuta soko. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba inaweka mazingira yaliyo bora ili mkulima kazi yake iwe ni kulima mbegu iliyokuwa bora na soko litafutwe na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tutafanyaje? Kwa kuhakikisha kwamba sio kwamba mahindi yatumike kwa ajili ya chakula cha binadamu peke yake, tu-extract kutoka kwenye mahindi tupate mafuta inasemekana kwamba ni mafuta yaliyo bora na tukienda supermarket unayakuta. Mafuta haya yanapatikana wapi? Kama iko mbegu mahsusi ni wajibu wa Serikali kwa kupitia research and development kutuletea mbegu hizi ili wakulima wetu waweze kufaidika na kilimo hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende mbali Zaidi, sasa hivi bei ya mafuta ya kula imepanda kweli kweli. Zaidi ya dola milioni 126 tunatumia kama nchi kwa ajili ya kuagiza mafuta. Tafsiri yake ni kwamba ajira tunawapelekea wengine na sisi tunabaki kuwa soko. Ifike wakati wa kuwekeza vya kutosha ili mafuta ya kula ambayo yanachukua mzigo mkubwa kwa Taifa tuweze kupeleka kwa watu wetu ili kilimo kiwe na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la local content. Ukitafuta namna gani tunamsaidia Mtanzania, mzalendo ili aone fahari ya kuzaliwa Tanzania tofauti na mwingine ambaye hakuzaliwa Tanzania, unatafuta kwa kurunzi ndiyo unaenda kuziona hizo fursa. Ifike wakati kwa makusudi mazima kama ambavyo wenzetu wamefanya kama Afrika ya Kusini, mwananchi wa Afrika Kusini anajua haki zake katika kuwekeza na fursa zipi ambazo anatakiwa kuzipata. Ni wakati muafaka tusione aibu ya kumpendelea Mtanzania ajivunie na fursa za kuwa Mtanzania na zionekane wazi. Hizi sheria ambazo zipo unaenda kwenye madini ndiyo unakutana nayo, sijui unaenda wapi zote zikusanywe kwa pamoja ili ionekane dhahiri kwa Mtanzania fursa alizonazo na upendeleo wa Dhahiri, tusione aibu kuwapendelea Watanzania. Wako wa nchi za jirani ambao wao wamekuwa na wivu na watu wao. Ni wakati muafaka, tusichelewe muda ndiyo sasa hivi, tuhakikishe kwamba tunawalinda Watanzania kwa kuweka vivutio vya wazi kabisa bila hata kuona aibu katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda upande wa ujenzi, kazi kubwa sana imefanyika katika ujenzi wa miundombinu, lakini ni watu gani ambao wamejenga hiyo miundombinu na hiyo fedha ambayo wamepata wameenda kuwekeza wapi, utakuta kwamba inaenda kwa wenzetu. Ni wakati muafaka kuhakikisha kwamba tunawasaidia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)