Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Mpango wa Tano wa Maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ya msingi tunapotaka kufanya mabadiliko ya kiuchumi na kwenye biashara. Ukichukua mfano wa nchi ya China ilipotaka kufanya mabadiliko yake kwenye masuala ya uchumi na biashara zaidi ya miaka 40 walikuwa wakiendelea kusuguana na sheria na sera zao. Mipango na mikakati yao ilikuwa imekaa vizuri; ilikuwa ikijali muda, lakini ukienda kwenye mambo ya sheria na sera zao zilikuwa zinawarudisha nyuma na zikafanya uchumi wao kuendelea kuwa duni, ulishindwa kuendelea kukua, tegemezi na usiozingatia ushindani wa kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye walipoamua sasa kuanza kubadili sera na sheria zao ndipo walipoanza kuleta maendeleo makubwa na ndani ya miaka nane kwa ripoti za Benki ya Dunia, walikuwa wanakua mara mbili zaidi ya GDP ambayo ilikuwa ni kwa asilimia 9.5. Ndipo walipoweza sasa kutoa umaskini kwa watu wao zaidi ya milioni 800 maana tunapoongelea China ni watu zaidi ya milioni 1,400.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa Mpango huu wa kwetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ni mzuri na umezingatia standard na spidi au umejikita katika muda lakini kikwazo kikubwa kitakachokuja kutukuta, katika ukurasa wa tano wa maeneo ya muhimu ya kuzingatia ambao Mpango unaeleza, umeeleza mambo mazuri lakini haukuweka msisitizo katika kuhakikisha kwamba tunabadili na sisi sheria na sera zetu ambazo huwa zinatusababisha tusiende kwa spidi au tusiende kwa wakati ule ambao tumeupanga, hicho kipengele hakijawekwa. Kwa hiyo, tunaomba tushauri kwamba katika Mpango huu tujaribu kuangalia namna gani tutabadilisha sheria na sera zetu ili ziweze kuendana na muda ili tuweze kuutekeleza huu mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi sana tumekuwa tukipanga vitu vingi lakini unakuta kuna sheria zinakinzana. Tunakwenda kwa spidi tunataka kuinua utalii, Mpango unatuambia kwamba tutoke katika watalii 1,500,000 mpaka itakapofika 2025 tuwe tumefika watalii 5,000,000, lakini kuna sera nyingine ambazo zipo sasa zinahusiana na masuala ya kutoa vibali au permit za kuishi, unakuta zinakinzana na ile sera ya sisi kuboresha spidi ya kuendeleza utalii wetu au kuboresha spidi ya uwekezaji. Mwekezaji anakuja katika taifa letu, amekuja na mtaji, anakuja kupambana na Sheria ya Labour ambapo yeye anataka kuja na mke wake lakini sheria inamkatalia asije na mke wake au anapata usumbufu kupata permit ya kuishi na mke wake. Sasa unakuta vitu kama hivi vinakuwa vinakinzana, tusipoziangalia sheria na sera zetu, bado hatutaweza kuutelekeleza huu Mpango kwa wakati kama ambavyo tunatarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukajifunza kutoka kwenye Sekta ya Madini, namna ambavyo madini yamechangia kwenye maendeleo yetu katika Mpango wa Pili, ni kwa sababu pia yalifanyika mabadiliko makubwa ya kisheria kwenye sheria za madini na ile ikatusababisha tukaenda vizuri. Kwa hiyo, ushauri ni kwamba tunaomba sheria na sera nazo ziangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kujua kwamba tuna mkinzano wa kisheria na mipango yetu utaona mara nyingi sana mambo yetu mengi yanakwenda kwa waraka, matamko, yanakuwa kama ya zimamoto hivi. Kwa sababu kama sheria ingekuwa inakwenda sawasawa na mipango, hivi vitu vya zimamoto, kwenda kwa matamko na nyaraka visingekuwa vinakwenda namna hii. Hii inaonesha namna gani sheria yetu inawezekana haiko sawasawa na mipango ile ambayo tunaiweka. Kwa hiyo, tujitahidi kubadilsiha sheria zetu na tujitahidi kuangalia mabadiliko makubwa kwenye sera zetu ili tuweze kwenda sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wetu unatakiwa ujengwe sasa kwa misingi ya soko. Tusitengeneze tu mpango kwamba tulime mazao haya zaidi, tulime kitu hiki au kile zaidi, hebu tuangalie soko lina uhitaji gani. Kama tunasema tuna uhitaji mkubwa wa mafuta ya alizeti, huko ndiko sasa tutengeneze mpango namna gani tunawashawishi wakulima ili waweze kulima alizeti na namna gani tunatengeneza sheria ambayo itazuia uingizaji wa mafuta ya alizeti kwenye nchi yetu ili soko letu la ndani lenyewe lianze kuwa ni soko kabla hatujategemea soko la nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, lazima …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Kengele imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)