Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Mpango huu wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuipongeza sana Wizara kwa kuleta Mpango huu. Nitajikita katika vipaumbele vitano vya mpango huu na nitajikita kwenye kipaumbele namba tatu ambacho kinasema, kukuza biashara na kipengele namba nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja nijielekeze kushauri mambo kadhaa kwa ajili ya Mpango huu ambao umekuja mbele yetu. Kwanza, nitazungumzia mpaka wetu wa Kongo na Kigoma. Mpaka huu kihistoria unaonyesha kwamba umekuwa na mchango mkubwa wa kukuza uchumi katika Mkoa wetu wa Kigoma na hata kwa Taifa letu la Tanzania. Hivi karibuni hali ya kibiashara Mkoani Kigoma imedorora na imekuwa ni ya chini sana kwa sababu mpaka ule umekuwa hauthaminiwi. Hii ni kutokana na sera za kiuchumi ambazo kwa kweli Serikali ikizifanyia kazi tunaweza tukatoka mahali hapa tulipo na kuelekea sehemu ambayo tunataka twende. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisoma historia ya mpaka ule wa Kongo na Tanzania inaonesha kabisa mwaka 1986 mpaka 1993 kulitokea Mkuu wa Mkoa wa pale kwetu Kigoma, Mkuu wa Mkoa wa kumi kama sijakosea, alikuwa akiitwa Christian Mzindakaya. Mzindakaya alifanya mambo makubwa sana katika uongozi wake ambayo yaliweza kuitoa Kigoma mahali ambapo katika hali ya uchumi ilikuwa ni kwenye shimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye alifanya vitu vichache tu; alichokifanya ni kurekebisha baadhi ya sera za kiuchumi, mfano visa fee ya wa Kongo kuja pale Kigoma aliweza kuishusha, lakini akaondoa na usumbufu wa wageni ambao umekuwepo hivi sasa na unashusha uchumi katika mkoa wetu wa Kigoma. Hivi sasa Mkongo akitoka Kongo kuja Kigoma anasumbuliwa na taasisi nyingi, akiingia tu kidogo TRA atakuwa nyuma, akikaa kidogo hata Polisi atamfuata kwenye hotel. Jambo hilo limekuwa likiwachukiza na hatimaye linaweza kushusha uchumi wetu. Naishauri Serikali kwamba kwa kutumia tu mpaka wa Kongo tunaweza tukapata mapato makubwa sana na tukaweza kusaidia hali ya uchumi katika Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nizungumzie zao la kahawa. Zao la kahawa linaweweseka sana na nimeweza kushauri hata hapo nyuma nimekaa na Naibu Waziri Kilimo nikamweleza, zao la kahawa linadorora kutokana na vyama vya ushirika tulivyonavyo. Vyama vingi vya ushirika mpaka dakika hii havijawalipa wakulima pesa zao na hawa wakulima wamewakopesha toka mwaka jana na wengine mpaka dakika hii wanawadai. Mfano pale jimboni kwangu kuna Chama cha Kalinzi Mkongoro kina wanachama 273 bado kinadai pesa zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hali inasababisha zao hili la kahawa na tena kahawa inayotoka Kigoma imeonesha inapendwa duniani kote. Kwa namna hii ambavyo tunalimbikiza madeni ya wakulima kwa kweli inashusha hali ya zao hili la kahawa na kusababisha kukosa mapato mengi kwa sababu zao la kahawa ni la tatu kwa kuingiza fedha kigeni hapa nchini kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na muda pia nigusie kipengele cha elimu. Ni kweli tunaandaa vijana wetu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)