Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya. Kwa mwelekeo wa bajeti hii inayoonesha wazi Serikali imedhamiria kuboresha elimu kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze uamuzi wa Serikali kuhamishia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) kuhamishwa Wizara ya Elimu kwa dhana ya dhamira ya kuvifanya vyuo hivi kutoa elimu ya ufundi, jambo hili litasaidia sana kuwezesha vijana wetu wengi ambao hawajapata fursa ya elimu ya sekondari wapate elimu ya ufundi ambayo wataweza kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo hivi kwa muda mrefu vimekuwa vikiendeshwa katika mazingira magumu sana, vimekuwa havipati fedha za kutosha, dhamira ya kutoa elimu imefikiwa kwa kiasi kidogo.
Sasa Serikali iongeze bajeti kwenye vyuo hivi viweze kutoa elimu bora na wanafunzi bora, yale maeneo ambayo hayana vyuo hivi vya FDC‟s basi Serikali ijenge vyuo vya VETA. Mfano ni Jimbo langu la Kilindi halina FDC‟s wala VETA japo kwa mwaka wa fedha unaoanza Julai 2016 Serikali imedhamiria nasi tupate chuo cha VETA. Naomba nipate uthibitisho wa dhamira ya Serikali katika hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie juu ya upungufu wa walimu katika shule zetu za msingi na Serikali, japo Serikali kwa sasa inaonesha kutatua tatizo hili hususani katika masomo ya sayansi, hisabati, fizikia na kadhalika. Mfano, katika Jimbo langu la Kilindi shule za sekondari Mafisa, Kibirashi, Kikude hazina walimu wa kutosha, nitaleta ofisini kwa Mheshimiwa Waziri upungufu wa walimu ili Serikali ione namna ya kutatua tatizo hili vinginevyo kiwango cha elimu katika Wilaya ya Kilindi kitashuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nieleze juu ya suala la Maafisa Elimu na Walimu kukaa katika eneo moja la kazi. Jambo hili kwa kweli halileti ufanisi katika utendaji. Mtumishi kukaa eneo moja kwa muda mrefu kunamfanya mtumishi kutojifunza changamoto na morali ya kazi kwa mfano, katika Jimbo langu la Kilindi, Afisa Elimu Sekondari na Elimu ya Msingi wamekaa muda mrefu, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI, tupate watumishi wapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba suala la Wilaya kupata High School lipo chini ya Serikali za Mitaa lakini bado Wizara hii inalo jukumu la kusimamia Wilaya ambazo hazina kabisa shule za kidato cha tano na cha sita zinapewa fursa hizo. Mfano katika Wilaya yetu ya Kilindi hatuna hata shule moja, hii inanyima fursa kwa vijana ambao wazazi wao hawana uwezo kujiunga na shule ambazo zipo mbali na Wilaya ya Kilindi. Wazazi, uongozi wa maeneo hawana nguvu za kiuchumi. Wanafunzi wanachaguliwa mbali na Wilaya ya Kilindi mara nyingi hawaendi. Wizara ituone nasi, itusogezee shule ya wavulana na wasichana katika ngazi za kidato cha tano na cha sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake ya kutoa elimu bure kwa wananchi. Wananchi wa Tanzania na wa Kilindi wamenufaika sana na fursa hii. Naunga mkono hoja.