Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza kupitia kitabu cha Mpango tunaojadili wa mwaka mmoja na miaka mitano ukurasa wa 13; nipende tu kusema ndugu zangu Wabunge wote twende pamoja, pamoja na kwamba tunajadili Mpango ambao uko mbele yetu, tujaribu kukumbushana tu kupitia ukurasa wa 13 yale mazuri ambayo ameyafanya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ili tunapokwenda kujadili twende sambamba pasipo kupotosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, baadhi tu peke yake idadi ya kaya imeongezeka, zilizounganishiwa umeme zaidi ya 14.9% ndani ya miaka mitano (2015 mpaka 2020 Desemba). Vijiji vilivyounganishiwa umeme kutoka vijiji 2000 mpaka vijiji 10,000. Kuongezeka kwa kiwango cha uandikishaji, juzi Waheshimiwa Wabunge tulikuwa tunajadili hapa namna idadi ya wanafunzi walivyoongezeka mpaka madarasa yamepungua na mengine mengi ambayo ameyafanya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kwa hiyo tunapokwenda kujadili Mpango uliopo mbele yetu tunatakiwa tujadili yale mazuri ambayo yako mbele, lakini tujaribu kuainisha changamoto, namna gani sasa Waziri wa Mipango, Waziri aliyewasilisha Mpango huu aone namna gani sasa anatoka hapa ili kwenda mbele kuyafanyia kazi yale mawazo yote ya Waheshimiwa Wabunge bila kubagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia hilo niende kujadili Jimbo langu la Rorya. Leo asubuhi tulikuwa tunajadili hapa Mheshimiwa Waziri alikuwa anajibu kuhusiana na hoja ya maji. Ndani ya Jimbo la Rorya, zaidi ya 77% imezungukwa na maji maana yake shughuli kubwa ya kiuchumi ukiacha shughuli ya kijamii ya maji, ni uvuvi. Mpango unasema kuna mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa zaidi ya dola milioni 500 ambao unatoka kwenye Jimbo la Rorya unakwenda Tarime, lakini kijiji ambacho unatoka jimbo ambalo unatoka huo mradi halijawekwa kwenye mpango wa utekelezaji wa hayo maji. Kwa hiyo, naomba sana, tunapojadili na tunapopanga mipango tuangalie namna gani inagusa wananchi kwenye maeneo ambao mradi unatoka ili kwenda maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ushauri wangu kwenye upande wa viwanda, natamani sana nimshauri Mheshimiwa Waziri upande wa viwanda, viwanda hivi ninavyovizungumza yawezekana visiwe vina mashiko sana hasa maeneo ya vijijini. Ningetamani sana Serikali ije na mpango wa namna gani ambayo itaanzisha viwanda ambavyo zinashiriki moja kwa moja kwenye shughuli za maendeleo za kiuchumi za kule ndani ya halmashauri, ikibidi waainishe mazao ya kibiashara ambayo yanatolewa kwenye halmashauri husika ili Serikali iwe na mpango wa kiwanda kulingana na zao la kibiashara linalozalishwa kwenye halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu ukitoa tathmini ongezeko la viwanda, leo tunasema kuna ongezeko la viwanda zaidi ya 8,400, yawezekana kwenye maeneo mengine hicho kiwanda hakipo. Kwa hiyo, yawezekana ukisema kuna ongezeko la viwanda kuna baadhi ya maeneo haliwagusi moja kwa moja wale wananchi, maana yake watakuwa wanashabikia ule mpango, lakini hauwagusi wale wananchi wa chini kabisa ambao tunawawakilisha. Ningetamani kwenye hii mipango Serikali izingatie sana unapopanga mipango ya kuongezeka viwanda, basi viwanda viwe moja kwa moja kwenye maeneo ambako kuna uzalishaji kwa wananchi hasa ukizingatia yale mazao wanayozalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nizungumzie sana upande wa uvuvi, mimi kama nilivyosema 77% ya jimbo langu inazungukwa na maji, shughuli kubwa inayofanyika kule ni uvuvi, lakini ndani ya miaka hii mitano iliyopita nyinyi wote mtakuwa mashahidi, wavuvi hawa hawana furaha kwenye maeneo yao. Ningetamani sana kama nilivyosema mara ya kwanza, Serikali ije na mpango wa namna gani itakaa na hawa wavuvi, ianishe na ione ni changamoto gani kubwa inawasumbua, kama shida ni nyenzo zile za uvuvi, wenyewe wanasema wanaponunua hakuna shida, ikija huku inakuwa na shida, Serikali ione namna gani inavyowasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeomba Serikali kupitia Ofisi ya DPP iende ikaone wale wavuvi wadogo wadogo waliokamatwa kwa miaka mitano kwa makosa ya uhujumu uchumi ili iweze kuona namna gani inaweza ikawasaidia ili kuwaondoa, kwa sababu kuna wengine kimsingi mwingine hana hata fedha, lakini amekamatwa kwa makosa ya uhujumu uchumi. Kwa hiyo tuone namna gani kupitia Ofisi ya DPP inaweza ikawaona hawa watu na ikawasaidia kwa maana hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakiniā¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Muda umeisha Mheshimiwa, kengele imeshagonga.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)