Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami nichangie Mpango ulioko mbele yetu. Kwanza, niungane na waliotangulia kuchangia Mpango huu wa maendeleo ambao dhima yake kubwa ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wowote hauwezi kufanikiwa endapo maeneo fulani hayatapewa kipaumbele. Nitaanza na eneo la kilimo. Asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania wanashiriki kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kilimo lakini kilimo hiki sasa hivi badala ya kuwa uti wa mgongo kinakuwa ni kiua mgongo cha wananchi walio wengi, hasa wa maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu, kilimo sasa hivi hakina tija kwa wakulima wetu badala yake kimekuwa kinaleta dhiki kwa hawa wakulima wetu na hatimaye kuwasababishia kukata tamaa. Hivyo, niiombe na kuishauri Serikali, kama kweli tuna nia ya dhati ya kufikia malengo yaliyokusudiwa katika mpango huu, basi Sekta hii ya Kilimo ipewe kipaumbele hasa kwa kuiongezea bajeti. Pia masoko kwa ajili ya bidhaa za wakulima wetu yapatikane na yawe na bei elekezi ili hawa wananchi wetu waweze kuwa na uhakika wa kuuza mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la bima ya kilimo; suala hili kama halitapewa kipaumbele wananchi wetu watakuwa na uhakika hata kama yatatokea mabadiliko ya hali ya hewa, basi watakuwa na uhakika wa kufidiwa endapo matatizo ya kijiografia yanaweza yakatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwenye kilimo ni suala la kuanzisha hizi block farming ambazo kwa kiasi kikubwa zitakuwa zina tija kwa hawa wananchi wetu kwani asilimia kubwa ya maeneo yaliyopo Tanzania hayalimwi kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, kama tutaanzisha hizi block farming, nina uhakika kabisa wananchi watalima kwa eneo kubwa na pia watakuwa na uhakika wa masoko ya mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uhakika wa pembejeo kufika kwa wakati na kuwezesha mazao ambayo yako kwenye ushindani katika Soko la Dunia. Mfano kwenye maeneo yetu, mazao kama tumbaku, chikichi na korosho, ni mazao ambayo yanaweza yakahimili udongo kwenye maeneo yetu. Hivyo, naomba mazao haya sasa yawekewe umuhimu mkubwa na wananchi waweze kuelimishwa juu ya kulima mazao haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala lingine la TARURA. Hatuwezi kuwa na uchumi wa viwanda endapo tu uhakika wa kusafirisha mazao yetu hautakuwepo kutokana na barabara nyingi kuwa mbovu. Barabara nyingi sana ambazo ndiyo zinalisha barabara kubwa ni mbovu na hazipitiki. Hivi mfano ninavyoongea mimi barabara yangu ya kutoka Mnange - Uliyanhulu, Urambo - Uliyanhulu, Uliyanhulu – Tabora ambazo zinapitisha bidhaa nyingi sana, ni mbovu na hazipitiki. Naomba TARURA iongezewe bajeti kwani bajeti inayowekwa ni ndogo sana ukilinganisha na mtandao wa barabara unaohudumiwa na TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naziomba Halmashauri na ikiwezekana zilazimishwe, ziweze kuwa na vitendea kazi; mitambo ya kutendea kazi kama excavator, magreda na kadhalika. Vifaa hivi vikiwepo Halmashauri zetu zitakuwa na uwezo wa kufanya matengenezo ya barabara zetu pindi inapotokea uharibifu wa mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nafikiria kuna haja sasa ya kufanya mabadiliko kwenye bajeti ya TARURA ya TANROADS. Haiwezekani kila mwaka tutegemee bajeti hiyo hiyo ya TARURA ya asilimia 30 na TANROADS asilimia 70. Naomba kama kutakuwa na demand na kwa wakati huo, basi pawepo na mabadiliko. Kama demand itakuwa ni kubwa kwa wakati huo, TARURA iweze kuongezewa bajeti kuliko mtindo uliopo sasa hivi wa kutegemea bajeti hiyo hiyo tu kila mwaka bila kuangalia kwamba mahitaji yanabadilika kulingana na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la ukusanyaji wa mapato. Katika Mpango huu kilicholeta mtafaruku mpaka changamoto hizi zitokee na Mpango usifanikiwe inavyotakiwa ni kukosekana kwa mapato kwa wakati na yanayotosheleza. Hivyo, naomba sasa Halmashauri na Serikali ziweze kubuni vyanzo vingine vya mapato ambavyo ni vikubwa kuliko kutegemea vyanzo vidogo vidogo. Leo Serikali inategemea vyanzo vidogo vya mapato hali ambavyo inasababisha mapato yasipatikane. Pia ni kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia watu wenye utaalam kuliko task force, kazi yao ni ku-force tu watu na kusababisha utoroshaji wa mapato kwa njia ambazo siyo stahiki.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)